Vita vya Ukraine: Mkataba wa START kuhusu silaha za nyuklia ni nini na inamaanisha nini kujiondoa kwa Urusi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Urusi Vladimir Putin alisema Jumanne kwamba serikali yake inajiondoa kwenye Mkataba wa Kimkakati wa Kupunguza Silaha, unaojulikana kama mwanzo mpya {New START}.
Ni mkataba wa mwisho uliosalia wa silaha za nyuklia kati ya Urusi na Marekani, ambao uliongezwa kwa miaka mitano mnamo 2021.
"Ninalazimika kutangaza leo kwamba Urusi inasitisha ushiriki wake katika mkataba wa silaha za kimkakati za kushambulia," Putin alisema wakati wa hotuba yake kwa taifa.
Alisema kuwa Urusi lazima iwe tayari kufanya majaribio ya silaha za nyuklia ikiwa Marekani itafanya hivyo kwanza.
Kwa upande wake, hivi karibuni serikali ya Marekani ilieleza kuwa Urusi ilikiuka mkataba huo kwa kukataa kuruhusu ukaguzi.
Putin alitoa tangazo hilo siku moja baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kusafiri kwenda Ukraine kwa ziara ya kushtukizia kuonyesha uungaji mkono wake kwa Rais Volodymyr Zelensky dhidi ya uvamizi wa Urusi.
Hapo chini tunaeleza ni nini mkataba huo unajumuisha na matokeo gani yatajiri kufuatia uamuzi wa Putin wa kujiondoa kwenye mkataba huo.

Chanzo cha picha, Reuters
New START ni nini?
Mkataba wa Kimkakati wa kupunguza Silaha au New START uliundwa ili kuzuia vita vya nyuklia. Unaweka kikomo idadi ya vichwa vya kimkakati vya nyuklia ambavyo nchi zote mbili zinaweza kutumia mbai na kuipatia kila nchi uwezo wa kuikagua nchi nyengine.
Awali makubaliano hayo yalitiwa saini mwaka 2010 na marais wa wakati huo, Barack Obama na Dmitry Medvedev.
Mkataba huo unathibitisha kwamba Marekani na Urusi zinaweza kuwa na vichwa vya nyuklia vya masafa marefu hadi 1,550, idadi iliyo chini ya makubaliano ya awali, na kuidhinisha ukaguzi wa vituo vya nyuklia.
Makubaliano hayo yalianza kutekelezwa mwaka 2011 na kuongezewa miaka 10 zaidi. Lakini, ukaguzi wa silaha uliingiliwa na janga la covid.
Wapinzani hao wawili wa zamani wa Vita Baridi wana takriban silaha zote za nyuklia duniani. Hapo awali Urusi ilisema inataka kuheshimu mkataba huo, licha ya maneno ya uhasama kutoka pande zote mbili wakati wa vita vya Ukraine.
Nini kinaweza kutarajiwa ?
Steve Rosenberg, mhariri wa BBC nchini Urusi, anasema kuwa kusitishwa kwa mkataba wa Moscow "kunaongeza hatari ya nyuklia" .
Neno "kuchochea" limekuwa "neno la Rais Putin," anasema Rosenberg.
Mkataba wa New Start "ulikuwa katika matatizo mwezi uliopita, Washington ilishutumu Moscow kwa kukiuka makubaliano kwa kukataa kuruhusu shughuli za ukaguzi katika eneo lake," anakumbuka mhariri wa BBC.
Ingawa Putin alisema hataanzisha majaribio ya nyuklia "kwanza," aliongeza kuwa "Marekani inafanya majaribio, tutajaribu pia."

Chanzo cha picha, Getty Images
Hatahivyo, Rosenberg anasema kuwa rais wa Urusi alitangaza kwamba alitia saini amri ya "kuweka maeneo mapya ya kimkakati katika huduma ya hifadhi ya kupambana."
Na alionya kuwa Urusi iko tayari kuanza tena majaribio ya silaha za nyuklia.
"Ni zaidi kuhusu ulaghai wa nyuklia, lakini ni hatari sana," anasema Andrei Kolesnikov wa Taasisi ya Carnegie Endowment for International Peace tank, "kwa sababu hatuwezi kutabiri jinsi Putin atakavyofanya katika siku zijazo na kile anachofikiria."
"Ili kuepuka vita vya nyuklia, ni bora kuwa na mfumo," aliongeza. "Kwa kupoteza mfumo huu tunashuhudia tishio halisi la vita vya nyuklia."
Jibu la Marekani
Kufuatia tangazo la Putin, Biden kutoka Poland alisisitiza dhamira ya NATO ya kushikamana ili kuhakikisha kuwa "hamu na kiu ya Putin ya ardhi na madaraka inashindwa."
"Putin hana shaka na nguvu ya muungano wetu, lakini anaendelea kutilia shaka imani yetu," rais wa Marekani alisema.

Chanzo cha picha, Reuters
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken aliutaja uamuzi wa Urusi kusitisha ushiriki wake katika mkataba huo "kama bahati mbaya na usiowajibika".
"Tutafuatilia kwa karibu kuona kile ambacho Urusi inafanya. Bila shaka tutahakikisha kwamba kwa vyovyote vile tuna mkao ufaao kwa usalama wa nchi yetu na washirika wetu," aliwaambia waandishi wa habari.
Lakini, Blinken aliacha mlango wazi ili kuanza tena mazungumzo wakati wowote.
"Tunasalia tayari kujadili vikwazo vya kimkakati vya silaha wakati wowote na Urusi, bila kujali kitu kingine chochote kinachotokea, duniani au katika uhusiano wetu," alisema.












