Waziri Mkuu aliyemvutia Trump ambaye sasa nguvu zake zinaporomoka

c
    • Author, Nick Thorpe
    • Nafasi, BBC
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orban ameushambulia kwa nguvu zake zote mtazamo wa ulimwengu wa kiliberali kwa angalau miongo miwili, na kuibadilisha nchi hiyo kuwa kile alichokiita "demokrasia isiyo ya kiliberali" na taifa la "uhuru wa Kikristo."

Hilo limewavutia watu wanaomuhusudu duniani kote, akiwemo Naibu Rais wa Marekani JD Vance na Waziri Mkuu wa Georgia, Irakli Kobakhidze. Na Rais wa Marekani Donald Trump amemuita Orban "mwerevu" na "mwenye nguvu."

Kabla ya uchaguzi ujao wa Hungary wa Aprili 2026, jumuiya ya LGBTQ inaonekana kuwa miongoni mwa walengwa wa chama cha Orban cha Fidesz. Chama hicho kiliweka sheria mpya iliyotaka kupiga marufuku maandamano ya watu wa jamii hiyo. Lakini watu 100,000 hadi 200,000 walijitokeza mwezi uliopita - kutoka 35,000 wa mwaka jana.

Umati mkubwa wa watu uliandamana Budapest kusherehekea mapenzi ya jinsia moja, uhuru wa kujieleza na haki ya kukusanyika.

Nguvu ya Orban kwa sasa iko katika tishio, lakini sio kutoka kwa watu ambao unawafikiria. Wala kitisho hicho hakitoki upande wa mrengo wa kushoto (liberali), bali ni kutoka mrengo wa kati kulia.

Mpinzani wa kushangaza

ed

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Peter Magyar alionekana kama mpinzani wa ghafla kuanzia Februari 2024

Peter Magyar, mwenye umri wa miaka 44 ambaye zamani alikuwa mfuasi wa Orban, amaibuka kama mpinzani wa ghafla mwezi Februari 2024.

Ni baada ya kashfa iliyohusisha uamuzi wa kumsamehe mwanaume aliyepatikana na hatia ya kuficha unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto, ambao ulipelekea Rais Katalin Novak kujiuzulu kupitia tangazo mubashara katika televisheni.

Waziri wa Sheria Judit Varga (mke wa zamani wa Magyar) pia alijiuzulu - na kashfa hiyo ilileta pigo kwa Orban anayedai kusimama maadili ya jadi ya familia.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Magyar alifanya mahojiano marefu na Partizan, chaneli ya upinzani ya YouTube, na kuzungumzia kile alichokiita upendeleo na ufisadi wa chama tawala.

Robert Puzser, mwanaharakati wa upinzani ambaye anaongoza vuguvugu jipya lisilo na chama liitwalo Citizens Resistance, anasema Magyar anafanya harakati zake kwa uangalifu, huku maafisa wa Fidesz na baadhi ya vyombo vya habari vikijaribu kumsema kuwa ni mliberali au mtu wa mrengo wa kushoto.

Magyar, anasema, anajaribu kuepuka kujitenga na wafuasi wake wa mrengo wa kihafidhina walio mashinani, ambako ndiko kuna ufuasi mkubwa wa Orban.

Kura nyingi za maoni za kitaifa zinakiweka chama cha Tisza, chama kikuu cha upinzani nchini Hungary kinachoongozwa na Magyar, kuwa juu kwa 9% na 18%, mbele ya chama cha Orban. Ni Taasisi moja tu ya fikra tunduizi inayoiunga mkono serikali iitwayo Viewpoing Institute, ambayo bado inakiweka chama cha Fidesz mbele kidogo.

Mambo yanayohusu hospitali za serikali, shule za serikali, na reli za serikali yote yanatumiwa dhidi ya Orban na Magyar na chama chake.

