Je siasa za Tanzania zitabadilika kufuatia kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara ya kisiasa?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Ezekiel Kamwaga
- Nafasi, Mchambuzi
- Iliyochapishwa
Macho na masikio ya Watanzania yataelekezwa jijini Mwanza patakapofanyika mkutano mkubwa wa hadhara wa kwanza wa chama cha upinzani nchini Tanzania tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipotoa ruhusa ya kufanyika kwa mikutano hiyo mapema mwezi huu.
Hii si mara ya kwanza kwa Jiji la Mwanza kuwa kitovu cha siasa za Chadema nchini Tanzania. Hadi mwaka 2005, chama hicho kilionekana kuwa na ushawishi katika eneo la Kaskazini mwa Tanzania ambako mwasisi wake, Edwin Mtei – Gavana wa Kwanza mzalendo wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), pamoja na baadhi ya waliokuwa viongozi mashuhuri wa chama hicho walikuwa wanatoka. Uchaguzi wa mwaka 2005 ulioingiza vijana wapya wengi ndani ya chama hicho na kampeni maarufu ya kisiasa iliyojulikana kwa jina la Operesheni Sangara iliyofanyika kuanzia mwaka 2008, ikilenga mikoa ya Kanda ya Ziwa – eneo lenye idadi kubwa zaidi ya watu nchini Tanzania kwa ujumla wake, na maeneo mengine ndiko kulikobadili mustakabali wa kisiasa wa chama hicho.
Sangara ni aina maarufu ya samaki wanaopatikana katika Ziwa Victoria lililo kwenye eneo hilo na jina la kampeni hiyo liliakisi taswira ya wananchi wa mikoa ya upande huo.
Watafiti mbalimbali wa siasa za Tanzania wamekuwa wakielezea mikutano ya hadhara kama “hewa ya oksijeni” ya mawasiliano ya kisiasa hapa nchini. Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, taasisi ya Afrobarometer ilifanya utafiti ambapo asilimia 72 ya waliohojiwa walikiri kuhudhuria walau mkutano mmoja wa hadhara. Kwa wastani, kwa mujibu wa Afrobarometer, asilimia 37 ya Waafrika huhudhuria mikutano ya hadhara ya kisiasa.
Kwa maana hiyo, kuliko mahali pengine popote barani Afrika, Watanzania wengi zaidi huhudhuria mikutano ya hadhara ya kisiasa. Takwimu nyingine muhimu ni kwamba takribani asilimia 60 ya Watanzania hupata habari kupitia njia ya redio na kwa wastani huu, ina maana mikutano husikilizwa na wengi zaidi kuliko hata redio. Ndiyo sababu zuio lililowekwa na Serikali ya hayati John Magufuli mnamo Julai mwaka 2016, lilikuwa na athari zaidi kisiasa kwa Tanzania pengine kuliko kwingine kokote barani Afrika. Na athari ilikuwa kubwa zaidi kwa vyama vya upinzani kwa sababu chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilitumia ziara za Magufuli mikoani na kwingineko kufanya kazi za kisiasa.

Ushawishi wa Rais Samia
Bila shaka, kulikuwa na uwezekano mdogo wa kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara kisiasa wakati huu endapo Rais Magufuli angekuwa hai.
Rais huyo wa Tano wa Tanzania aliamini kwamba siasa zinapaswa kufanyika wakati wa kampeni tu na zikimalizika, chama kilichoshinda uchaguzi kinatakiwa kuachiwa muda wa kutimiza ahadi ilizotoa wakati wa uchaguzi pasipo kukosolewa au kuzodolewa na wapinzani wake.
Mara baada ya kushika hatamu za uongozi, Rais Samia amekuwa akisisitiza kuhusu umuhimu wa kujenga taifa lenye maridhiano, ustahamivu, mabadiliko na ukuaji. Ni katika eneo la maridhiano ya kisiasa ndipo ambapo suala hili la mikutano linapoingia.
Tayari amekutana na viongozi karibu wote wa vyama vya upinzani na ruhusa hii ya mikutano ilikuwa mojawapo ya mambo aliyoshauriwa kufanya na wadau mbalimbali wa siasa za Tanzania.

Chanzo cha picha, CCM
Katika muda wake wa takribani miaka miwili tu madarakani, Rais Samia ameunda Kikosi Kazi Maalumu cha kufanya mapitio ya sheria za Tanzania zinazohusu masuala ya siasa, kuvirejesha vyama vya Chadema na ACT Wazalendo kwenye meza ya mazungumzo kufuatia kulegalega kwa uhusiano kutokana na matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2020 na kupunguza uhasama wa kisiasa ulioanza kumea katika kipindi cha miaka iliyotangulia mwaka 2021.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Nini kinaweza kutokea?
