Kifo cha mtoto wa Davido : Je, janga hili linaweza kuboresha usalama wa waogeleaji Nigeria?

Kuzama kwa mtoto wa miaka mitatu wa nyota wa Afrobeats Davido kwenye bwawa la kuogelea nyumbani kwake mjini Lagos mwezi uliopita kumeweka bayana juu ya usalama wa waogeleaji nchini Nigeria.
Kifo cha Ifeanyi Adeleke kilikuja miaka minne baada ya mtoto wa mwaka mmoja wa mwimbaji mwingine wa Nigeria, D'Banj, kufariki katika mazingira kama hayo.
Kupata bwawa la kuogelea nchini Nigeria ni nadra, na hasa hifadhi ya matajiri, lakini ni jambo ambalo wengi wanatamani kuchukua hatua za kimsingi za usalama na kujua jinsi kuogelea kunaweza kuwa muhimu kuokoa maisha.
Ingawa jiji lao limezungukwa na maji - rasi nyingi na njia za maji, na vile vile Bahari ya Atlantiki - watu wengi wa Lagos hawawezi kuogelea.
"Hiki ni kifo kimoja ni kikubwa mno," anasema Bolanle Edwards wa Wakfu wa Strap and Safe Child Foundation wenye makao yake Lagos, akimaanisha mtoto wa Davido.
Amekuwa akitoa wito wa kuongezwa kwa usalama kwenye bwawa la kuogelea kwa watoto kote nchini kwa zaidi ya muongo mmoja. "Hii imekuwa ikitokea mfululizo kuanzia 2018 hadi 2022 ... katika hoteli, ufuo na nyumba binafsi pia," anaongeza.

Chanzo cha picha, AFP
Masuala mawili ni muhimu:
- Kuongeza usalama karibu na mabwawa na fukwe.
- Kujifunza jinsi ya kuogelea.
Walinzi wa ufuo waliofunzwa
Katika moja ya maeneo mazuri ya bahari ya Lagos kulikuwa na ufahamu wazi kuhusu dondoo hizi. Wazazi wakiwatazama watoto wao wakirusha maji kwenye mawimbi yenye povu ya Landmark Beach walitafakari habari kuhusu mtoto wa Davido.
"Nilihuzunika sana kwa sababu si jambo unalotamani kwa mtu yeyote," alisema Femi Nedd ambaye watoto wake watatu waliandikishwa katika madarasa ya kujifunza jinsi ya kuogelea kabla ya kutembea.
"Kuogelea sio anasa, ni ujuzi wa maisha kwa sababu unaweza usijue wakati unauhitaji."
Ingawa watoto wake wamekuwa wakiogelea bila kusaidiwa tangu wakiwa na umri wa miaka minne, anasema usimamizi ni muhimu na kuwepo kwa waokoaji waliofunzwa katika fuo za umma wanazotumia kunampa hakikisho.
Adeola Folivi alisema binti yake mwenye umri wa miaka 12, shabiki wa Davido, alifadhaika aliposikia kilichompata mtoto wa kiume wa nyota huyo - na alijifunza umuhimu wa masomo ya kuogelea.
"Ninawahimiza wapwa zangu na watoto wa rafiki yangu kujiandikisha katika masomo ya kuogeleamradi tu yafanywe katika mazingira yanayofaa, na tahadhari zinazofaa kuchukuliwa, na vifaa vinavyofaa vya usalama," alisema.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wale walio na mabwawa binafsi ya kuogelea pia wamekumbwa na habari za kuzama. Adekunle Akanbi, ambaye anashiriki kutumia bwawa la kuogelea na jirani yake katika mji wa kusini-magharibi wa Ibadan, aliingiwa na wasiwasi sana baada ya kusikia kuhusu mkasa wa Davido.
Aliiambia BBC kwamba watoto katika nyumba yake sasa watafuatiliwa kwa karibu zaidi karibu na bwawa: "Wanaweza kuogelea kikamilifu lakini bado chini ya uangalizi mzuri." Hii ni sawa kwa Nora Chukwuma katika jiji la Port Harcourt kusini-mashariki. Alisema milango yote inayoelekea eneo la bwawa lake ilikuwa imefungwa vizuri ili kuwazuia watoto kukaribia maji bila mtu mzima kuwepo.
"Kwa sasa tunafanya kazi ya kufunga kizuizi cha bwawa," aliongeza.
Takwimu za kuzama kwa maji nchini Nigeria ni ngumu kupatikana lakini mwanaharakati wa usalama Bi Edwards anasema kuwa linapokuja suala la mabwawa ya kuogelea, kumeripotiwa vifo 18 vya maji katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Nane kati ya hizo zilitokea mwaka huu pekee. Shirika la Afya Duniani (WHO) limeorodhesha kuzama kwa maji kuwa chanzo cha tatu cha vifo vinavyotokana na majeraha bila kukusudia duniani kote.
Inasema takribani watu 236,000 hufa kutokana na kuzama kila mwaka.
Takribani 90% ya vifo hivi hutokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati kama Nigeria.
Katika jitihada za kuzuia ajali kama hizo, serikali ya jimbo la Lagos mwezi Septemba iliwataka waendeshaji wa mabwawa ya kuogelea na wamiliki wa fukwe kuimarisha hatua za tahadhari karibu na vituo vyao.
Mnamo mwaka wa 2017 ilianzisha kanuni za usalama za jimbo zima ambazo zilitaka kupiga marufuku uendeshaji wa huduma ya bwawa la kuogelea bila ruhusa na mlinzi mahali pake.
Lakini bila utekelezaji sahihi na mashtaka haya mara nyingi hupuuzwa. Bi Edwards anasema tangu kuanzishwa kwa waokoaji waliofunzwa, sasa kuna ajali chache katika fuo binafsi za Lagos.
Lakini kuna majimbo machache ambayo yana kanuni sawa katika maeneo mengine ya nchi.
Mafunzo ya gharama kubwa
Ujuzi kuhusu jinsi ya kuogelea, pamoja na hatari za maji, haujaenea.

