Jinsi operesheni ya siri ilivyofichua wasafirishaji haramu wa kakakuona

gtrwer

Chanzo cha picha, getty image

Maelezo ya picha, Aina zote nane za Kakakuona ziko hatarini kutoweka
Iliyochapishwa

Viongozi wa genge la kusafirisha wanyama pori duniani wametiwa hatiani baada ya uchunguzi wa miaka minne nchini Nigeria. Walipatikana na hatia mwezi uliopita kwa kusafirisha kakakuona, wanyama walio hatarini kutoweka barani Afrika.

Wafanyabiashara hawa walihusika na nusu ya biashara haramu ya kakakuona duniani. Makala haya yanaeleza jinsi walivyozidiwa ujanja na wanunuzi feki - katika operesheni iliyofanywa na shirika dogo la misaada kutoka Ulaya.

Katika mkahawa

GRTFGGF
Maelezo ya picha, Van

Mwanamke wa Kivietinamu yuko kwenye operesheni hatari ya siri. Ameketi karibu na meza katika mkahawa fulani huko Vietnam. Pembeni yake ni mmoja wa wafanyabiashara wakuu wa wanyamapori nchini.

Van - sio jina lake halisi - anajifanya kama mnunuzi kwa ajili ya bosi wa Kichina. Nje ya mkahawa, ipo timu ya uchunguzi inafuatilia. Kakakuona huliwa barani Afrika, wakati barani Asia hutumika kwa tiba za jadi.

Watafiti wanakadiria kutoka 2010, karibu kakakuona milioni moja waliuawa na kusafirishwa katika biashara haramu.

Aina zote nane - nne za Kiafrika na nne za Asia - zimeorodheshwa kama zilizo hatarini, na tatu zikizingatiwa kuwa katika hatari kubwa ya kutoweka.

Van anafanya kazi katika Tume ya Haki ya Wanyamapori, shirika la usaidizi lililoanzishwa mwaka 2015 ili kuzuia mitandao ya uhalifu inayopata pesa kutokana na biashara haramu ya wanyamapori.

Msimamizi mkuu wa upelelezi ni Steve Carmody, afisa wa zamani wa polisi kutoka Australia – miongoni mwa majukumu yake alikuwa akikabiliana na magenge ya dawa za kulevya.

Kuaminiwa na walanguzi

EDWD
Maelezo ya picha, Steve Carmody mkuu wa upelelezi
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwaka 2018, Carmody aligundua mabaki ya wanyama yaliyofichwa yakisafirishwa kwenye makontena ya meli kutoka Afrika Magharibi kwenda Asia. Alianza kukusanya taarifa juu ya wanunuzi wa Asia. Uchunguzi huu umepewa jina la Operesheni Hydra.

Janga la Covid-19 lilipotokea 2020, lilimpa fursa asiyoitarajia. Wafanyabiashara wakubwa wa wanyamapori hujificha, anaeleza: "Unaweza kuwaona wake zao wakionyesha utajiri wao, lakini wafanyabiashara wakuu tunaowachunguza hawako kwenye mitandao ya kijamii."

Lakini Covid ilisababisha usafirishaji kuwa mdogo, wasafirishaji waligeukia Facebook kutafuta wanunuzi. "Tulianza kutumia watu wa siri kuzungumza na watu hawa," Carmody anasema, ‘’mmoja alikuwa Van."

Kuwa mwanamke katika biashara hii si jambo la kawaida, lakini Van anasema ilikuwa faida kwake, kwani wafanyabiashara hawakujificha: "Hawana mashaka na mwanamke."

Kwa miezi kadhaa alipata kuaminiwa na Morybinet Berete, ambaye anatoka Guinea, Afrika Magharibi lakini alikuwa na makaazi yake nchini Nigeria, kitovu cha biashara haramu ya kakakuona.

‘Berete alikuwa na maisha mazuri,’ anasema Carmody, "akiendesha gari zuri, ana nyumba nzuri". Timu ya uchunguzi ilimpa jina la siri la Genie.

Van kupitia mtandao, alipata namba ya WhatsApp ya Berete. Katika simu moja ya video anaoekana akiingia uani. Anaelekeza kamera ya simu kwenye rundo kubwa la magunia. Gunia moja lililojaa mabaki ya kakakuona anayotaka kumuuzia Van analifungua kwa juu.

Kuna magunia mengi kote uani, kila moja likiwa na maelfu ya magamba yaliyotolewa kutoka mizoga ya kakakuona.

'Wanyama hawana maana kwao'

fvfd

Chanzo cha picha, WILDLIFE JUSTICE COMMISSION

Maelezo ya picha, Phan Chi, almaarufu Big Mac

Wakati Van akichunguza alilazimika kuficha hisia zake za kweli, lakini miaka miwili baadaye, kumbukumbu zinamshitua. "Kakakuona laki moja ni lazima kuuawa," anasema, "nilihuzunika sana kwa sababu napenda wanyama."

Je, Morybinet Berete alikuwa na maoni gani kuhusu viumbe hao ambao yeye na genge lake walikuwa wakisafirisha magamba yao?

