Wanajeshi wa Tanzania kurejeshwa nyumbani kufuatia tuhuma za unyanyasaji wa kingono CAR

.

Chanzo cha picha, AFP

Iliyochapishwa

Umoja wa Mataifa umetangaza kukirudisha nyumbani kikosi cha walinda amani 60 kutoka Tanzania waliokuwa Magharibi mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) kufuatia madai ya unyanyasaji wa kingono na dhulma.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amewaambia waandishi wa habari kwamba uamuzi wa kukirudisha kikosi hicho nyumbani ulifanywa kufuatia mashauriano na ujumbe wa kulinda amani nchini CAR, MINUSCA.

"Uamuzi huo unawadia baada ya uchunguzi wa awali ambao ulipata ushahidi wa kuaminika kwamba wanachama 11 wa kitengo hicho walidaiwa kujihusisha na unyanyasaji wa kingono na kuwadhulumu waathiriwa wanne", Bw. Dujarric alisema.

Ipi hatma ya wanajeshi wa TZ waotuhumiwa kwa unyanyasaji wa kingono?

Katika taarifa, MINUSCA ilisema kuwa timu nyingine ya kukabiliana haraka na hali hiyo "imetumwa mara moja" kutathmini madai hayo.

Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa Twitter, Mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix, amesema kwamba tabia hiyo haina nafasi katika sehemu yoyote ya idara yake.

Ameongeza kuwa kuwarejesha nyumbani "ni hatua madhubuti iliyochukuliwa kuwalinda waathiriwa na kuonyesha azimio letu la kushughulikia haraka makosa haya na nchi inayochangia wanajeshi."

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

Mwisho wa X ujumbe

Waathiriwa wapatiwa msaada

"Waathiriwa waliotambuliwa wanapatiwa matunzo na usaidizi na washirika wa Misheni ya kibinadamu. Misheni pia imetuma timu ili kujihusisha zaidi na jamii”, aliongeza.

Msemaji huyo alisema Serikali ya Tanzania tayari imearifiwa rasmi kuhusu uamuzi huo, na wao wenyewe wametuma kikosi cha taifa kwenda CAR kufanya uchunguzi.

Tanzania yaahidi kuchukua hatua

.

Chanzo cha picha, AFP

UN imeandika kwenye tovuti yake, "Katika kuthibitisha dhamira yao ya kutovumilia kabisa dhulma na unyanyasaji wa kijinsia, mamlaka ya Tanzania ilibainisha uzito wa tuhuma hizo na imejitolea kuchukua hatua zinazohitajika kushughulikia masuala haya."

Bw. Dujarric aliongeza kuwa kitengo hicho kilihamishwa mbali na eneo ambalo madai ya unyanyasaji ulifanyika na sasa wamefungiwa kwenye kambi ili kuwalinda waathiriwa pamoja na uadilifu wa uchunguzi.

Taarifa imeongeza kuwa kikosi hicho kitarejeshwa nyumbani mara uwepo wake hautahitajika tena na wachunguzi.

Kitendo hicho hakitavumilika kabisa

.

Chanzo cha picha, UN

Maelezo ya picha, Antonio Guterres

Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametangaza sera thabiti na madhubuti mapema na 'kutovumilia kabisa' unyanyasaji wa kingono unaofanywa na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, akitoa wito kwa nchi wanachama kutia saini mkataba wa hiari wa kuzuia na kushughulikia janga hilo, mwaka 2017.

Bw. Dujarric alisisitiza kuwa Umoja wa Mataifa unasalia kujitolea "kutekeleza kikamilifu" sera ya kutovumilia kabisa unyanyasaji wa kingono katika ngazi zote.