Chanzo cha picha, TOUGH ATELEMO
Mnamo mwaka 2014 jeshi la wanamaji la Nigeria lilisema lilikuwa likianzisha masomo ya lazima ya kuogelea kwa maafisa wake wote baada ya kugundua wafanyakazi wengi hawakuwa waogeleaji wazuri.
Kwa vile kuogelea ni ujuzi wa kuishi, wazazi wanahitaji kuuzingatia kuwa muhimu kama ujuzi mwingine, anasema mwalimu wa kuogelea Tough Atelemo, ambaye amefundisha mamia ya watoto wadogo, wengine wakiwa na umri wa miezi sita katika miongo miwili iliyopita.
"Unapomfundisha mtoto, unapaswa kumfundisha jinsi ya kuishi," anasema. Hata hivyo, anakubali kwamba kwa bei ya takriban $220 (£200) kwa masomo 10, Wanigeria wengi hawaudu.
Anaongeza kuwa inapaswa kujumuishwa katika mtaala wa shule wa miaka ya mapema, ambayo pia ni pendekezo la WHO.
Kuweka ngome za ulinzi, mabwawa ya kufunika, uzio katika mabwawa ya kuogelea na kuwaweka watoto kwenye uangalizi wanapokuwa karibu na maji ni baadhi ya hatua za vitendo ambazo zinaweza kupunguza hatari zinazozunguka maji, WHO inasema.
Bi Edwards anaunga mkono hili, akisema kwamba mabwawa ya kuogelea yanapaswa kuwa na uzio kila upande unaowatenganisha na nyumba.
Teknolojia, kama vile taa zinazowashwa kwa mwendo na CCTV, zinaweza pia kusaidia kuwalinda watu, hasa watoto, kutokana na hatari ya kuzama, anasema mbunifu Daniel Ette.
Haijulikani ni aina gani za hatua za usalama zilikuwa zikiwekwa nyumbani kwa Davido.
Uchunguzi wa maiti ulihitimisha kuwa mtoto wake alikufa kwa kuzama lakini uchunguzi unaendelea.
Wanapitia picha za CCTV za nyumba hiyo, huku wakiwa wamemshikilia yaya wa Davido na mpishi chini ya ulinzi kwa mahojiano zaidi.













