Kushindwa kufungwa jela kwa wabakaji wa watoto kumesababusha mimba za utotoni kuongezeka Uganda

.
Maelezo ya picha, Obita David Livingstone anawashutumu polisi kaskazini mwa Uganda kwa kutofuatilia kesi za unyanyasaji
Iliyochapishwa

Ongezeko la kushangaza la unyanyasaji wa kijinsia kwa wasichana wadogo kaskazini mwa Uganda lilifichuliwa wakati iliripotiwa kuwa kutokana na janga hilo kulikuwa na ongezeko la zaidi ya mara nne la wale wenye umri wa miaka 10-14 kupata mimba.

BBC Africa Eye imekuwa ikichunguza ni kwa nini wahalifu wanaotekeleza uhalifu huo wanakwepa mkono wa sheria.

Msichana mjamzito - asiyezidi umri wa miaka 12 - anatazama chini kwenye mikono yake wakati mwenyekiti wa baraza la mtaa anapouliza kuhusu ziara yake ya hivi punde kwa daktari.

Ni aina ya swali ambalo mwanafamilia anapaswa kuuliza, lakini huu sio ujauzito wa kawaida.

Msichana huyo anaishi kivyake katika nyumba ndogo, wilayani Kitgum, na anatarajiwa kujifungua siku yoyote.

Biashara ya wazazi wake ya mihogo ilishindikana, wakarudi kijijini kwao kutafuta pesa kwa ajili ya familia.

"Aliachwa hapa kwa sababu huku ni karibu kidogo na shule," mwenyekiti Obita David Livingstone anasema.

"Lakini kwa bahati mbaya, chumba kinachofuata hapa ndipo watu wanakunywa pombe. Hiyo pekee imemuweka kwenye changamoto nyingi."

Hakuna anayejua baba ni nani, au nini kilitokea.

'Kesi tatu kwa wiki'

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

BBC Africa Eye inaruhusiwa tu kurekodi msichana huyu, ambaye hatumtaji jina, kwa sababu Bw Livingstone alisema alitaka kuhamasisha unyanyasaji wa kingono unaofanyika katika jamii.

"Katika wiki moja, huwa tunakuwa na kesi kama tatu za unajisi. Wakati mwingine tunapompata mhusika, tunapaswa kuwafunga kwa kamba na kuwapeleka polisi. Lakini hawajisumbui kulifuatilia suala hili."

Amechoshwa na viwango hivyo vya kutokujali.

"Hakuna mtu ambaye anaweza kumuunga mkono mtu ambaye amebakwa. Kwangu mimi naiona haki hii kama haki dhaifu," mwenyekiti wa mtaa anasema.

Unajisi unamaanisha kujamiiana kinyume cha sheria na msichana aliye chini ya umri wa miaka 18.

Kulingana na Mfumo wa Taarifa za Usimamizi wa Afya wa Uganda, mimba kati ya wasichana wenye umri wa kati ya miaka 10 na 14 iliongezeka kwa 366% wakati wa kutekelezwa kwa mara ya kwanza kwa Covid-19 (Machi-Juni 2020).

Katika hospitali kuu ya mkoa mjini Gulu karibu robo ya wajawazito wote katika mwaka wa fedha uliopita walikuwa wasichana wa chini ya miaka 18, umri wa kupata ridhaa nchini Uganda.

.
Maelezo ya picha, Dk Baifa Arwinyo anaona vijana wengi wajawazito ambao walikuwa wahasiriwa wa ubakaji

Mkuu wa masuala ya uzazi Dk Baifa Arwinyo alisema: “Nikizungumzia akina mama vijana wote wamenajisiwa, ni vijana, hawatakiwi kuwa na mimba.

Utapata kwamba idadi ya wanaokufa wakati wa wakujifungua imeongezeka. Kadiri mama anavyokuwa mdogo ndivyo matatizo yanavyoongezeka."

'Unyanyasaji wa kijinsia ulikuwa mkakati wa vita'

Viwango vya juu vya unyanyasaji wa kijinsia vinafikiriwa kuwa urithi wa mzozo wa miongo miwili kaskazini mwa Uganda, ambao ulikuwa maarufu kwa ukatili wake.

Vita hivyo vilianzishwa na Joseph Kony, mkuu wa Lord's Resistance Army (LRA), kundi la waasi lililotaka kupindua serikali.

Wapiganaji wake walijulikana kwa kuwatendea unyama wale waliowateka nyara: kuwalemaza, kuwakata midomo na miguu na mikono, na kuwalazimisha watu kujisalimisha kwa woga.

Inakadiriwa watoto 40,000 walitekwa nyara, kulazimishwa kuwa wanajeshi au watumwa wa ngono, na watu milioni 1.7 waliishi katika kambi za wakimbizi wa ndani.

Waasi walihama kutoka Uganda mwaka 2008, lakini athari za ukatili wao bado zipo hadi leo, kulingana na mwanaharakati wa haki za kijinsia Pamela Angwech, mkurugenzi wa Gulu Women Economic and Globalisation, asasi isiyo ya kiserikali ya msingi (NGO).

