WARIDI WA BBC : 'Niliahidiwa nikifika India nitapewa ajira lakini mambo yakabadilika'

Chanzo cha picha, Susan
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
Simulizi yake Susan Micheal kwa jina la utani ‘Pretty Kind’
Kutoka nchini Tanzania utadhani ni kutoka tamthilia au sinema ila ndio hali halisi ya maisha yake ya hapo awali .
Kati ya mwaka wa 2014 hadi mwaka wa 2017 alisafiri nchini India. Akilini mwake alifahamu kuwa anasafiri kwa ajili ya kupata ajira ambayo ingemlipa pesa nyingi.
Swahiba wake mmoja ambaye walifahamiana kutoka Mwanza Tanzania alimshawishi kwamba badala ya kuteseka na kuhangaika mno kutafuta ajira nchini mwao Tanzania ingekuwa rahisi asafiri India kwa ajira yenye mapato makubwa kila ya kila wiki .
''Tangu utotoni mwangu nilikuwa na ndoto ya kuwa msanii muigizaji , nilifanya juhudi nyingi , ila sikufanikiwa ,wakati ninachukua uamuazi wa kusafiri India ni kutokana na pandashuka nyingi zilizonikumba nikitafuta nafasi za uigizaji nchini Tanzania'' anasema Susan.
Kusafiri India

Chanzo cha picha, susan
Kwa hiyo Susan hakuwa na wasiwasi wowote wa kusafiri. Ni rafiki yake aliyemsaidia pesa ya kutafuta hati ya kusafiri(Passport ) Visa ya usafiri pamoja na vyeti vingine ambavyo vilikuwa vinahitajika kwaajili ya safari hiyo.
Baada ya kuwasili India ndipo ukweli ulianza kudhihirika na ikawa dhahiri kuwa alikuwa ashiriki kwenye biashara ya kuuza mwili.
Mwanadada huyu anasema kuwa sio kitu ambacho alikuwa anategemea wala hakufahamishwa. Ni ukweli uliokuwa mgumu kuukubali mara moja.
Mahangaiko yake yalitokea wakati alipoelezwa kinagaubaga kuhusu kazi ambayo alikuwa aifanye. Anasema alijaribu kukataa ila waliomsaidia kusafiri hadi India walikuwa wanamdai fedha walizowekeza wakati anasafiri India.
Juhudi zake za kujaribu kutoroka ziliambulia patupu siku zilivyozidi kusonga hali halisi ya mambo ilimjia na akawa hana cha kufanya ila kukubali na kuanza kutumika kama kahaba .
Mwanadada huyu anasema kuwa kwa miaka 3 alitumika kwenye kazi ya kujiuza.
Nchini India anasema kuwa baadhi ya wasichana wanaotoka nchi za Afrika huwa wana maeneo mahususi ya kufanyia biashara hiyo .
Kulingana na mwanadada huyu wateja wengi ni wale ambao wanaishi India lakini wanatoka nchi za Afrika.

Chanzo cha picha, Susan
Kurejea Nyumbani
Mwaka wa 2017 ndio wakati Susan alirudi nchini mwao Tanzania , Kwa miaka aliyoishi India alikuwa anaweka akiba ili apate nauli ya kurejea nchini mwake .
Susan anajutia kusafiri japo anasema kuwa imekuwa somo kwake na anachukua kila fursa ambayo anapata kuzungumza na wazazi na wasichana ambao wanashawishika haraka kusafiri nchi za nje.
Susan anasema kuwa kabla ya mtu hajasafiri ni vizuri athibitishe ni ajira gani ambayo anasafiri kuifanya kwani mwisho wa siku huenda mtu akajikuta amehadaiwa au ametumiwa vibaya