Sasa, mikakati ya muda mrefu ya Orban, ambayo ilipendwa sana hadi nje ya nchi, inaanza kushindwa nyumbani - na Hungary iko karibu zaidi kuliko wakati mwingine wowote kumuondoa mtu aliyetawala kwa miaka 15 sasa.

Mikakati wa Orban

dc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Maelfu ya watu walijitokeza Budapest katika maandamano ya LGBQ na kukaidi marufuku iliyowekwa

Orban yuko katika serikali kwa miaka 19 tangu kuanguka kwa Ukomunisti miaka 35 iliyopita mwaka 1990, na kumfanya kuwa mmoja wa viongozi mwenye uzoefu zaidi katika Umoja wa Ulaya.

Mwanzoni mwa miaka ya 1990, Fidesz kiliachana na mizizi yake ya kiliberali, na Orban akaanzisha utambulisho mpya wa kihafidhina, utaifa, wa mrengo wa kulia.

Mwaka 2015, wageni walipokuwa wakisafiri kwenda Ulaya kuomba hifadhi, Orban alisema ni sehemu ya "vuguvugu la wahamiaji linalojumuisha wahamiaji wa kiuchumi, wakimbizi na pia wapiganaji wa kigeni."

Amepinga kuiunga mkono Ukraine kijeshi tangu uvamizi wa Urusi wa mwezi Februari 2022, na pia anapinga ombi la Ukraine la kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Msingi wa mikakati ya Orban ni katika uwezo wake wa kutambua kile ambacho wapigakura wake wanakiogopa. Ametumia mkakati huo kwa kila ushindi wake wa kishindo, kuanzia mwaka 2010, 2014, 2018, na 2022.

Utafiti wa maoni ya umma uliofanywa na Publicus kuanzia tarehe 23-25 Juni uligundua 45% ya watu waliunga mkono maandamano ya wapenzi wa jinsia moja huko Budapest na 48% walipinga. Lakini ni 8% tu ya wapiga kura wa chama cha Fidesz ndio waliunga mkono, kwa hivyo alipinga ili kuwanga mkono wafuasi wa chama chake.

Tangu maandamano hayo, wafuasi wa Fidesz wamechapisha baadhi ya picha za uchochezi kutoka Maandamano ya Budapest, ikiwa ni pamoja na picha za uchi na hadithi ya mtu aliyekamatwa na polisi kwa kupiga punyeto hadharani.

2022, serikali ilipanga kura ya maoni kuhusu ulinzi wa watoto wakati wa uchaguzi mkuu. Maswali yalijumuisha: "Je, unaunga mkono kuruhusu watoto katika shule za umma kushiriki katika masomo yenye mwelekeo wa kingono bila idhini ya wazazi?"

Jumla ya Wahungaria milioni 3.7 walishiriki, huku walio wengi wakipiga kura ya "Hapana." Maafisa wa serikali wamesema matokeo hayo ya kura ya maoni ni udhibitisho kwamba Wahangari wanapinga masuala ya mapenzi ya jinsia moja.

Mshindi wa uchaguzi

d

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Orban ameitawala Hungary kwa miaka 15 iliyopita

Mkakati mwingine wa Orban ni kwamba mshindi anachukua kila kitu. Orban alipoteza mamlaka mwaka 2002 kisha akarejea ofisini mwaka 2010, na katika sheria mpya ya uchaguzi ya 2011 alipunguza Bunge kutoka viti 386 hadi 199 na kufuta duru ya pili ya uchaguzi, na ushindi ni kwa chama chenye kura nyingi tu.

Pia amewateua majaji wanaopendelea chama cha Fidesz katika Mahakama ya Kikatiba na Mahakama Kuu.

Mwaka 2014 alisema "nchi isiyo ya kiliberali" anayoijenga "haipingi kanuni za msingi za uliberali kama vile uhuru ... lakini haifanyi itikadi hiyo kuwa sehemu kuu ya serikali."

Baadhi ya viongozi wa ng'ambo wanaonekana kuvutiwa na mbinu yake, Warepublican wengi wa MAGA wanampenda Orban kwa kukabiliana na utamaduni wa "woke."

