Unajua hatari ya kumpa mtoto lishe ya mboga mboga pekee bila nyama?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kesi ya Sheila O'Leary, mama aliyehukumiwa kifungo cha maisha gerezani nchini Marekani kwa tuhuma za kumuua mtoto wake mwenyewe kwa utapiamlo na upungufu wa maji mwilini baada ya kumpa lishe yenye matunda, mboga mbichi na maziwa ya mama pekee, ilizua mashaka miongoni mwa wazazi.
Je, inawezekana kulisha watoto wadogo mlo wa mboga bila nyama wala bidhaa zozote za wanyama tu?
Miongoni mwa taasisi za matibabu kama vile Chuo cha Marekani cha Madaktari wa Watoto na Jumuiya ya Madaktari wa Watoto ya Brazil (SBP) - pendekezo ni kuepuka mlo ambao hauna chanzo chochote cha asili ya wanyama hadi umri wa miaka miwili.
Lakini wataalam wanakubali kwamba, ndiyo, unaweza hata kuondoa nyama, mayai, maziwa na bidhaa nyingine za wanyama kutoka katika chakula cha watoto wako - lakini unapaswa kuchukua tahadhari kubwa ili kuhakikisha wanapata virutubisho vya kutosha, vitamini na madini.
Hii inahusisha kuchagua viungo vinavyoenda kwenye meza na wakati mwingine, hata kusindikiza na ziada ya vidonge na sindano.
Utaratibu huu wote lazima ufuatiliwe kwa karibu na wataalamu wa afya, kama vile madaktari wa watoto na lishe ili kuepuka matatizo katika maendeleo ya mwili na akili.
"Miaka miwili ya kwanza ya maisha ni kipindi muhimu, ambapo ubongo na mwili wa mtoto hukua sana na uhitaji aina mbalimbali za virutubisho", anaeleza daktari Fabíola Suano, rais wa Idara ya Sayansi ya Nutrology katika SBP.
"Yaani, upungufu wa lishe katika hatua hii unaweza kuleta hatari kwa maisha", anaongeza.
Ukosefu wa baadhi ya michanganyiko hii ambayo huonekana pekee au kwa wingi zaidi katika vyakula vya asili ya wanyama, kama vile vitamini B12, madini ya chuma na kalsiamu, kwa mfano, inahusiana na upungufu katika ukuaji wa mfupa na matatizo katika malezi ya miundo muhimu ya ubongo kwa kumbukumbu, kujifunza na kufikiria.
Haya ni mapendekezo muhimu ya wataalam na jinsi wazazi na mama ambao hawatumii bidhaa zitokanazo na wanyama wanaweza kuhakikisha watoto wao wana afya njema, ikiwa wanataka kuwaweka mbali na nyama, mayai, maziwa na kadhalika wakati wa utoto.
Utata mezani
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mashirika kama vile Shirika la Afya Duniani na Wizara ya Afya yanapendekeza kwamba mtoto apewe maziwa ya mama pekee hadi mwezi wa sita ya mwanzo baada ya kuzaliwa
Katika hatua hii, mlo wa mama unaweza kuleta mabadiliko yote: kwani virutubisho muhimu humfikia mtoto kupitia maziwa ya mama, ni muhimu kwamba mwanamke ale vizuri na awe na viwango vya kutosha vya vitamini na madini.
"Mara nyingi, mama anayetumia lishe isiyo na bidhaa za nyama anahitaji kuchomwa sindano za vitamini B12, ili kuhakikisha kuwa kiungo hiki kipo kwenye maziwa yake", anatoa mfano Suano, ambaye pia ni profesa katika Idara ya Madaktari wa Watoto katika Chuo Kikuu cha Shirikisho cha São Paulo (Unifesp).
Kama kunyonyesha haiwezekani, mbadala katika kesi hizi ni kutumia maziwa ya formula yenye protini hidrolisisi mchele au soya yenye protini pekee.
Kunyonyesha, kunaendelea kupendekezwa hadi umri wa miaka miwili - katika kipindi hiki, hata hivyo, ni vizuri kuanzisha vyakula vingine kidogo kidogo.
Hapa ndipo wazazi wengi wanaotumia lishe ya mboga mboga au vegan wana tia shaka: inawezekana kutenga baadhi au bidhaa zote za wanyama katika lishe ya watoto wao? Mwongozo wa hivi karibuni wa SBP juu ya mada hii, iliyochapishwa mwaka wa 2017, inakubali kwamba "mlo wa mboga wenye virutibisho vyote una uwezo wa kukuza ukuaji na maendeleo katika utoto na ujana".
"Hata hivyo, kwa kuwa wako katika hatari zaidi ya kupata upungufu wa virutubisho, [watoto hawa] lazima wafuatiliwe vya kutosha na mara nyingi kuongezwa virutubisho vya ziada, kwa kuwa hatari ni usawa na aina ndogo za vyakula vinavyotumiwa", maandishi yanaonyesha.
Lishe ya vegan haswa, ambayo hupunguza bidhaa zote za wanyama, hutazamwa kwa kutoridhishwa katika miaka hii miwili ya kwanza ya maisha.
"Ni muhimu kuzungumza na familia na kutafuta njia ya kati. Ikiwa wazazi hawataki kuwapa nyama nyekundu, si inawezekana kuandaa samaki au yai?", anapendekeza Suano.
"Ikiwa kati ya miezi sita na miaka miwili mtoto anakabiliwa na mlo usio na bidhaa za nyama kabisa, ana upungufu chakula na lishe," anaamini daktari.
Daktari wa watoto anasema kuwa mjadala huu ni mbali na kufikia makubaliano, hata kati ya wataalamu katika sekta hiyo.
"Taasisi nyingine zinasema kwamba, ndiyo, inawezekana kupitisha ulaji mboga katika umri wa miezi sita, wakati wengine wanaona hiyo kuwa hatari na yanapingana", analinganisha.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Lakini kuna angalau kuna kauli moja katika taasisi zote: familia inayochagua kupunguza au kukata kabisa matumizi ya nyama, maziwa na mayai kwa watoto lazima ifuatiliwe kwa makini sana."
Mwongozo huu unapatikana hata katika chapisho la Brazilian Vegetarian Society.
Kama aina yoyote ya maisha, kuondoa viungo vya wanyama kuna faida na hasara zake.
Kwa upande mmoja, lishe kama hiyo inahusiana na matumizi ya kalori chache na mafuta yaliyojaa, ambayo hupunguza hatari ya hali kama vile ugonjwa wa uzito kupita kiasi na magonjwa ya moyo na mishipa katika utoto na maisha yote.
Kiwango cha juu cha nyuzi lishe kinatoka kwenye mboga mboga, pia ni nzuri katika mfumo wa usagaji chakula - ingawa hii inaweza kuingiliwa kati na ufyonzwaji wa baadhi ya madini.
Kwa upande mwingine, kutokuwepo kwa nyama, mayai na bidhaa za maziwa kwenye mlo inaleta hatari ya ukosefu wa madini ya chuma, vitamini B12, kalsiamu na zinki katika mwili.
Suala kubwa, wataalam wanaeleza, ni kwamba baadhi ya viinilishe vidogo hivi hupatikana zaidi katika bidhaa za wanyama - matunda na mboga hata hubeba kiasi kizuri, lakini upatikanaji wao wa kibayolojia (au sehemu ambayo miili yetu inachukua kutoka kwao) ni ya chini. .
Jinsi ya kuepuka matatizo
Inahitajika pia kuzingatia kuwa lishe yenye kalori ya chini au mafuta kidogo sio habari njema kila wakati. Baada ya yote, watoto wanahitaji virutubisho hivi kwa kipimo sahihi ili kukua vizuri na afya.
Mapitio ya tafiti zilizofanywa katika Hospitali ya das Clínicas de Ribeirão Preto, huko São Paulo, ilionyesha kuwa watoto wanaofuata lishe ya mboga isiyokuwa na nyama huwa wafupi na wembamba, ingawa urefu na uzito wao wa wastani bado uko ndani ya kiwango kinachochukuliwa kuwa cha kawaida.
Wasiwasi mwingine wa mara kwa mara wa wataalam ni ukosefu wa virutubishi vidogo vidogo muhimu kwa afya.
Upungufu wa madini haya unahusiana na "mabadiliko katika ukuaji wa neuropsychomotor, mfumo wa kinga dhaifu na kupungua kwa uwezo wa kufanya kazi", imeorodhesha katika chapisho la SBP.
Ili kuhakikisha uwepo wa madini chuma kwenye lishe, inawezekana kuanza na mikakati rahisi, kama vile kuloweka maharagwe kwa masaa 12.
Wazo lingine ni kula mboga zenye madini haya, kama vile dengu, maharagwe na njegere, pamoja na vyanzo vya vitamini C, kama vile machungwa na ndimu, ambayo huongeza unyonyaji wa madini chuma katika miili yetu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Calcium, iliyopo katika maziwa na baadhi ya bidhaa za maziwa, ni muhimu kwa ajili ya muundo wa mifupa ambayo inasaidia mwili na kuhakikisha mwendo wa miguu.
Inawezekana hata kupata madini haya katika baadhi ya mboga, lakini upatikanikaji wake pia ni kikwazo muhimu.
Kwa watoto ambao wako kwenye mlo wa vegan usio na bidhaa za wanyama kabisa, njia salama zaidi ni ziada ya Calcium, ambayo inahakikisha usambazaji wa kutosha kwa ajili ya ukuaji wa mifupa.
Mapendekezo sawa huenda kwa vitamini B12, ambayo inaonekana tu katika nyama, offal na mayai. Virutubisho vingine vidogo vinavyohitaji uangalizi wa ziada katika muktadha huu ni zinki, iodini, vitamini A, asidi ya foliki, vitamini D na omega 3. Wengine, wanaendelea kutumia ziada katika njia ya vidonge na sindano.
"Tunajua kwamba ulaji wa Vegan yaan mlo usio kuwa na bidhaa zozote za wanyama kumeongezeka sana katika miaka ya hivi karibuni, iwe kwa sababu ya kutafuta lishe bora au kujali mazingira", anachambua Suano. "Na sisi, kama wataalamu wa afya, tunahitaji kuzungumza na familia, kuelewa maoni yao na kufikia msingi wa kuridhisha na wa afya kwa wote wanaohusika", anahitimisha daktari wa watoto.