Chama cha Chadema kimetangaza kuanza mikutano yake Januari 21 na ni wazi kwamba vyama vingine kama vile CUF na ACT Wazalendo navyo vitatangaza siku zake za kuzindua mikutano hiyo. Wakati huohuo, wanachama mashuhuri wa upinzani kama vile Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, tayari wametangaza nia ya kutaka kurejea nyumbani.
Lissu anatarajiwa kuwasili wiki ijayo. Jambo la kwanza linaloweza kutokea ni kwamba mikutano ya awali itahudhuriwa na watu wengi. Kwa sababu ya tabia niliyoieleza awali ya Watanzania kupenda mikutano hiyo na kiu waliyonayo baada ya marufuku ya miaka sita, matarajio ni kwamba maelfu watahudhuria mkutano wa Chadema kwenye Viwanja na wengine watafuatilia kwenye vyombo vya habari.
Jambo la pili ni kwamba mikutano hii itatoa fursa kwa watu kusema yaliyo moyoni mwao. Katika Uyunani ya kale, haki ya watu kutoa maoni ilijulikana kama 'Forum internum', ikimaanisha fursa hiyo humpa mtu kuzungumza kile kilichomjaa moyoni mwake. Si kila kitakachosemwa na kuzungumzwa, kitamfurahisha kila atakayeona na kusikia.
Pengine huu ndiyo utakuwa mtihani mkubwa zaidi kisiasa kwa utawala wa Rais Samia. Kwa sasa, dunia inapitia katika wakati mgumu kiuchumi kutokana na athari za ugonjwa wa Uviko 19, ukame uliokabili Afrika na vita inayoendelea nchini Ukraine. Matokeo yake ni kupanda kwa gharama za maisha, ukosefu wa ajira na shida nyingine kwenye jamii.
Kama kuna wakati ambapo vyama vya upinzani vina fursa nzuri ya kuonyesha mapungufu katika tawala zilizo madarakani, huu ni wakati bora zaidi katika miaka ya karibuni. Kwa wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa, huu ni wakati mzuri wa kuona ni kipi kitasemwa na wapinzani na serikali ya Rais Samia itakuja na hoja zipi za kukabiliana na mashambulizi. Zipo taarifa ndani ya CCM kwenyewe wapo wanaodhani hatua ya kuruhusu mikutano imekuja mapema kabla hawajajipanga. Kundi hili lina wanasiasa wanaoamini kwamba kushinda kwao kwenye uchaguzi wa mwaka 2020 kulitokana zaidi na aina ya siasa za wakati huo – zilizokuwa na upendeleo mkubwa kwa chama tawala na zilizokosa ushindani, na kuwa mabadiliko haya yanahatarisha mustakabali wao kisiasa.
Hili ni kundi linalosubiri kwa hamu kumwonyesha Rais Samia “tulikwambia” endapo hitilafu yoyote itajitokeza kwenye siku hizi za awali. Kwenye hotuba yake ya kuruhusu mikutano hiyo, Rais Samia alisema anataraji siasa za kistaarabu zitatamalaki na kwamba wanasiasa watatumia fursa hii kujadili masuala muhimu pasipo kufanya mambo yatakayoharibu amani, utulivu na maadili ya Watanzania.
Kuruhusiwa kwa mikutano hii kumekuja katika wakati ambapo mitandao ya kijamii imeanza kuwa na ushawishi mkubwa kuliko hata vyombo vya habari vilivyozoeleka.
Wakati marufuku inawekwa, bado watumiaji walikuwa wakisubiri vyombo rasmi viripoti na kufanya uchambuzi hali ambayo kwa sasa imebadilika.
Inatarajiwa kuwa ruhusa hii itavizimua vyombo vya habari – rasmi na visivyo rasmi kuandika zaidi kuhusu siasa na kama vyombo rasmi vya habari vitapata namna ya kushindana na mitandao, huenda soko la magazeti, redio na runinga likarejea – hata kama si katika viwango vya miaka 10 hadi 15 iliyopita. Mkutano wa Mwanza ni hatua muhimu katika siasa za Maridhiano zinazopigiwa chapuo na utawala wa Rais Samia.
Mikutano hii itakuwa ni kipimo tosha cha kuona ni kwa jinsi gani vyama vya upinzani vimejipanga kuwa vyama tawala katika miaka ya usoni na chama tawala kiko himilivu kiasi gani kwa mashambulizi na hoja kinzani kutoka upinzani. Lakini, angalau sasa Watanzania wameanza kuelekea katika njia walioanza kuizoea na kuifahamu vizuri. Mpira sasa ni kwa vyama vya upinzani na CCM.















