Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
WARIDI WA BBC : 'Wiki moja hospitalini iligeuka kuwa zaidi ya mwaka mmoja'
Na Anne Ngugi
BBC News Swahili
Eulene Igobwe Kamau ni mama, mke na mtoa ushauri nasaha kutoka nchini Kenya ambaye ameniambia kuwa mwaka mmoja uliyopita maisha yake yalibadilika sana baada ya mwanae wa kike kwa jina Becky ambaye anaishi na hali ya utindio wa ubongo almaarufu Cerebal Palsy kulazwa katika hospitali moja kuu.
Eulene na mumewe walidhani kuwa binti yao alilazwa kwa matibabu ambayo yangechukua muda wa wiki mmoja pekee na sio zaidi.
Mwaka mmoja baadaye Eulene na familia yake wamefanya wadi ya watoto katika hospitali moja kuu nchini Kenya kuwa makao yao , sio kwa hiari yao ila kutokana na usugu wa hali ya ugonjwa wa binti yao.
Tangu kuzaliwa kwa Becky, alianza kuonyesha dalili za ugonjwa pindi alipotimiza miezi 5 , shingo lake hailikuwa wima, licha ya hilo Eulene kama mama anasema hakuwa na wasiwasi, hadi alipofahamishwa na daktari pamoja na baadhi ya jamaa zake kwamba huneda binti yake alikuwa na utindio wa ubongo kkwa sababu ya daalili alizokuwa nazo .Eulene aliendelea kupuuza hofu hiyo.
Anasema kuwa kukosa habari zaidi kuhusiana na hali hiyo kulipelekea familia yake kuchukua muda kabla ya kumpeleka hospitalini kwa matibabu.
Na hadi wakati mtoto alipoanza kuonyesha dalili za ugonjwa sugu , kwa mfano ishara za kifafa, kupata ugumu wa kupumua pia kudumaa ndipo familia yake ilipoamua kutafuta matibabu .
Ilikuwaje hadi kuishi hospitalini kwa mwaka mzima?
Tangu Februari mwaka jana , Eulene aliarifiwa na wataalam kuwa bintiye angestahili kulazwa hospitalini kutokana na ongezeko la hali ya degedege (convulsions) , hali iliyomkosesha binti yao hewa ya kutosha mwilini mwake , kuathiri mfumo wake wote wa kupumua na kwa hiyo alistahili kusalia hospitalini ili kuhakikisha hali hiyo imeshughulikiwa.
Licha ya kuahidiwa kuwa wangelazwa kwa wiki moja,kipindi hicho kiligeuka na kuwa zaidi ya mwaka mmoja .
Ndani ya kipindi hicho bintiye Eulene kwa wakati mmoja alizidiwa na kupelekwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU ), alipoteza uwezo wake wa kuona , na kusikia , lakini wakati huo wote Eulene na familia yake hawakukata tamaa ya kuwa binti wao ambaye kwa sasa anaendelea kupata matibabu angepona.
“Nadhani kuwa hali ya binti yangu imetufungua macho sote kama jamii , maana ya upendo halisi sasa ni dhahiri kwetu , sidhani tungefaulu hadi tulipofika kama hatungekuwa na upendo kwa binti yangu na kati yetu sisi wote ”Eulene anasema.
Changamoto za kuishi hospitalini
Kama mama ambaye alikuwa amezoea kuwa na shughuli zake za kila siku, maisha yaligeuka ghafla na alilazimika kuwa hospitalini na binti yake.
Eulene anaeleza kuwa kuna siku ambazo zilikuwa ngumu kwake huku akiona maisha yakimtoka bintiye mara kwa mara , lakini kimuujiza alirejea katika hali ya kawaida.
“Hali ya binti yangu Becky, imetubadilisha sana, sisi sote tuna matumaini kuwa Becky ataendelea kupata nafuu na wakati mmoja tutarejea na yeye nyumbani , licha ya kuwa kwa hivi sasa haoni wala kusikia nina imani kuwa kila siku anaendelea kupata nafuu ”anasema Eulene.
Changamoto kubwa kwamba wakiw akatika wadi ya watoto. wamelazimika kushuhuduia watoto ambao wanafariki wakipokea matibabu na kuona jinsi hatima hiyo inavyowavunja wazazi na wapendwa wao.
“Nimeona makumi ya watoto wakiaga , nimeshuhudia vilio vya kutamausha hapa hospitalini ' Eulene anasema
Imekuwa ni miaka 8 tangu Becky kuzaliwa na licha ya kuwa hajawahi kuzungumza neno hata moja au hata kufanya mambo ya kawaida ambayo watoto wa umri wake wanafanya familia yake imeendelea kumpenda,wakitumai kuwa siku mmoja huenda mambo yakabadilika.
Eulene amekuwa mstari wa mbele kutoa ushauri na mafunzo kwa umma kuhusiana na ugonjwa huu , anasema kuwa uzoefu wake hasa hospitalini umemdhihirishia kuwa kuna watu katika jamii wanaofikiria kuwa Utindio wa ubongo ni ugonjwa wa kiukoo.
Anawasihi watu kuwa wenye kusoma na kupata habari zaidi kuhusu magonjwa ambayo hayaeleweki kwa urahisi.
Je ugonjwa wa Utindio wa ubongo ni nini?
Utindio wa ubongo au Cerebral Palsy kwa lugha ya kimombo ni ugonjwa unaoathiri ubongo, na mara nyingi hutokea kwa watoto na husababishwa na uvujaji wa damu kwenye ubongo au ukosefu wa hewa y akutosha kwenye ubongo.
Unaweza kutokea wakati mtoto anapoanza kupoteza fahamu punde baada ya kuzaliwa au mwezi wa kwanza wa kuzaliwa. Vilevile jeraha kwenye ubongo linaweza kusababisha matatizo ya kuongezeka na ugumu wa kuelewa mambo.
Ugonjwa huu una viashiria tofauti na sio watoto wote wanauopata ugonjwa huu wanakuwa na viashiria sawia kwa mfano kuna wale ambao watakuwa na uwezo mdogo wa kuzungumza na kutembea , wapo wengine ambo hukosa uwezo wowote wa kujitunza na kuwategemea watu wengine kuwahudumia.