Mataifa 5 ya Afrika ambayo Rais na Makamu wake waligeuka maadui

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Ambia Hirsi
- Akiripoti kutoka, BBC Nairobi
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Tangu kuondolewa kwa Rigathi Gachagua kutoka wadhifa wa Naibu Rais wa Kenya mwezi Oktoba 2024, mvutano wa kisiasa baina yake na Rais William Ruto umeendelea kushika kasi, ukichukua sura ya maneno makali ya wazi, shutuma nzito, na hata miito ya mabadiliko ya kisiasa ya kitaifa.
Gachagua aliondolewa kupitia mchakato wa kikatiba uliohusisha kura ya Bunge la Kitaifa kufuatia tuhuma 11 za matumizi mabaya ya ofisi na ukiukaji wa maadili ya umma.
Baadaye, Bunge la Seneti na Baraza la Mawaziri walithibitisha uamuzi huo, na mnamo tarehe 1 Novemba 2024, Profesa Kithure Kindiki akaapishwa rasmi kuwa Naibu Rais mpya wa Jamhuri ya Kenya.
Licha ya kuondolewa kwake, Gachagua ameendeleza kampeni ya kisiasa inayotafsiriwa na wachambuzi kama hatua ya kujijenga upya kwa uchaguzi wa mwaka 2027.
Kauli zake dhidi ya Rais Ruto zimekuwa za moja kwa moja, huku akimtuhumu kwa usaliti, kiburi cha madaraka, na kukengeuka kwa misingi ya muungano wa Kenya Kwanza. Kwa upande mwingine, Rais Ruto na wandani wake wamemshutumu Gachagua kwa uchochezi, kupinga ajenda ya maendeleo, na kujaribu kugawa nchi kwa misingi ya ukabila.
Rais Ruto aliwahi pia kukwaruzana na bosi wake, Rais Uhuru Kenyatta wakati huo Ruto akiwa naibu Rais, ingawa yeye hakuondolewa madarakani. Sasa hali hii ya sintofahamu imezua maswali mapya kuhusu uimara wa taasisi za utawala barani Afrika, na kwa namna gani migogoro ya juu ya uongozi huathiri siasa, uchumi, na mshikamano wa kitaifa.
Katika historia ya bara hili, kumekuwa na migongano mikubwa baina ya marais na manaibu wao, migogoro ambayo kwa baadhi ya nchi ilisababisha kupinduliwa kwa tawala, vita vya wenyewe kwa wenyewe, au hata kuzaliwa kwa tawala mpya kabisa.
Makala hii inachambua mifano mitano mashuhuri ya migogoro ya namna hii kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Zimbabwe: Robert Mugabe dhidi ya Emmerson Mnangagwa (2017)
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mnamo mwaka 2017, Zimbabwe ilikumbwa na mtikisiko mkubwa wa kisiasa baada ya Rais wa muda mrefu, Robert Mugabe, kumfuta kazi Naibu wake, Emmerson Mnangagwa.
Hatua hiyo ilitafsiriwa kama jitihada za Mugabe kumrahisishia mkewe, Grace Mugabe, njia ya kurithi uongozi wa taifa hilo.
Kwa muda mrefu, Mnangagwa alikuwa mshirika wa karibu wa Mugabe, lakini uhasama wao ulianza pale Mnangagwa alipoonekana kuwa na ushawishi mkubwa kuliko ilivyokubalika ndani ya familia ya kisiasa ya Mugabe.
Mnangagwa, aliyejulikana kwa jina la utani la "Ngwena" (Mamba), alikimbilia nje ya nchi baada ya kuondolewa kazini.
Hata hivyo, tukio hilo lilichochea hatua ya kijeshi mnamo mwezi Novemba 2017, ambapo jeshi lilitwaa mamlaka kwa muda na kumuweka Mugabe chini ya kifungo cha nyumbani.
Baada ya wiki chache za shinikizo kutoka kwa chama tawala ZANU-PF na umma wa Zimbabwe, Mugabe alilazimika kujiuzulu, na Mnangagwa akarudi nchini na kuapishwa kuwa Rais.
Tukio hili lilionyesha namna mivutano ya ndani ya uongozi inaweza kusababisha mabadiliko makubwa ya mamlaka. Kwa upande mmoja, lilifungua ukurasa mpya kwa Zimbabwe.
Lakini kwa upande mwingine, wengi walihisi kuwa ilikuwa ni mabadiliko ya sura, si mfumo, kwani serikali mpya ya Mnangagwa iliendelea kukosolewa kwa ukandamizaji wa haki za binadamu na kuzorota kwa uchumi.
Nigeria: Olusegun Obasanjo dhidi ya Atiku Abubakar (2006)

Chanzo cha picha, Getty Images
Uhusiano kati ya Rais Olusegun Obasanjo na Naibu wake Atiku Abubakar ulianza kwa mshikamano mkubwa mwaka 1999, wakati Nigeria iliporejea katika utawala wa kiraia baada ya miaka kadhaa ya tawala za kijeshi.
Atiku alihesabiwa kama msaidizi muhimu, hasa katika kuendeleza mageuzi ya kiuchumi na mapambano dhidi ya ufisadi. Lakini kadri muda ulivyokwenda, tofauti baina yao zilianza kujitokeza wazi.
Mwaka 2006, hali ilifikia pabaya baada ya Obasanjo kujaribu kubadilisha katiba ili aruhusiwe kugombea muhula wa tatu hatua iliyopingwa vikali na Atiku.
Hatua hiyo iligeuka kuwa chanzo cha uhasama mkubwa kati yao. Obasanjo alimnyima Atiku fursa ya kushiriki katika shughuli nyingi za serikali, huku akijaribu kumtenga kisiasa.
Atiku alihamia chama kingine (Action Congress) na kuwania urais mwaka 2007, ingawa hakufanikiwa.
Mgogoro huu uliibua hoja pana kuhusu hatari ya marais wa Kiafrika kuvuruga katiba kwa faida ya kibinafsi, na jinsi manaibu wao mara nyingi hujipata wakigeuka kuwa wapinzani wa serikali walizoshiriki kuziunda.
Sudan Kusini: Salva Kiir dhidi ya Riek Machar (2013 & 2025)

