Waridi wa BBC: “Siku ya tano baada ya ajali mguu wangu ulianza kuoza”

Chanzo cha picha, Consololata Waitherero
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
Kila kukicha katika maisha yake Consololata Waitherero kwa jina la utani Konsah kutoka nchini Kenya , ni siku mpya ambayo anaitazama kama neema kuwa hai . Akiwa na miaka 25 sasa anasema kwamba tangu alipopata ajali mbaya ya barabarani iliyosababisha kukatwa kwa mguu wake wa kulia alianza kuwa na mtazamo mpya kuhusu Maisha nini hasa.
Siku ya Ajali
Siku ambayo Konsah anasema hatawahi isahau kamwe ilikuwa mnamo mwezi Aprili mwaka wa 2021 , alikuwa ni mjasiriamali aliyekuwa anashughulika na mgahawa mmoja katika mtaa aliokuwa anaishi viungani mwa mji mkuu Nairobi,
“Siku hio nilikuwa na miadi ya kuzuru soko, kununua bidhaa mbalimbali za mapishi kwa wateja wangu, na kama kawaida basi nilijibidiisha na kuhakikisha kwamba mzigo wangu ulikuwa na kila aina ya bidhaa ya mapishi ,kwa kuwa nilikuwa na mzigo niliamua kuchukua usafiri wa bodaboda”anakumbuka Konsa
Anakumbuka akiabiri bodaboda mwendo wa saa kumi na moja hivi jioni akielekea nyumbani , ila simulizi yake inakumbwa na huzuni kwani anasema kwamba safari yake ilikatika ghafla baada ya bodaboda aliyokuwa ameabiri kugongwa kwa upande wa nyuma na gari lililokuwa linakimbia kwa kasi mno
Konso anasema kwamba alipoteza fahamu kwa dakika kadhaa na alipojaribu kuamka kutoka Eneo la ajali aligundua kuwa mguu wake wa kulia ulikuwa umevunjika na akasalia amelala barabarani bila uwezo wa kutembea .
“Matukio ya siku ya ajali hio , bado ni kama sinema katika mawazo yangu , ninakumbuka watu wengi wakinizingira , wengine walikuwa wanapiga mayowe huku wengine wakijaribu kila wawezalo kunisukuma kando ya barabara ”anakumbuka Konsah

Chanzo cha picha, Consololata Waitherero
Mwanadada huyu anasema kwamba dereva wa bodaboada aliyekuwa amembeba alifariki papo hapo , hadi wa leo hafahamu mengi kuhusu Maisha ya dereva wake ila anasononeka kwamba yeye alinusurika ila dereva wake alifariki.
Hatua ya kukatwa mguu wake wa kulia
Konsah anasema kuwa baada ya ajali alikuwa na uchungu mwingi mno na alikuwa anatokwa na damu nyingi , anakumbuka alikimbizwa kwenye hospitali ya kwanza ambako hakufanyiwa chochote bali huduma za dharura za kuokoa Maisha kwani anasema hospitali aliyowasilishwa kwanza walihitaji pesa taslimu, baadaye alihamishwa hadi hospitali mmoja kuu nchini Kenya.
“Ilikuwa ni siku ya tano baada ya ajali, mguu wangu ulikuwa umefungwa, niligundua kuwa ulikuwa unanuka vibaya huku ukitoa madudu iliyoashiria mguu ulikuwa umeoza kabisa , ”anasmea Konsah

Chanzo cha picha, Consololata Waitherero
Mwanadada huyu anasema kuwa ni wakati huo ilipoamuliwa kuwa hakuwa na wakati mwingi wa kuishi kwani ishara za mguu kuoza kuliashiria kuwa maisha yake yalikuwa hatarini .
Japo kwa uchungu na hofu Konsah alikubali mguu wake wa kulia ukatwe kuanzia sehemu ya magoti , anasema kuwa watabibu walimweleza kuwa hio ndio ilikuwa njia ya kipekee ya kunusuru Maisha yake hatarini.
Kukubali hatma ya kuishi bila mguu

Chanzo cha picha, Consololata Waitherero
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Imekuwa ni karibu miaka miwili sasa tangu Konsah kuanza kuishi Maisha mapya bila mguu wa kulia , anataja mabadiliko ya Maisha yake kama mwamko mpya ambao ulijaa panda shuka za kuanza kujifunza mambo upya.
“Kupoteza mguu wangu kulimaanisha kuwa ningeanza kufanya mambo niliyoyafahamu kwa njia mpya, pia ilibidi niwekwe mguu bandia kunisaidia kutembea.” anasema Konsah
Kuishi na Mguu bandia kulikuja na uzuri na pia changamoto, Konsah anasema kuwa changamoto ya kwanza na ambaye alifaulu ni kukubali hatma yake ya kuwa kamwe hatakuwa na mguu wa kulia , Mwanamke huyu anasema kwamba haikuwa rahisi .
“Kwa miezi 8 nililia kila siku juu ya kupoteza mguu wangu , niliishi miezi hio nikitafakari mguu wangu na jinsi Maisha yatakavyokuwa ,”
Lakini sasa Konsa amejikubali alivyo , kwenye mitandao ya kijami kwa mfano Instagram ,tiktok na mitandao mengine utampata kule akifanya mazoezi , akiigiza na hata akipiga densi kama sehemu ya Maisha yake mapya na mguu wake bandia.

Chanzo cha picha, Consololata Waitherero
Mwanadada huyu amekuwa sehemu ya kutia wengi moyo hasa watu wazima ambao kupitia ajali za barabarani au za nyumbani hujipata wamepoteza viungo vya mwili ghafla .
Konsah hajakata tamaa na anasema kwamba kujikubali ilikuwa hatua ya kwanza ya kupona, sasa anaishi akifahamu kuwa Maisha ni Zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu , amejifunza kuishi kila dakika kana kwamba ni ya mwisho lakini kwa kufanya mambo chanya katika jamii yake .
Mmmojawapo wa changamoto kubwa ambayo anapitia kuhusiana na kuishi na mguu bandia ni kwamba ni lazima awe mwangalifu asinenepe au asipunguze uzito chini ya kiasi ambacho mguu huo unaweza kuhimili. Konsah anasema kuwa sio wengi ambao wanamudu kununua miguu bandia kwani bei yake sio nafuu kwa hivyo kwake anahakikisha anafuata maagizo ya mguu wake.
Huvalia mguu bandia katika shughuli zake za kikazi na akiwa nje ya anakoishi ila anaporudi nyumbani na inawadia wakati wa kulala mguu bandia hutolewa kupanguswa tayari kwa siku mpya.












