Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
WARIDI WA BBC : 'Nilijipata nimetekwa na usingizi nilipokuwa nikivuka barabara’
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
Je unaweza kutafakari kuishi maisha ambayo hauna udhibiti wa wakati au sehemu ambayo usingizi unaweza kukupata ghafla ?
Je maisha yako yangebadilika kiasi gani ?
Ugonjwa huu unafahamika kama Narcolepsy
Ndio maisha yalivyo kwa Mary Anne Njuguna mwanamke kutoka Kenya , ambaye tangu alipohitimisha miaka 14 , aligundua kuwa kulikuwa na mabadiliko makubwa kupitia tabia yake mpya ya kusinzia kila wakati bila uwezo wa kujidhibiti .
'Unafahamu kwamba kwa hali hii ya wanaoishi na ugonjwa wa Narcolepys ,dalili na madhara ni ya kipekee kwa kila mgonjwa na sawia na matibabu ambayo utapewa.
Kwa hio nilijipata nikibanwa na usingizi hata wakati nimekaa sebuleni nikipata kiamsha kinywa , anasema Mary Anne Ngugi
Ugonjwa ulianza aje ?
Mwanadada huyu anasema kuwa mahangaiko yake yalianza wakati alipokamilisha masomo ya shule ya msingi .
“Kila asubuhi nilikuwa ninaamka nikiwa na uchovu mwingi kana kwamba sikuwa nimelala usiku kucha , wakati huo sikuwa ninaelewa ni kipi kilikuwa kinafanyika , licha ya kulala usiku ,mchana pia ningeendelea kusinzia' anasema Mary Anne Ngugi
Na kwa hivyo alipojiunga na shule ya sekondari Maisha hayakuwa mepesi kwake , anakiri kuwa alikuwa hana uhusiano mzuri na waalimu wake , kutokana na kushikwa na lepe la usingizi kila wakati hasa akiwa darasani , waalimu hawakumuelewa walidhani ni utundu tu , na yeye pia hakujielewa ni kwanini alikuwa akikabwa na usingizi bila kujizuia .
“ Cha kustajabisha sana nilikuwa nalala nikichukua maelezo darasani ,nilikuwa nagundua kuwa maandishi yangu yalikuwa kama ya mtoto mdogo kwani usingizi uliponibeba nikiandika masomo hayangewezekana tena' anasema
Anaongeza: 'Nilijipata kwenye hali ya aibu hata wakati wa gwaride nikiwa shuleni,nikiwa nimesimama nilikuwa napiga lepe la usingizi '.
Mary Anne anasema kwamba , walimu kwa wanafunzi wenzake walikuwa hawataki kuhusishwa naye , ilichukua miaka 5 kabla ya hali halisi ya ugonjwa uliokuwa unamsumbua kugundulika katika hospitali moja kuu nchini Kenya . Alielezwa kuwa alikuwa na ugonjwa wa Narcolepsy .
Kutafuta matibabu.
Kwa kuwa hali hii ilizidi kumhangaisha Mary Anne alitafuta matibabu ambayo baada ya vipimo iligunduliwa kwamba alikuwa anaishi na ugonjwa wa Narcolepy .
Tangu wakati huo Mary Anne alianza kupitia matibabu mengi yakiwemo ya kumeza tembe za kila siku , anasema kwamba ugonjwa huo umempatia nafasi ya kuuelewa na pia kutafuta mbinu mbalimbali ambazo anaweza kuzitumia kuhakikisha kwamba hategemei dawa za kila siku kuepukana na usingizi wa ghafla .
Kwa mfano anasema kwamba kila siku anahakikisha kwamba anatenga dakika kadhaa za kulała kila baada ya masaa machache mchana ili kuepukana na kupatwa na usingizi bila kutarajia .
Ila anasema kuwa kuna kisa kimoja ambacho hajakisahai maisha mwake , wakati alipojiunga na taasisi mmoja , viungani ma jiji la Nairobi , alikuwa katika pilkapilka za kutoka chuoni .Akiwa kwenye kivukio usingizi ulimpata akiwa anavuka barabara .
Mwanadada huyu anasema kwamba hakumbuki mengi , ila akilini mwake anakelele za honi ya gari ambalo lilikuwa linakuja kwa kasi na mengine hakumbuki ila alijipata kando ya barabara asijue iwapo ni watu walimsaidia kuvuka au ni vipi.
Ndizo mojawapo wa hatari za kuishi na hali hii ya Narcolepsy
Je Narcolepsy ni Ugonjwa upi
Kulingana na wakfu wa ugonjwa wa Narcolepsy nchini Kenya , tatizo hili ni ugonjwa sugu wa neva unaodhihirishwa na dalili za kusinzia kupita kiasi mchana.
Mgonjwa wa Hypersomniac hawezi kukaa macho siku nzima, anaweza kupata hali ya usingizi wa ghafla ambayo hawezi kuepuka (kwa mfano, anaweza kusinzia wakati wa mazungumzo, wakati wa chakula au hata wakati wa kuendesha gari), na anaweza kuwa na shida kubwa ya kuamka asubuhi.
Inaweza kuwa vigumu kwa mgonjwa kukaa macho wakati wa shule au saa za kazi, ambayo inafanya maisha yake kuwa magumu - ikiwa haiwezekani kwa narcoleptic - kutekeleza taaluma fulani ambapo ni muhimu kudumisha umakini kwa muda mrefu.