Chanzo cha picha, Getty Images
Sudan Kusini, taifa changa zaidi duniani, limekuwa mfano halisi wa jinsi migogoro ya uongozi inaweza kuibua madhara makubwa ya kijamii na kiusalama.
Rais Salva Kiir na Naibu wake wa muda mrefu, Dkt. Riek Machar, walianza kwa ushirikiano mwaka 2011 mara tu baada ya taifa hilo kupata uhuru kutoka Sudan. Lakini tofauti za kiitikadi, kikabila na hata kimamlaka zilisababisha migogoro ya mara kwa mara.
Mnamo Desemba 2013, Kiir alimshtumu Machar kwa kupanga mapinduzi, hatua iliyozua vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha maelfu ya vifo na mamilioni ya wakimbizi.
Baada ya makubaliano ya amani yaliyosuasua kwa miaka mingi, Machar alirudi serikalini, lakini mvutano haukuisha.
Kufikia mwaka 2025, ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa bado kuna mgawanyiko mkubwa ndani ya jeshi, ukosefu wa utekelezaji wa mkataba wa amani, na mashaka makubwa kuhusu uaminifu kati ya viongozi hao wawili.
Kisa cha Sudan Kusini kinaonyesha namna migogoro ya kisiasa inapopambwa na masuala ya ukabila, inaweza kuwa chanzo cha maangamizi makubwa.
Pia, kinaibua hoja kuhusu umuhimu wa kujenga taasisi imara ambazo zinaweza kudhibiti migogoro ya madaraka bila kupelekea umwagaji damu.
Malawi: Bingu wa Mutharika dhidi ya Joyce Banda (2010)

Chanzo cha picha, Getty Images
Mgogoro kati ya Rais Bingu wa Mutharika na Naibu wake Joyce Banda ni mfano mwingine wa migogoro ya kisiasa iliyosababisha mabadiliko makubwa nchini Malawi.
Mutharika alimteua Banda kama Naibu Rais mwaka 2004, na alidhani kuwa atakuwa mshirika wa karibu na mwenye ufanisi katika serikali yake. Hata hivyo, baada ya Mutharika kushinda uchaguzi wa pili mwaka 2009, hali ilianza kubadilika.
Mutharika alijaribu kubadili katiba ili kuwawezesha marais kuwa na muhula wa tatu, jambo ambalo lilisababisha mivutano kati yake na Banda.
Hali ilizidi kuwa mbaya mwaka 2010, wakati Banda alipopigwa vita vikali na kuondolewa kwenye wadhifa wake wa kiongozi wa chama cha Democratic Progressive Party (DPP).
Hata hivyo, migogoro hii ilikuja kuwa na athari kubwa zaidi wakati Mutharika alipofariki ghafla kwa mshtuko wa moyo mwaka 2012.
Kwa mujibu wa katiba ya Malawi, Joyce Banda, kama Naibu Rais, alichukua hatamu za uongozi.
Alikuwa Rais wa kwanza mwanamke wa Malawi na aliendesha sera za mageuzi na kuboresha hali ya uchumi na utawala wa nchi.
Ingawa alikubaliwa na wengi, utawala wake ulijikuta ukikumbana na changamoto za kisiasa kutoka kwa wafuasi wa Mutharika, na pia alikumbwa na shinikizo la kiuchumi kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.
Sudan: Omar al-Bashir dhidi ya Ali Osman Taha (2013)

Chanzo cha picha, Getty Images
Migogoro kati ya Rais Omar al-Bashir na Naibu wake Ali Osman Taha ilikuwa moja ya vipindi vya mvutano mkubwa katika siasa za Sudan.
Taha alikuwa msaidizi mkubwa wa Bashir na mmoja wa viongozi wa kiutawala wa chama cha National Congress Party (NCP).
Walikuwa na ushirikiano wa muda mrefu, lakini uhusiano wao ulianza kuporomoka mwishoni mwa miaka ya 2000.
Mnamo mwaka 2013, mgogoro mkubwa wa kisiasa ulizuka wakati Bashir alipojumuisha viongozi wa makundi ya upinzani katika serikali yake, jambo ambalo lilitafsiriwa na Taha kama hatari kwa usalama wa chama tawala.
Mivutano hii ilijitokeza wazi katika uchaguzi wa 2015 ambapo Taha alionekana kuwa na msimamo tofauti na Bashir, na hali hii ilizusha wasiwasi mkubwa katika chama cha NCP na serikali ya Sudan.
Ingawa Taha aliondolewa kwenye nafasi muhimu serikalini, Bashir alikumbwa na maandamano makubwa kutoka kwa wananchi, yakihusiana na kushuka kwa hali ya kiuchumi na ukandamizaji wa haki za binadamu.
Mivutano hii ilimalizika kwa mapinduzi ya kijeshi mwaka 2019, ambapo Bashir aliondolewa madarakani na baadaye kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za uhalifu wa kivita na ukiukaji wa haki za binadamu.















