Makiivka: Urusi inalaumu shambulio la kombora kwa matumizi ya simu za wanajeshi

Chanzo cha picha, Getty Images
Urusi imesema shambulio la mwaka mpya la kombora lililoua takriban wanajeshi 89 wa Urusi lilitokea kwa sababu wanajeshi walikuwa wakitumia simu zao za rununu.
Ukraine ilishambulia chuo cha kujiunga na jeshi huko Makiivka, katika eneo linalokaliwa la Donetsk, muda mfupi baada ya saa sita usiku tarehe 1 Januari.
Matumizi ya simu zilizopigwa marufuku na wanajeshi yaliruhusu adui kupata shabaha yake, jeshi la Urusi sasa limesema.
Ingawa idadi ya watu waliouawa haijathibitishwa, ni idadi kubwa zaidi ya vifo vinavyotambuliwa na Urusi katika vita hivyo.
Ukraine inadai idadi hiyo ni kubwa zaidi, ikisema wanajeshi 400 waliuawa katika shambulio hilo na wengine 300 kujeruhiwa.
Urusi ilisema kwamba saa 00:01 kwa saa za huko katika Siku ya Mwaka Mpya, roketi sita zilirushwa kutoka kwa mfumo wa roketi uliotengenezwa na Amerika wa Himars katika chuo cha ufundi, mbili kati yao zilidunguliwa.
Naibu kamanda wa kikosi hicho, Lt Kanali Bachurin, alikuwa miongoni mwa waliouawa, jeshi la ulinzi lilisema katika taarifa kwenye Telegram mapema Jumatano.
Tume inachunguza hali iliyosababisha shambulio hilo, ilisema taarifa hiyo.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Lakini ni "dhahiri tayari" kwamba sababu kuu ya shambulio hilo ilikuwa uwepo na "matumizi makubwa" ya simu za rununu na wanajeshi ‘
"Jambo hili liliruhusu adui kupata na kushambulia eneo la wanajeshi kwa shambulio la kombora."
Maafisa watakaopatikana na hatia katika uchunguzi huo watafikishwa mahakamani, taarifa hiyo iliongeza, na hatua zinachukuliwa kuzuia matukio kama hayo katika siku zijazo.
Urusi pia iliongeza idadi ya wanajeshi wake waliouawa katika shambulio hilo hadi 89 - kutoka 63 - ingawa hakuna njia ya kuthibitisha ni wanajeshi wangapi waliuawa. Ni nadra sana kwa Moscow kudhibitisha majeruhi wowote kwenye uwanja wa vita.
Chuo hicho cha ufundi kilijaa watu walioandikishwa wakati huo - wanaume ambao walikuwa kati ya 300,000 walioitwa katika uhamasishaji wa watu kujiunga na vita uliofanywa na Rais Vladimir Putin mnamo Septemba. Risasi pia zilikuwa zikihifadhiwa karibu na eneo hilo, ambalo lilikuwa limeharibiwa na kuwa kifusi.

Chanzo cha picha, Reuters
Baadhi ya wachambuzi na wanasiasa wa Urusi wamelishutumu jeshi kwa kutokuwa na uwezo, wakisema kuwa wanajeshi hao hawakupaswa kamwe kupewa makao hayo katika sehemu moja .
Pavel Gubarev, afisa mkuu wa zamani katika mamlaka ya uwakilishi ya Urusi huko Donetsk, alisema uamuzi wa kuweka idadi kubwa ya wanajeshi katika jengo moja ni "uzembe na uhalifu".
"Ikiwa hakuna mtu atakayeadhibiwa kwa hili, basi itakuwa mbaya zaidi," alionya.
Naibu spika wa bunge la eneo la Moscow, Andrei Medvedev, alisema ilitabirika kwamba wanajeshi hao wangelaumiwa badala ya kamanda aliyefanya uamuzi wa awali wa kuwaweka wengi wao katika sehemu moja.
Rais Putin alitia saini amri siku ya Jumanne kwa familia za wanajeshi waliouawa wakiwa kazini kulipwa rubles 5m (£57,000; $69,000).















