Waridi wa BBC: 'Ninajivunia kuwa mchezaji wa timu ya Tanzania ya tenisi ya kiti cha magurudumu

Chanzo cha picha, Lucy Shirima
- Author, Martha Saranga
- Akiripoti kutoka, Tanzania
- Author, Niambietz
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Kwa walio wengi ulemavu huonekana kama laana ama kutokuwa na bahati na kuwafanya kukosa kujiamini na hata kukata tamaa ya maisha. Lakini Lucy Shirima ameikubali hali ya ulemavu wa viungo aliyozaliwa nayo na kuamua kupambania maisha yake.
'Nilitamani kuwa mwanajeshi nchini Tanzania, lakini kutokana na hali ya ulemavu wa viungo niliyo nayo isingewezekana' alisimulia Lucy Shirima ambaye ni mkazi wa jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania.
Alipataje ulemavu?
Lucy mwenye asili ya mkoa wa Kilimanjaro kaskazini mwa Tanzania, anasema alipomaliza kidato cha nne mwaka 2017, ndipo alipoelewa rasmi na kusimuliwa namna alivyo pata ulemavu huo.
''Mimi nimelelewa upande mmoja wa mama tu mpaka nimekua, hii iliniumiza sana. Nilipofika miaka 17 hivi nilianza kuuliza uliza kwanini mimi nipo hivi...awali sikupewa majibu maalumu iliniumiza sana'' anasimulia.
'Ninakumbuka 2017 mama mkubwa ambaye alinilea wakati wote alinisimulia kwamba nilizaliwa hivi kutokana na mama yangu kupendelea kuvaa mavazi ya kubana akiwa na ujauzito wangu' anaeleza kuwa hizo ni simulizi tu alizopewa kuhusu mama yake ambaye hakubahatika kumuona.
'Hata hivyo baadaye nilikubaliana na hali na kuamua kupambana na maisha yangu nikilenga kufaulu na kufikia maisha mazuri'.
'Bado baadhi ya watu wana fikra potofu kuhusu watu wenye ulemavu'

Chanzo cha picha, Lucy Shirima
Lucy anasema tangu amejiunga na mchezo wa tenisi ya kiti cha magurudumu amekuwa akikutana na baadhi ya watu wanaojaribu kumvunja moyo kwa kumuonesha kwamba hawezi.
'Wengi wetu tunakuja wenyewe kufanya mazoezi hatutegemei kubebwa kuletwa mazoezini' alieleza Lucy
'Mimi ninajikubali sana, wala sikati tamaa licha ya baadhi ya watu kutaka kunionesha kwamba siwezi, lakini siyo kweli walemavu tunaweza kufanya mengi tu hasa tukiwezeshwa tunaweza kufika mbali' anaeleza.
Lucy anasema miundo mbinu isiyo rafiki kwa walemavu ni moja kati ya mambo yanayomsikitisha kwenye jamii.
''Kuna wakati ninakwenda kumuona kiongozi kwenye ofisi mtaani kwetu, ninakuta kuna foleni, pia kuna ngazi ambazo siwezi kupanda wala sikubali kubebwa kuingizwa ndani kwani ninaona kama ni aina pia ya uyanyasaji, inanibidi kumsubiri amalize kuhudumia watu ndipo anifate nje baada ya muda mrefu'' anaeleza
Lucy anatamani mazingira ya ofisi na maeneo ya umma yazingatie miundo mbinu rafiki kwa watu wote wakiwemo wenye ulemavu.
''Haki sawa kwa wote iwe sawa kweli ili itupe urahisi pia wenye ulemavu kuona hatujatengwa na siyo kusumbua watu kutusaidia'' anasisitiza.
Mwanamichezo bingwa wa tennisi
Lucy ambaye anasema bado hajaolewa wala hana mtoto anajiskia vizuri kwamba tangu amejiunga na mchezo huu wa tenisi amekuwa mwenye furaha na kuhamasisha vijana wengine kwenye jamii.
'Ninafurahi ulemavu umenipa maisha kwa kuwa ninajishughulisha na michezo ninapata kipato na kujitegemea kimaisha' anaeleza Lucy
Anajivunia kuwa mtu mwenye ulemavu na mchezaji wa timu ya taifa ya tenisi ya kiti cha magurudumu kwa kingereza wheelchair tennis na kuwa kioo kwa jamii.
'Walemavu tunaweza kuishi na kupambana kama watu wengine tunapopewa nafasi na hasa miundo mbinu inapokuwa rafiki kwetu. Mimi ni mfano hai kwani mchezo huu ni mzuri kwangu pia ni rahisi kwa mlemavu yoyote kucheza na watu wenye ulemavu wengi duniani wanaucheza.
Nimefanikiwa kucheza tenisi ya kiti cha magurudumu katika nchi mbalimbali kama, Afrika kusini, Uturuki, Nigeria, Kenya, Ghana na Rwanda.

Chanzo cha picha, Lucy Shirima
'Ninatamani kuwa kama Naomi Osaka katika mchezo wa tenisi duniani'
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa Lucy Shirima ulemavu haukuwa sababu ya kukata kiu yake ya kuwa mwanamichezo bingwa wa tennis duniani akimuhusudu Mjapani Naomi Osaka anayeshikilia nambari moja kwa upande wa wanawake.
Naomi Osaka ni mchezaji wa tennis maarufu kutoka Japan mwenye asili ya Japan na Haiti. Ni mmoja kati ya wachezaji bora wa tenisi duniani kwa upande wa wanawake na amekuwa maarufu si tu kwa umahiri wake uwanjani, bali pia kwa kutambua na kujali masuala ya kijamii na haki za binadamu.
''Ni mchezo ambao umeweza kunikutanisha na watu wenye ulemavu kutoka sehemu mbalimbali duniani na kutufanya tuwe na furaha, uthubutu, kujiamini, kujipenda zaidi, hali kadhalika kutimiza ndoto zetu'' anafafanua.
Lucy anasema kila mara akikutana na watu wenye ulemavu huwa anawaelimisha na kuwaambia kuwa ulemavu sio mwisho wa maisha.
''Watu wenye ulemavu tunakwama pale tunapojikataa kuhusu hali yetu''.
Anasema kwa sababu ameshajikubali mara zote akikutana na fursa hakai nyuma wala kujinyanyapaa.
''Dunia ya sasa ina mtaka mtu mwenye kitu ajitokeze, ili imsaidie. Sasa mlemavu akijikubali akaonesha alichonacho anakubalika' anasema Lucy.
Imehaririwa na Leonard Mubali