Mawaziri wakuu wa Slovakia na Georgia pia wanaonekana kuwa watu wanaovutiwa sana, na wengine ni Alice Weidel wa chama cha Mbadala wa Ujerumani, Geert Wilders wa Dutch Party for Freedom, na Herbert Kickl wa Austrian Freedom Party.

Nyufa zinaanza kuonekana?

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Oraban ana uhusiano mzuri na Putin kama dhamana ya gesi ya bei nafuu ya Urusi na mafuta

Peter Magyar amezuru nchi nzima, akiishambulia serikali kwa hali mbaya katika hospitali, usafiri wa reli na mishahara ya utumishi wa umma ambayo ni kati ya kiwango chini kabisa barani Ulaya.

Anavutia umati mkubwa wa watu, na ziara zake katika hospitali, shule au nyumba za kutunza wazee zinatangazwa moja kwa moja kwenye Facebook, na nyingi zikivutia maelfu ya maoni.

Orban mwenyewe ameanza kufanya makosa fulani, kama kumuunga mkono mgombea mwenye itikadi kali za kizalendo George Simion katika uchaguzi wa rais wa hivi majuzi wa Romania, licha ya historia ndefu ya matamshi mabaya dhidi ya Wahungaria.

Alimchukulia kuwa mshirika muhimu katika Bunge la Ulaya ambako anatoa maoni sawa na ya Orban kwamba, "Ulaya ya Kikristo" iko katika tishio. Lakini Simion ailshindwa katika duru ya pili ya uchaguzi huo.

Kushindwa kwa Orban kuzuia maandamano ya wapenzi wa jinsia moja, baada ya kuwaahidi wafuasi wake hayatafanyika, pia kunaonyesha kudhoofika kwa nguvu zake.

Lakini kubwa zaidi, uchumi wa Hungary, unaotegemea sana soko la Ujerumani, haswa magari ya Ujerumani yanayotengenezwa huko Hungaria, unadorora.

"Orban anaweza kupata kura kutoka kwa wafuasi wake wakuu, ambao ni takriban watu milioni mbili, lakini haitoshi kushinda uchaguzi," anasema Zoltan Kiszelly, mchambuzi wa siasa aliye karibu na chama cha Fidesz.

Chama cha Tisza sasa pia kina wafuasi wapatao milioni mbili. Na zaidi ya Wahungaria milioni tano walipiga kura katika uchaguzi wa 2022, na 69% ya waliojitokeza kupiga kura - hivyo uchaguzi wa Aprili 2026 huenda ukaamuliwa na wale ambao hawajaamua kwa sasa.

Mwaka 2022, huku kukiwa na vita Ukraine, Orban alijionyesha kama mgombea wa "amani", na kudai upinzani utaiingiza Hungary vitani. Ni mbinu iliyompa mafanikio katika nchi, ambayo ina historia ya kuvamiwa na majeshi ya kigeni.

Mwaka 2026, Ukraine inaweza kumsaidia Orban kushinda tena, anaamini Kiszelly.

Hata hivyo ikiwa vita vya Ukraine vitakwisha kufikia wakati huo, Orban anaweza kudai kuwa yeye ni kiongozi wa Magharibi ambaye alionya kwamba Ukraine haiwezi kushinda nguvu ya Urusi.

Au, ikiwa vita vitaendelea, Fidesz itaweka kampeni yake dhidi ya Manfred Weber, kiongozi wa Chama cha Watu wa Ulaya (EPP), ambacho kinaunga mkono misaada ya kijeshi ya Magharibi kwa Ukraine.

"Orban anaweza kujionyesha, kwa mara nyingine tena, kama njiwa wa amani," Kiszelly anaelezea.

Orban pia anaonyesha uhusiano wake mzuri na Rais wa Urusi Vladimir Putin kama hakikisho la gesi ya bei nafuu ya Urusi na mafuta kwa watumiaji wa Hungary.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi