Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Israel na Gaza: Hatma isiyojulikana ya Hind Rajab mwenye umri wa miaka sita aliyekwama katika mapigano
Upande wa pili wa mapigano ilisikika sauti ndogo na dhaifu; sauti ya mtoto wa miaka sita, ikisikika kwenye simu ya mkononi kutoka Gaza.
"Kifaru cha kijeshi kiko karibu nami. Kinasonga."
Akiwa ameketi katika kituo cha simu za dharura cha shirika la Msalaba mwekundu la Palestina, Rana alijaribu kuzungumza kwa utulivu.
"Je, ni karibu sana?"
"Sana, sana," sauti ndogo ilijibu. "Utakuja kunichukua? Ninaogopa sana."
Hakukuwa na kitu ambacho Rana angeweza kufanya isipokuwa kuendeleza mazungumzo.
Hind Rajab mwenye umri wa miaka sita alikwama katika mapigano katika Jiji la Gaza na kuomba msaada, akijificha ndani ya gari la mjomba wake, akiwa amezungukwa na miili ya jamaa zake.
Hind alikuwa ameondoka nyumbani kwake katika Jiji la Gaza mapema siku hiyo akiwa na mjomba wake, shangazi yake na binamu zake watano.
Ilikuwa Jumatatu tarehe 29 Januari. Asubuhi hiyo, jeshi la Israel lilikuwa limewaambia watu kuhama maeneo ya magharibi mwa mji na kuelekea kusini kando ya barabara ya pwani.
Mama yake Hind, Wissam, anakumbuka kulikuwa na mashambulizi makali ya makombora katika eneo lao. "Tuliogopa, na tulitaka kutoroka," alisema. "Tulikuwa tukikimbia kutoka sehemu moja hadi nyingine, kukwepa mashambulizi ya anga."
Familia iliamua kuelekea katika Hospitali ya Ahli iliyoko mashariki mwa jiji, wakitarajia pangekuwa mahali salama pa kujihifadhi.
Wissam na mtoto wake mkubwa walianza kwenda huko kwa miguu; Hind alipewa nafasi katika gari la mjomba wake, Kia Piccanto nyeusi.
"Kulikuwa na baridi sana na mvua," Wissam alieleza. "Nilimwambia Hind aende kwenye gari kwa sababu sikutaka ateseke kwenye mvua."
Mara tu gari lilipoondoka, alisema, walisikia sauti ya risasi ikitoka upande huo huo.
Wakati mjomba wa Hind akiendesha kuelekea katika Chuo Kikuu maarufu cha al-Azhar cha jiji hilo, gari hilo linadhaniwa kuwa lilikutana uso kwa uso na vifaru vya Israel. Wakaingia kwenye kituo cha petroli cha Fares kilicho karibu kwa ajili ya usalama wao, na walionekana kupigwa risasi.
Ndani ya gari, familia ilimpigia simu ndugu kuomba msaada. Mmoja wao aliwasiliana na makao makuu ya dharura ya Shirika la Msalaba Mwekundu la Palestina, lililokuwa umbali wa maili 50 (80km) katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Ilikuwa saa nane unusu kwa saa za eneo (12:30 GMT): wahudumu katika kituo cha simu cha Red Crescent huko Ramallah walipiga simu ya mjomba wa Hind, lakini binti yake mwenye umri wa miaka 15, Layan, alijibu badala yake.
Katika simu iliyorekodiwa, Layan anawaambia wafanyakazi wa Shirika la Msalaba Mwekundu kwamba wazazi wake na ndugu zake wote wameuawa, na kwamba kuna kifaru cha kijeshi kilichopo karibu na gari. "Wanatufyatulia risasi," anasema, kabla ya mazungumzo kuishia kwa milio ya risasi na mayowe.
Timu ya Msalaba Mwekundu ilipofika, ni Hind aliyejibu, sauti yake karibu isisikike, ilizama kwa hofu.
Hivi karibuni inakuwa wazi kuwa yeye ndiye pekee aliyenusurika kwenye gari, na kwamba bado yuko kwenye eneo la mapigano.
"Jifiche chini ya viti," timu Shirika la Msalaba Mwekundu ilimwambia. "Usiruhusu mtu yeyote akuone."
Opereta Rana Faqih alikaa kwenye mstari na Hind kwa saa nyingi, huku Shirika la Hilali Nyekundu likitoa wito kwa jeshi la Israeli kuruhusu gari lao la wagonjwa kufikia eneo hilo.
"Alikuwa akitetemeka, huzuni, akiomba msaada," Rana alikumbuka. "Alituambia [jamaa zake] walikuwa wamekufa. Lakini baadaye aliwaelezea kama 'waliolala'. Hivyo tukamwambia 'waache walale, hatutaki kuwasumbua'."
Hind aliendelea kuomba , tena na tena, mtu aje kumchukua.
"Wakati mmoja, aliniambia kumekucha," Rana aliiambia BBC. "Aliogopa. Aliniuliza nyumba yangu ilikuwa mbali kiasi gani. Nilihisi kupooza na kukosa la kufanya."
Saa tatu baada ya simu kuanza, hatimaye gari la kubebea wagonjwa lilitumwa kumuokoa Hind.
Wakati huo huo, timu ya Msalaba Mwekundu ilikuwa imemfikia mama yake Hind, Wissam, na kumuwekea laini ya simu yake kwenye simu hiyo.
Alilia zaidi aliposikia sauti ya mama yake, Rana anakumbuka.
"Alinisihi nisikate simu," Wissam aliiambia BBC. "Nilimuuliza alijeruhiwa wapi, kisha nikammliwaza kwa kusoma naye Quran, na tukaswali pamoja. Alikuwa akirudia kila neno nililolisema baada yangu."
Ilikuwa ni baada ya giza wakati wafanyakazi wa ambulensi - Yousef na Ahmad - waliwajulishawahudumu kuwa walikuwa wanakaribia eneo hilo, na walikuwa karibu kufanyiwa msako na vikosi vya Israeli ili waingie.
Ilikuwa w ni mara ya mwisho kupata taarifa kutoka kwa wahudumu - au kutoka kwa Hind. Mawasiliano kutoka kwa wahudumu wa afya wote wawili, na kwa msichana wa miaka sita waliyekuja kumuokoa yalikatika na hayakupatikana tena.
Babu yake Hind, Bahaa Hamada, aliiambia BBC kwamba mawasiliano ya msichana huyo na mama yake ulidumu kwa dakika chache zaidi, na kwamba jambo la mwisho ambalo Wissam alisikia ni sauti ya mlango wa gari ukifunguliwa, na Hind alimwambia kwamba aliweza kuona gari la wagonjwa kwa umbali.
"Kila sekunde, moyo wangu unauma," Wissam aliiambia BBC. "Kila wakati ninaposikia sauti ya ambulensi, nadhani, 'labda ni yake.' Kila sauti, kila risasi, kila kombora linaloanguka, kila bomu - nahisi ni kama linaelekea kwa binti yangu, najiuliza ikiwa amepigwa au la."
Si wa Shirika la Mslaba Mwekundu huko Gaza, wala familia ya Hind, hakuna aliyeweza kufika eneo hilo, ambalo bado liko ndani ya eneo la mapigano likidhibitiwa na jeshi la Israeli.
"Ni vigumu usiku," mhudumu wa simu Rana alisema, "unapoamka na kusikia sauti yake katika sikio lako, akisema 'njoo unichukue'".
Tuliliuliza jeshi la Israeli kwa maelezo ya operesheni zake katika eneo hilo siku hiyo, na kuhusu kutoweka kwa Hind na ambulensi iliyotumwa kumchukua. Tuliuliza tena saa 24 baadaye, na wakasema bado walikuwa wakiangalia.
"Mahakama ya Kimataifa iko wapi? Mbona marais wamekaa kwenye viti vyao?" Mama yake Hind, Wissam, aliuliza.
Wiki moja baada ya kutoweka kwa binti yake, Wissam anakaa na kusubiri katika hospitali ya Ahli, siku baada ya siku, huku matumaini ya kumpata Hind akiwa hai yakiendelea kutoweka.
"Nimeleta vitu vyake, na ninamsubiri hapa," alisema. "Namsubiri binti yangu dakika yoyote, sekunde yoyote. Ninaomba kutoka kwa moyo wa mama uliovunjika usisahau hadithi hii."
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi