Urusi yafunga bomba kuu la gesi kwenda Ulaya

Urusi imesitisha kabisa usambazaji wa gesi kwenda Ulaya

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Urusi imesitisha kabisa usambazaji wa gesi kwenda Ulaya
Iliyochapishwa

Kampuni kubwa ya nishati inayomilikiwa na serikali ya Urusi, Gazprom, imesema vikwazo katika bomba la Nord Stream 1 vitadumu kwa siku tatu zijazo.

Urusi tayari imepunguza mauzo ya gesi kwa kiasi kikubwa kupitia bomba hilo.

Lakini inakanusha shutuma za kutumia nishati kama njia ya kuadhibu mataifa ya Magharibi kwa kuiwekea vikwazo kutokana na uvamizi wa Ukraine.

Bomba la Nord Stream 1 lina urefu wa kilomita 1,200 (maili 745) chini ya Bahari ya Baltic kutoka pwani ya Urusi karibu na St Petersburg hadi kaskazini-mashariki mwa Ujerumani.

Ilifunguliwa mnamo 2011, na inaweza kutuma kiwango cha juu cha mita za ujazo 170 za gesi kwa siku kutoka Urusi hadi Ujerumani.

Bomba hilo lilifungwa kwa siku 10 mwezi Julai - tena kwa ajili ya kufanyiwa maboresho, kulingana na Urusi - na hivi karibuni limekuwa likifanya kazi kwa uwezo wa 20% tu kwa sababu ya kile Urusi inaelezea kama vifaa vibovu.

Rais wa mdhibiti wa mtandao wa Ujerumani amesema nchi hiyo itaweza kukabiliana na hali hiyo - ikiwa Urusi itarejelea utoaji katika siku zijazo.

‘’Nadhani tutaweza kukabiliana nayo’’, Klaus Mueller aliambia Reuters.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

‘’Nina imani kuwa Urusi itarejea hadi 20% Jumamosi, lakini hakuna anayeweza kusema.’’

Viongozi wa Ulaya wanahofia kwamba Urusi inaweza kuongeza muda wa kukatiza usambazaji wa gesi hiyo katika jaribio la kuongeza bei ya gesi, ambayo tayari imeongezeka kwa kasi mwaka uliopita.

Kupanda kwa bei kunatishia kuongeza gharama ya maisha katika miezi ya msimu wa baridi, ambayo inaweza kulazimisha serikali kutumia mabilioni ili kupunguza mzigo kwa wananchi.

Siku ya Jumanne, Waziri wa Mpito wa Nishati wa Ufaransa Agnes Pannier-Runacher aliishutumu Urusi kwa ‘’kutumia gesi kama silaha ya vita’’.

Alikuwa akizungumza baada ya Gazprom kusema kuwa itasitisha utoaji wa gesi kwa kampuni ya nishati ya Ufaransa ya Engie.

Lakini msemaji wa Rais wa Urusi Vladimir Putin amekataa shutuma hizo - na kusisitiza kwamba vikwazo vya Magharibi vimesababisha usumbufu huo kwa kuharibu miundombinu ya Urusi.

Alisisitiza kwamba ‘’matatizo ya kiteknolojia’’ yanayosababishwa na vikwazo ndiyo kitu pekee kinachozuia Urusi kusambaza gesi kupitia bomba hilo, bila kutaja shida ni nini.

Mzozo wa hivi majuzi zaidi umekuwa juu ya magurudumu yaliyowasili Ujerumani baada ya kukarabatiwa huko Canada na ambayo Urusi ilikataa kuchukua tena, ikisema kuwa ilikuwa chini ya vikwazo vya Magharibi.

Ujerumani, hata hivyo, inakanusha hili.

Mapema mwezi huu, Waziri wa Uchumi Robert Habeck alisema bomba hilo lilikuwa likifanya kazi kikamilifu na kusema hakuna masuala ya kiufundi kama inavyodaiwa na Urusi.

Mapema wiki hii, Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen aliahidi kuingilia kati katika masoko ya nishati, akiuambia mkutano huko Slovenia kwamba ‘’hawafai tena kwa malengo yaliyopo’’.

‘’Tunahitaji mfumo mpya wa soko la umeme ambao unafanya kazi kweli na kuturudisha katika usawa,’’ alisema.

Kabla ya mzozo huo, Ujerumani ilikuwa imeidhinisha bomba la €10bn (£8.4bn) la Nord Stream 2 - ambalo linakwenda sambamba na jingine lenye jina kama lake - lakini ilisimamisha shughuli zake baada ya Urusi kutuma wanajeshi wake nchini Ukraine mwezi Februari.

Wiki iliyopita, BBC ilifichua kuwa Urusi imekuwa ikiteketeza gesi inayokadiriwa kufikia $10m (£8.4m) kila siku kwenye kiwanda karibu na mpaka wa Finland.