Yajue masuala saba yaliyomsumbua mzee Mwinyi

Aliyekuwa rais wa awamu ya pili Hayati Ali Hassan Mwinyi

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Na Florian Kaijage
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa

Aliyekuwa Rais wa Tanzania Ali Hassha Mwinyi anazikwa leo, Jumamosi tarehe 2 mwezi Machi katika eneo la Mangapwani, Unguja-Zanzibar.

Katika kitabu chake: “Mzee Rukhsa, Safari ya Maisha Yangu” kilichozinduliwa mwaka 2020, kuna masuala ambayo aliyaeleza kwa msisitizo hususan akiwa rais kama yanavyotanabaishwa hapa…

Mzee Mwinyi anazungumzia uteuzi wa Joseph Sinde Warioba kuwa Waziri Mkuu mwaka 1985 baada ya uchanguzi mkuu akiwa kijana wa miaka 45 na kwamba kuna madai ya kushinikizwa na Mwalimu Nyerere kumteua Warioba lakini anasema uamuzi huo aliufanya yeye mwenyewe kwani alimfahamu Warioba kwa uwezo wake.

Anaweka bayana kuwa alikuwa amteue tena Warioba mwaka 1990 kuendela kuwa Waziri Mkuu lakini mwenyewe aliomba kupumzika.

Kiongozi huyo anaelezea pia suala la wabunge 55 maarufu (G55) wa Tanzania Bara waliodai serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano wakitaka muundo wa serikali tatu hoja ambayo chimbuko lake ni msimamo wa Zanzibar kutaka Rais wa Zanzibar aendelee kuwa Makamu wa rais wa muungano pamoja na uanachama wa Zanzibar katika Umoja wa nchi za Kiislamu (OIC).

Ameeleza, “jambo hili la muungano lilikuwa gumu sana na kuna wakati lilielekea kunizidi kimo”.

Anakiri kuwa aliona Muungano ulikuwa katika hatari ya kuvunjika kama si jitihada za Mwalimu Nyerere ambaye alifanya naye vikao mbalimbali ikiwemo kusafiri hadi Butiama na kushauriana yaye mara kadhaa kwa simu na ana kwa ana.

Anasema kuna wakati wapo viongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi CCM na serikalini waliokuwa hawafurahishwi namna Rais na viongozi wengine walivyokuwa wakimtumia Mwalimu Nyerere kudhibiti mambo yaliyokwenda kombo na kutaka kumpelekea ujumbe Mwalimu kuwa ni mstaafu asiye na mamlaka serikalini na chamani.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Anasema kwa kufanya hivyo ilikuwa ni makosa makubwa sana na kwa baadhi makosa hayo yaliwagharimu.

Jambo jingine ni Dr. Salim Ahmed Salim kuteuliwa kuwa Naibu waziri Mkuu pia Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwani alikuwa ni Waziri Mkuu awali akiteuliwa baada ya kifo cha Edward Moringe Sokoine Aprili mwaka 1984.

Sasa kwa sababu ya mahitaji ya kikatiba kuwa Waziri Mkuu na Mkamu wa kwanza wa Rais asingeweza kutoka Zanzibar kama alivyo Rais Mwinyi wakati huo, hivyo alilazimika kuunda nafasi isiyo ya kikatiba lakini ya kumpa Salim heshima anayostahili, baada ya kushauriana na Mwalimu Nyerere.

Mzee Mwinyi anakumbuka jinsi ambavyo hawezi kusahahu aibu iliyomkuta kwenye sherehe za kukabidhiwa barabara ya Mombo-Lushoto iliyokuwa imejengwa upya na serikali ya Ujerumani na aliyekuwa balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Christel Steffler alimsuta waziwazi kwamba barabaraba ile ilikuwa imejengwa kwa mara ya pili na Ujerumani kwa sababu ya Tanzania kushindwa kuitunza hadi lami yote ikang’oka na kwamba hiyo ilikuwa mara ya mwisho kwa Ujerumani kufanya hivyo.

Mzee mwinyi anajikosoa kuwa akitazama nyuma anaona kuwa pengine haikuwa sahihi kwake kumteua Profesa Kighoma Malima kuwa Waziri wa fedha mwaka 1992 ikizingatiwa kuwa huko nyuma Malima alikuwa mpinzani mkubwa wa kuanzisha mageuzi ya kiuchumi na kwamba hiyo ilikuwa ni sababu ya itikadi na si elimu kwani Prof. Malima alikuwa msomi wa uchumi aliyebobea tena aliyesomeshwa katika vyuo maarufu vya Dartmouth College, Yale na Princeton vya nchini Marekani.

Profesa Kighoma Malima alijuzulu uwaziri wa Fedha na baadaye kuteuliwa kuwa waziri wa viwanda na biashara pia akajiuzulu nafasi hiyo Juni 1995.

Mzee Mwinyi anasema Prof. Malima alikuwa anautafuta sana urais kumrithi Mwinyi lakini kwa bahati mbaya sana alijiegemeza kwenye uislamu kama karata yake kwenye mchezo wa siasa.

Suala la mauaji ya kimbari ya Rwanda

Mzee mwinyi anasema kati ya mambo ya kikanda yaliyomsumbua sana ni magomvi ya Rwanda na Burundi hususanI mauaji ya Kimbari ya Aprili hadi Julai 1994.

Anasema kwenye mazungumzo jijini Dar es Salaam Rais wa Rwanda Juvenal Habyarimana alisemwa mno kwamba anakwamisha makubaliano ya Arusha na akaahidi kwenda kuyatekeleza japo alikuwa na hofu ya kuuawa au serikali yake kupinduliwa akiwa nje ya nchi.

Ameeleza kuwa kabla ya kuwenda Dar es Salaam, Habyarimana alikuwa Jamhuri ya Kidemkrasi ya Congo ambako alidokezwa na Rais Mobutu Sseseseko kuwa aliarifiwa na serikai ya Ufaransa kuwa ulikuwepo mpango wa kumuua akitokea Dar es Salaam au kumpindua akiwa nje ya nchi na akamshauri asiende Dar es Salaam lakini alikwenda na baadaye kuuawa baada ya ndege yake kudunguliwa kabla ya kutua uwanja wa ndege Kigali akiwa Pamoja na Rais wa Burundi Cyprien Ntaryamira.

Ubinafsishaji

Ameweka bayana pia lawama alizowahi kutupiwa kuwa serikali yake ilibinafsisha viwanda na mashirika ambayo yalikuwa yanapata faida ukitolewa mfano wa kiwanda cha Bia Tanzania (TBL).

Mzee Mwinyi anasema ni kweli kiwanda hicho kilikuwa kinafanya kazi lakini chini sana ya uwezo wake na chini ya kiwango cha ubora wa bia unaotakiwa, kwani chupa moja iliweza kuwa na kileo cha asilimia 4 na nyingine ikawa na asilimia saba.

Kama hiyo haitoshi, anasema haikuwa ajabu kukuta mzoga wa mende ndani ya chupa ya bia au kukuta bia inanuka mafuta ya taa.

Kali zaidi ni kuwa pale anaposema eneo la Kariakoo watu waliinunua bia ikiwa inapikwa kiwandani Ilala na inafika ikiwa ya moto lakini ilinywewa vivyo hivyo.