"Kuishi ndani ya mazingira mabaya ya maeneo ya migodi kulikuwa na madhara ya muda mrefu kwa jamii. Watu wamezoea kuona maiti, watu wamezoea kuona kifo. Unyanyasaji wa kijinsia ulitumiwa kama mkakati wa kijeshi na timu ya LRA.

"Ninaelezea kama vita vilipiganwa katika mwili wa mwanamke na mwanamke akawa uwanja wa vita."

Watu wachache waliwahi kuona haki kwa uhalifu wa kikatili uliofanywa wakati wa vita.

Kamanda mmoja wa LRA, Dominic Ongwen, alihukumiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) na kupatikana na hatia ya makosa 61 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu mnamo Februari 2021.

Kony pia anasakwa na ICC lakini bado hajulikani aliko.

.
Maelezo ya picha, Wakili Eunice Lakaraber Latim anazungumza na wanajamii kuhusu kiwango cha unyanyasaji wa watoto

Kulingana na wakili Eunice Lakaraber Latim, ambaye anafanya kazi katika NGO ya Caritas, urithi huo wa ukosefu wa uwajibikaji unaendelea kaskazini mwa Uganda hadi leo.

"Nilikua kutoka Gulu, niliona watoto wengi wakinajisiwa, na wengi wa wazazi hao hawakuwa na rasilimali za kutafuta haki ambayo watoto wao walistahili."

'Mtoto wangu anaishi kwa uchungu'

Bi Latim aliipeleka Africa Eye kwa familia ya msichana wa miaka mitatu ambaye alibakwa na jamaa yake.

Mama aligundua tu baada ya kuona mtindo wa kutembea wa mtoto umebadilika. Polisi walipokuja kumkamata jamaa yake, anasema walimwomba pesa za "kumsafirisha".

"Wakati huo nilitarajiwa kulisha mfungwa," asema Bi Latim.

"Lazima ulipe pesa ukiwa katika hali ya kutafuta kupata haki. Unapaswa kulipa pesa za mafuta ili mshukiwa akamatwe.

"Unatakiwa kuwapa chakula wakiwa bado kituo cha polisi."

Mshukiwa alishikiliwa kwa muda wa miezi sita, lakini kwa sababu baadhi ya taratibu sahihi za kisheria hazikufuatwa, aliachiwa kwa dhamana, mama huyo hakuwa na njia ya kuendeleza kesi hiyo.

Taarifa za polisi na za matibabu zinathibitisha kuwa mtoto huyo wa miaka mitatu aliambukizwa magonjwa ya zinaa.

"Mtoto wangu bado ana uchungu, hata sasa. Maambukizi hayajawahi kupona," mama yake alisema.

"Alistahili kukabiliwa na kifungo gerezani. Sikutaka imalizike hivi."

Bi Latim anasema si jambo la ajabu kwa mfumo wa haki kuwafeli waathiriwa, akisema wamekuwa na kesi kadhaa ambazo zimesambaratika.

"Kuna ufisadi mwingi. Watu hawaogopi kufanya uhalifu hapa, kwa sababu wanasema, ukiwa na pesa, utatoka. Hicho ndicho kinachotokea."

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Aswa, Nachula Damalie, anakiri kuwepo kwa matatizo ya namna baadhi ya kesi zinavyoendeshwa, lakini alikana rushwa imekithiri.

"Hatutakiwi kumwomba mwathirika alipie huduma zetu. Lakini wakati mwingine nikubali kwamba tunaweza kuishiwa na mafuta. Ndiyo.

"Kwa wakati huu na jinsi hali ya ufisadi ilivyo, imekuwa dhana ya jumla kwamba maafisa wa polisi ni wala rushwa, lakini sivyo. wote ni wafisadi, kama taasisi nyingine yoyote ingekuwa. Tuna wazuri na wabaya."

Waziri wa Nchi wa Kaskazini mwa Uganda, Grace Freedom Kwiyucwiny, pia anakiri kuna matatizo.

"Siwezi kukataa kwamba ufisadi upo. Upo katika ngazi zote, hata katika ngazi ya wizara," anasema.

"Tuna sheria za unajisi, tuna sheria za kujamiiana, lakini kwa namna fulani tena, watu wanaenda nyuma ya sheria na kuwahonga polisi halafu polisi wanasema, 'Sawa, nenda ukasuluhishe nyumbani.' Kuna kesi ambazo zimefunguliwa mashtaka, lakini idadi sio kubwa."

Hakuna hata mmoja wa washukiwa katika kesi yoyote iliyochunguzwa na BBC Africa Eye aliyefunguliwa mashtaka.

Uganda: Tazama kinachochochea ongezeka la mimba za utotoni

Maelezo ya video, Uganda: Kushindwa kuwawajibisha vijana ndio chanzo cha mimba za utotoni