Mwanamume aliyempata mama yake mzazi miaka 58 baada ya kuasiliwa

tt

Chanzo cha picha, TIMOTHY WELCH

Iliyochapishwa

Timothy Welch alikuwa mmoja wa maelfu ya watoto waliotolewa na mama zao ili kulelewa katika nyumba ya akina mama na watoto katika miaka ya 1960 nchini Uingereza.

Alikuwa na umri wa wiki sita tu alipotenganishwa na mama yake mzazi, June Mary Phelps, aliyekuwa na umri wa miaka 18 wakati huo.

Timothy, mwalimu wa London mwenye umri wa miaka 59, alilelewa na wazazi wake walezi Bill na Eunice.

"Wazazi wangu waliokua waliniambia kila wakati 'wewe ni maalum, ulikuja kwetu kwa njia tofauti'.

"Hawakujaaliwa kupata watoto wao wenyewe, kwa hivyo walianza mchakato wa kuasili na wakiwa na umri wa miaka 36 walinichukua."

Timothy alielezea maisha yake na wazazi wake waliomlea kama ya"furaha sana" , na aliishi bila kufikiria kumtafuta mama yake mzazi hadi wazazi wake wa kumlea walipokufa: Bill mnamo 2018 na Eunice mnamo 2020.

Timothy na wazazi wake walezi, Bill na Eunice.

Chanzo cha picha, TIMOTHY WELCH

Maelezo ya picha, Timothy na wazazi wake walezi, Bill na Eunice.

"Kama mtoto wa kuasiliwa kila wakati unaingiwa na mawazo ya kutafuta familia yako ya kuzaliwa, lakini kuchukua hatua au kutoifanyia kazi mawazo hayo ni suala jingine," Timothy alisema.

"Mawazo mengi yaliyonijia akilini yalihusiana na utambulisho wangu. Nilijiuliza mimi ni nani, tabia fulani katika utu wangu ambazo zilikuwa tofauti na familia yangu ya kuasili."

"Wazazi wangu walezi walikufa, ilinifanya nijisikie tofauti kuhusu ulimwengu na kujihusu mimi binafsi."

"Mshauri mmoja aliniambia kwamba wazazi wa kulea wanapofariki, mara nyingi watu huwa na hamu ya kutaka kujua kuhusu urithi wao wenyewe, kwa sababu sote tunatafuta uhusiano."

"Nadhani hiyo ndiyo ilikuwa hali yangu. Inakupa nafasi ya kufikiria: sasa itakuaje?"

"Baba yangu mlezi aliniambia kuwa nilipokuwa mtoto nilimwambia, 'Natumai mama yangu mzazi yuko sawa, nadhani ni mrembo na ninaelewa kwa nini hakuweza kukaa nami."

Chanzo cha picha, TIMOTHY WELCH

Maelezo ya picha, "Baba yangu mlezi aliniambia kuwa nilipokuwa mtoto nilimwambia, 'Natumai mama yangu mzazi yuko sawa, nadhani ni mrembo na ninaelewa kwa nini hakuweza kukaa nami."
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Timothy alianza kumtafuta mama yake mzazi mnamo Januari 2022, baada ya kupitia picha za zamani za familia.

"Nilipata picha ya mahali nilipozaliwa: Yateley Haven, Hampshire (Uingereza)," alieleza.

"Nilipokuwa nikipekua mitandao niligundua kuwa kulikuwa na kikundi cha Facebook kilichofunguliwa kwa ajili ya familia za akina mama na watoto ambao walizaliwa huko."

"Nilituma ombi la kujiunga na kikundi na msimamizi, Penny Green, aliwasilian nami na kuniuliza hadithi yangu."

"Kama mwanahistoria mahiri, alipendezwa sana na akajitolea kunisaidia kutafuta wazazi wangu walionizaa."

Penny Green, mfanyakazi wa zamani wa kutoa misaada kutoka Bedfordshire, aliunda kikundi cha Facebook kwa ajili ya watu waliozaliwa au kuwa na ushirika na The Haven, makazi ya akina mama na watoto Uingereza inayoendeshwa na Kanisa la Baptist, kwani yeye mwenyewe pia ni mzaliwa wa huko.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 62 alieleza kuwa akina mama wasio na waume waliomba kwenda huko kujifungua na watoto wao walitolewa kwa ajili ya kuasili, mara nyingine bila hiari yao.

"Nadharia ya wakati huo ilikuwa kwamba walikuwa wakiwasaidia akina mama wasio na waume, kwa sababu ilikuwa jambo la fedheha kuwa mama bila ya kuwa na mume," alisema.

Kulingana na Jumuiya ya Yateley, The Haven ilifunguliwa kutoka mwaka 1945 hadi 1970, na karibu watoto 1,800 walizaliwa huko.

Mamake Penny alikuwa na umri wa miaka 36 alipopelekwa huko na wazazi wake, kwa vile alikuwa mseja na mjamzito.

Penny Green alisaidia sana Timothy kupata familia yake ya kuzaliwa.