"Anafanya biashara tu. Wanyama hawana maana kwao," anasema Van.

Video ya WhatsApp ilikuwa kosa kubwa la Berete. Wachunguzi waliitumia ili kupata anuwani yake.

"Ni kama Pablo Escobar akikuambia anapoishi Colombia, na kukuonyesha kokeini kwenye handaki lake," anasema Carmody.

Rushwa ni kichocheo kikuu cha uhalifu kwa wanyamapori. Carmody anaelezea sehemu ngumu zaidi ya uchunguzi wowote wa kimataifa ni kutafuta "kundi dogo la maafisa wa kutekeleza sheria ambao hawawezi kununuliwa. Na mara tu unapowapata, ni kama kupata dhahabu".

Nchini Nigeria, walipata maafisa wa Huduma ya Forodha ya Nigeria (NCS).

Julai 2021, aliwadokeza maafisa wa NCS, ambao walivamia boma la Berete nchini humo na kukamata kilo 7,000 za mabaki ya kakakuona, na kiasi kidogo cha kucha na pembe za ndovu. Waliwakamata wanaume watatu, ingawa Morybinet Berete hakuwepo nyumbani.

Kupekua simu za washukiwa kulipelekea mafanikio mengine makubwa – walipata utambulisho wa wanunuzi wa Kiasia.

Big Mac na Fries

WFEDWDW

Chanzo cha picha, WILDLIFE JUSTICE COMMISSION

Maelezo ya picha, Benz

Hilo lilibadilisha mwelekeo wa uchunguzi kutoka Nigeria kurudi Vietnam, ambapo operesheni ya ufuatiliaji ilikuwa Machi mwaka jana ili kuwafuata wanunuzi.

Akijifanya kuwa anafanya kazi kwa mnunuzi wa Kichina, Van alijenga imani yao, na kusaidia kujua jinsi biashara ya ulanguzi ilivyofanya kazi.

Big Mac alinunua kakakuona waliouzwa kutoka kwa Berete. Mabaki ya kakakuona yalisafirishwa nje ya Nigeria kimagendo - hasa kwenye boti - na kuuzwa kwa wateja nchini China.

Huko, husafirishwa kama mabaki ya kakakuona ambako yanaweza kutumiwa kisheria katika dawa za jadi. Usafirishaji mara nyingi hulipwa kwa sarafu ya mtandaoni iliyounganishwa na dola ya Marekani.

Mpelelezi mwingine wa siri alishawishi genge hilo kujitia hatiani. Katika simu ya video kupitia WhatsApp anauliza wanataka kununua nini. "Nchini Nigeria tunataka kakakuona pekee," Big Mac anajibu.

Benz alisema alihitaji tani 20 za mabaki ya kakakuona kusafirishwa hadi Vietnam, akilalamika kwamba polisi walikuwa wamekamata mali yake wakati wa msimu wa joto. Ushahidi ulizidi kuongezeka.

Mei mwaka jana, wasafirishaji haramu wa Kivietinamu walikwenda Afrika kununua bidhaa zaidi za wanyamapori. Kutoka Msumbiji, Benz alituma video ya pembe za faru alizokuwa amezificha kwenye masanduku ili kusafirisha kinyemela ndani ya ndege.

Siku kadhaa baadaye genge hilo lilifika Lagos, Nigeria, huku Big Mac akijigamba kwenye video kwamba anaweza "kusafirisha kontena kutoka Nigeria."

Ambacho hakufahamu ni kwamba timu ya upelelezi ya Huduma ya Forodha ya Nigeria ilikuwa ikimfuatilia tangu alipowasili nchini. Big Mac alikamatwa katika chumba chake cha hoteli akiwa na simu mbili. Zilitoa ushahidi wa kutosha.

Nyuma ya nondo

grt

Chanzo cha picha, NIGERIA CUSTOMS SERVICE

Maelezo ya picha, Maafisa wa Nigeria wakishikilia kilo 700 za magamba ya Kakakuona, 2021

Phan Chi (Big Mac), Phan Quan (Benz) na Duong Thang (Fries) walishtakiwa kwa magendo na biashara ya kakakuona na pembe za ndovu.

Wakikabiliwa na nafasi ndogo ya kuachiliwa, walikiri makosa katika kesi yao ya mapema mwezi huu. Kakake Morybinet Berete, Mory pia alipatikana na hatia. Na mashitaka megine yanafuata.

Wanaume hao wanne walihukumiwa kifungo cha miaka sita kila mmoja, wakiepuka muda zaidi gerezani kwa kukubali kulipa faini kama sehemu ya makubaliano.

Vipi kuhusu Morybinet Berete, almaarufu Genie, aliyekimbia tangu Julai 2021 na kukabiliwa na amri ya mahakama ya kukamatwa?

"Ninapenda uvuvi," anasema Carmody. Ananyooshea kidole simu kwenye meza yake: "Mara nyingi mimi hupiga simu chache ili kuona ni nani anasumbua. Genie anaendelea kusumbua."

Si punde Carmody, Van na timu yao watamvua Genie.