Maisha yangu kama 'mke wa tano' nchini Niger: Mwanamke aliyepigania haki yake mahakamani na kushinda

Iliyochapishwa

Na Caroline Mwangi & Muktar Sadu Alize

BBC 100 Women

Hadizatou Mani aliuzwa kwa chifu wa eneo hilo nchini Nigeria chini ya utaratibu wa wahaya
Maelezo ya picha, Hadizatou Mani aliuzwa kwa chifu wa eneo hilo nchini Nigeria chini ya utaratibu wa wahaya

Hadizatou Mani-Karoau aliuzwa kwa chifu wa eneo hilo, mwenye umri wa miaka 12 tu, na kuwa wahaya au "mke wa tano".

"Yalikuwa maisha ya kutisha. Sikuwa na haki; si kupumzika, si chakula, hata maisha yangu," anaiambia BBC 100 Women kutoka nyumbani kwake kusini mwa Niger.

Wahaya ni aina ya utumwa iliyoenea katika eneo lake, ambapo wanaume matajiri huwanunua wanawake vijana kwa ajili ya ngono na kazi za nyumbani kwa kiasi kidogo cha dola 200 (£170) na kuwafanya wake wa tano kukwepa sheria ya Kiislamu, ambayo inaruhusu wake wasiozidi wanne.

Bi Mani aliuzwa mwaka wa 1996 na kumiwa kama mtumwa kwa miaka 11. Lakini mateso yake hayakuishia hapo.

Baada ya kuachiliwa mwaka wa 2005 na kuolewa na mwanamume aliyemchagua, mtumwa wake wa zamani alimshtaki kwa chuki kubwa na Bi Mani alihukumiwa na kufungwa jela akiwa mjamzito.

Hatimaye, zaidi ya miaka kumi baadaye, hatia yake ilibatilishwa. Kesi yake ilikuwa ya kihistoria nchini Niger, ambapo utumwa umeendelea licha ya juhudi zinazoendelea za kuuharamisha.

Hadizatou Mani sasa anaishi na familia yake kusini mwa Niger
Maelezo ya picha, Hadizatou Mani sasa anaishi na familia yake kusini mwa Niger

Sasa Bi Mani anaishi maisha yake mwenyewe katika Zongo Kagagi, mji ulio katika eneo la Tahoua kusini mwa Niger, na anaendesha kampeni kwa wanawake wengine kuelewa haki zao na kuepuka utumwa.

Yeye ni mmoja wa wanawake walioangaziwa kwenye orodha ya Wanawake 100 ya BBC, ambayo kila mwaka huwataja wanawake 100 wenye ushawishi na duniani.

Mwaka huu orodha hiyo inaangazia hatua ambayo imefikiwa tangu kuanzishwa kwake miaka 10 iliyopita.

Kesi ya Bi Mani ilikuwa muhimu katika kushinikiza sheria ibadilishwe katika nchi yake.

Hata hivyo licha ya amuzi wa mahakama, na kampeni za Bi Mani, zaidi ya watu 130,000 bado ni watumwa nchini Niger leo hii, kulingana na takwimu za Global Slavery Index.

Mke wa ziada

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Wake wa tano" wanafanywa watumwa na wanaume matajiri katika eneo hilo, na pia hutolewa kama zawadi chini ya desturi inayojulikana kama sadaka. Wahaya na sadaka zote huchukuliwa kuwa aina za biashara ya ngono.

Wake hawa wa tano, kimsingi, ni wanawake waliofanywa watumwa wa bwana wao, wake wanne halali - ambao angewaoa kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu - na watoto wao.

Wanakabiliwa na unyanyasaji wa kiakili, kimwili na kingono, mara kwa mara wananyimwa chakula na mahitaji mengine ya kimsingi, na kulazimishwa kufanya kazi za nyumbani, kuchunga mifugo na kulima mazao.

Haya yalikuwa maisha ya Hadizatou Mani-Karoau baada ya kununuliwa nchini Niger na kuvushwa mpaka hadi Nigeria.

Anasema chifu huyo mwenye ushawishi mkubwa "alipata dili nzuri" kwa kumnunua yeye na wanawake na wasichana wengine saba mara moja. Shughuli hiyo ilifanywa bila ridhaa yake au ya wazazi wake.

Mzunguko mbaya wa unyanyasaji ulimfanya atoroke kwa nia ya kurudi Niger, lakini kila mara alikamatwa na kurudishwa Nigeria kukabili adhabu kali zaidi.