Chanzo cha picha, PENNY GREEN

Maelezo ya picha, Penny Green alikuwa kiungo muhimu sana kwa Timothy kupata familia yake asili.

Tofauti na akina mama wengi wachanga, hata hivyo, alikataa kumuacha binti yake. Kulingana na Penny, mama yake ndipo alipobadilisha jina na kuwaambia watu kuwa alikuwa ameolewa, lakini baba wa mtoto huyo alikufa katika ajali ya barabarani.

Timothy pia anaamini kwamba mama yake alikuwa mwathirika wa kupokontwa mtoto kwa lazima, kusababu alikuwa mdogo sana.

"Juni hakuwa na chaguo, hasa ikiwa alitaka kuendelea kufanya kazi. Ningejikimu vipi bila kazi?"

Penny alisema kwamba ingawa baadhi ya akina mama huko The Haven walijua watoto wao walikuwa wakichukuliwa, hawakuambiwa ni lini au wangeweza kuaga.

"Mama alimtengezea mtoto wake kitu cha kichezea ili ampatie wakati atakapochukuliwa, lakini kwa vile hakuambiwa atachukuliwa lini, hakuwahi kumpa."

"Baadhi ya akina mama walikuwa na kiwewe kiasi kwamba walikuwa wamejificha na waliogopa sana kuibua yaliyopita."

Kufuatia ushauri wa Penny, Timothy aliomba Ofisi ya Msajili Mkuu kupata nakala ya cheti chake halisi cha kuzaliwa, ambacho kiliorodhesha jina kamili la mama yake mzazi, tarehe na mahali alipozaliwa.

Kisha, Penny alitumia orodha ya wapiga kura na mtandao wa Intaneti kumtafuta.

Baada ya Penny kufanya mawasiliano ya kwanza kwa niaba yake, Timothy alipata mume wa sasa wa mama yake, Michael Mortimer.

Timothy alimpatia Mortimer barua pepe yake, ambayo aliituma kwa ndugu zake Timothy na wakapanga siku ya kukutana London.

"Katika haya yote nimehisi msaada wa ndugu zangu ambao umekuwa wa ajabu."

Chanzo cha picha, TIMOTHY WELCH

Maelezo ya picha, "Katika haya yote nimehisi msaada wa ndugu zangu ambao umekuwa wa ajabu."

"Wote wawili ni watu wazuri: wema, wa kujali," alisema.

"Ninajihisi kuwa mwenye bahati sana kuwa nao katika hatua hii ya maisha na nitafurahi sana kuwafahamu wao na familia zao."

"Kikubwa kwangu ilikuwa kukutana na mpenzi wa Chris Amanda na mpenzi wa Greg Gemma na baadhi ya watoto wao, ambao wote ni wazuri."

Baada ya kutengana kwa miaka 58, Jumamosi, Septemba 19, 2022, Chris na Greg walimchukua Timothy ili kuungana na mama yake mzazi.

"Ilikuwa mara yangu ya kwanza kujiona machoni mwa mama yangu," alisema.

"Ulikuwa wakati uliyogubikwa hisia, lakini ulikuwa mzuri sana."

"Tulizungumza mambo mengi, lakini kilichonivutia zaidi ni kumwangalia na kumwonyesha jinsi alivyo."

Timothy alieleza kwamba licha ya matatizo yake ya afya, mama yake anamkumbuka vyema na jinsi alivyokuwa akipenda kula kama Mwana Olimpiki.

Timothy mwenyewe

Chanzo cha picha, TIMOTHY WELCH

Timothy alisema tangu mkutano huo, ameaanza kuweka pamoja maelezo kuhusu maisha yake ya utotoni.

"Mama yangu alikuwa na umri wa miaka 17 alipopata ujauzito na miaka 18 aliponizaa. Alikuwa na mtoto mwingine wa mwaka mmoja hivi ambaye alijifungua, akiwa na umri wa miaka 16. Mtoto huyo aliasiliwa na hajawahi kumuona tangu wakati huo," alielezea.

"Alikuwa mtoto wa mwisho kati ya watoto watatu: alikuwa na dada, Audrey, ambaye alimzidi umri kwa miaka kumi, na kaka, Bill, mwenye umri wa miaka minane. Bado yu hai."

"Baba yangu aliitwa Hedayat Mamagan Zardy na alikuwa raia wa Iran. Walichumbiana kwa muda mfupi na walipenda kucheza dansi usiku nyakati za huko Oxford."

"Juhudi za kumtafuta baba yangu mzazi na kaka yangu mkubwa ziko katika hatua za awali sana."

Timothy anaeleza kuwa June alioa mwaka 1966 na kupata watoto wengine wawili, kaka zake, ambao sasa anawasiliana nao.

Akitafakari juu ya uzoefu wake wa kutafuta familia yake, Timothy alisema: “Unapaswa kuwa na mawazo huria na ukakamavu wa hali ya juu.

"Nitaenda kumtembelea mama yangu na natarajia kukutana naye mara kwa mara kadri muda unavyokwenda."