Urusi yaishutumu Ukraine kwa kujaribu kumuua Putin
Urusi imesema ndege mbili zisizo na rubani zilishambulia Ikulu ya Kremlin mjini Moscow jana usiku katika kile inachodai kuwa ni jaribio la Ukraine la kumuua Rais Vladimir Putin.
Ikulu ya Kremlin ilidai kuwa ndege mbili zisizo na rubani zilitumiwa katika shambulio hilo lakini zilikabiliwa na kuzimwa na ulinzi wa Urusi.
Bw Putin hakuwa Kremlin wakati huo na hakukuwa na uharibifu wowote wa majengo, mashirika ya habari ya Urusi yaliripoti.
Picha ambazo hazijathibitishwa kwenye mitandao ya kijamii ya Urusi zilionyesha moshi katikati mwa Moscow.
Ukraine bado haijatoa maoni yoyote kuhusu madai hayo.
Kremlin imelitaja tukio hilo kuwa "kitendo cha kigaidi kilichopangwa" na kusema kwamba ina haki ya kujibu wakati na jinsi inavyoona inafaa, shirika la habari la RIA liliripoti.
"Kremlin imetathmini vitendo hivi kama kitendo cha kigaidi kilichopangwa na jaribio la kumuua rais katika mkesha wa Siku ya Ushindi, Gwaride la Mei 9," RIA ilisema.
Bw Putin hakujeruhiwa na ratiba yake itaendelea kama kawaida, ilisema taarifa hiyo. Vipande vya droni vilikuwa vimeanguka kwenye eneo nje ya Kremlin lakini hakuna mtu aliyejeruhiwa, ilisema.
Ofisi ya rais wa Ukraine iliiambia BBC kuwa haitoi maoni yoyote kwa wakati huu.
