"Angesema angeweza kunifanyia vile apendavyo kwa sababu alininunua kama alivyonunua mbuzi wake," anasema. Alibakwa na kulazimishwa kuzaa watoto wa ''mmiliki'' wake.

Bi Mani (aliyembeba mtoto wake) alifika katika mahakama ya Niamey mwaka wa 2008

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Bi Mani (aliyembeba mtoto wake) alifika katika mahakama ya Niamey mwaka wa 2008

Mazoea ya wahaya yalianza karne kadhaa zilizopita na yamejikita sana katika jamii.

Wakoloni wa Ufaransa waliipiga marufuku mwanzoni mwa Karne ya 20, lakini mara nyingi waliipuuza badala ya kuwashtaki wahusika.

Mwaka 1960, chini ya katiba mpya ya Niger, utumwa uliharamishwa tena kwa karatasi - lakini ukaruhusiwa kuendelea kwa vitendo.

Hatimaye nchi ilichukua hatua muhimu mwaka 2003 kwa kufafanua rasmi wahaya na kuwafanya kuwa wahalifu chini ya kanuni ya adhabu.

Kufuatia uamuzi huo, Bi Mani alipewa cheti cha uhuru na mwaka wa 2005 alitoka na watoto wake wawili na wahayou wenzake wawili, ili kuishi tena kama mtu huru.

Lakini alipoenda kuolewa na mume wake wa sasa, mwaka mmoja baadaye, mmiliki wake wa zamani alimpeleka mahakamani na kumshtaki kwa kwa kumkosea, akidai kuwa bado alikuwa mke wake

'Mzunguko wa aibu'

Bi Mani alipatikana na hatia ya ubinafsi na kuhukumiwa kifungo cha miezi sita gerezani - uamuzi ambao ungebatilishwa mnamo 2019 pekee.

Hata hivyo, pia aliendelea kuwasilisha kesi dhidi ya serikali ya Niger katika Mahakama ya Haki ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (Ecowas), ambayo ilisababisha uamuzi wa kihistoria.

Majaji waliamua kuwa Niger ilikuwa imevunja sheria zake za kupinga utumwa kwa kutomtia hatiani mwanamume aliyemfanya mtumwa, na kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kisheria wa kumlinda.

Alitunukiwa $20,000 (£17,000 au 10,000,000 CFA francs) mwaka 2009, ambazo serikali ya Niger ililipa.

Bi Mani alisaidiwa na shirika la Niger la kupambana na utumwa Timidria na NGO ya Uingereza ya Anti-Slavery International katika kupigania haki.

Rais wa Chama cha Timidria Ali Bouzou anasema utumwa bado umejaa katika mikoa ya Konni, Madaoua-Bouza na Illela, eneo ambalo wamelipa jina la "pembetatu ya aibu".

"Kuna vijiji vizima katika 'pembetatu ya aibu' ambapo zaidi ya nusu ya wakazi wameundwa na wahayou," anasema.

TIMIDRIA

Chanzo cha picha, TIMIDRIA

Maelezo ya picha, Mnamo 2009, kazi ya Bi Mani ilitambuliwa kwa Tuzo la Wanawake Jasiri - hapa, na Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo Hillary Clinton na Mke wa Rais Michelle Obama.

Baadhi ya mashtaka yanafanyika nchini Niger, chini ya sheria ya kupinga utumwa.

Kati ya 2003 na mapema 2022, kumekuwa na malalamiko 114 ya utumwa, Bw Bouzou anasema, ambapo kulikuwa na mashtaka 54 na hatia sita (nne kati ya hizi zilisimamishwa).

Lakini vita hii ya kisheria ni mbali na kushinda. Wale wanaopatikana na hatia ya makosa yanayohusiana na utumwa wanatakiwa kupokea vifungo vya jela kati ya miaka 10 na 30, lakini hukumu za hivi majuzi zimekuwa fupi zaidi, chini ya miaka 10.

Wataalam wanatoa wito kwa hatua kubwa zaidi kuchukuliwa kushughulikia suala hilo.

Shirika la Bw Bouzou linapendekeza kwamba machifu wa kimila - ambao mara nyingi huwa nyuma ya mila hiyo - wanapaswa kupokonywa mamlaka yao.

Pia inataka juhudi za kukabiliana na dhana potofu iliyoenea kwamba wahaya inaambatana na sheria za Kiislamu.

100 Women