Watu wenye asili ya Asia walioishi Uganda wakumbuka waliyopitia miaka 50 iliyopita

Bhavna Patani
Maelezo ya picha, Bhavna Patani alikuwa msichana wa shule wakati familia yake ililazimika kutoroka nyumbani kwao Uganda.
Iliyochapishwa

Miaka 50 baada ya Waasia wa Uganda kulazimishwa kuondoka nchini mwao na Idi Amin, baadhi yao walioishi Uingereza wanakumbuka hofu na kiwewe cha safari yao ya kuelekea eneo lenye usalama.

Mnamo Agosti 1972, makumi ya maelfu ya Waasia walipewa siku 90 kuondoka na £50 tu na begi.

Bhavna Patani alikuwa na umri wa miaka 13 tu wakati agizo lilipotolewa.

Anasimulia kuona maiti zikielea kwenye mito na kupekuliwa na maafisa wenye silaha huku familia yake ikikimbia.

Bi Patani
Maelezo ya picha, Familia ya Bi Patani imekuwa wamiliki wa kiwanda cha mtindi huko Coventry

“Nilikuwa shuleni Kampala na tulikuwa tunajivinjari wakati walimu wetu walipotuletea habari,’’ alisema.

Familia yake, ambayo hatimaye iliishi Coventry, ilikuwa ikiishi katika mji wa mashariki wa Tororo, ambapo waliendesha kiwanda cha mafuta na sabuni, walipoambiwa ‘’fungeni virago vyenu na muondoke,’’ alielezea.

Familia yaokubwa iliishi Tororo katika maeneo ya juu ya maduka ya kukodi.
Maelezo ya picha, Familia yaokubwa iliishi Tororo katika maeneo ya juu ya maduka ya kukodi.

Walikuwa wamefaulu kufunga baadhi ya vitu vya nyumbani kwenye vigogo ili kupeleka kwa familia zao nchini Kenya, lakini walizuiwa na kupekuliwa katika kituo cha treni cha mji huo‘’na wanajeshi watatu waliokuwa na bunduki’’.

‘’Walipekua kila begi ili kuhakikisha kuwa hatukuchukua pesa au vitu vya thamani,’’ Bi Patani alisema.

‘’Sasa inaonekana kama ndoto, unaendelea na maisha yako, lakini wakati huo, kwa hakika, hali ilikuwa ya kutisha sana.’’

Bhavna Patani na familia yake wanaishi Coventry baada ya kukaa Brighton na Leicester.

Tangazo ‘’la kutisha’’ lililotolewa na Idi Amin katika kipindi cha siku 90 kwamba wasichana wote wa Asia ambao hawajaolewa hawawezi tena kuondoka nchini ‘’lilisababisha hofu katika jumuiya ya watu wenye asili ya Asia,lakini haikuwahi kutekelezwa kamwe.

Familia hatimaye ilifika Uingereza kwa usalama, na iliendelea kumiliki na kuendesha kiwanda cha mtindi cha SpringDale huko Coventry.

‘’Haijalishi utajiri na mali zimetoweka,’’ anasema.

‘’Nadhani umoja na upendo wa familia na marafiki umetuleta pamoja.’’

Zakyu Bedani
Maelezo ya picha, Zakyu Bedani alisema familia yake ikawa Waasia wa kwanza wa Uganda kuishi Nuneaton.

Baadhi ya Waasia 30,000 wa Uganda walio na pasipoti za Uingereza za ng’ambo waliowasili Uingereza na maeneo yaliyo karibu wote wamepewa hifadhi.

Zakyu Bedani kutoka Nuneaton alikuwa miongoni mwao.

Kulingana naye, awali, tangazo la rais lilichukuliwa kama mzaha.

‘’Hatukuamini’’, anasema, lakini familia yake hatimaye iliondoka katika mji wa Masaka mnamo Novemba 1972.

Alimuona baba yake akipigwa na wanajeshi kando ya barabara kwa kulipita gari la kijeshi.

Alipofika kwenye kambi ya makazi mapya huko Gaydon, karibu na Leamington Spa, Warwickshire, anasema familia yake iliambiwa kwamba ‘’Nuneaton au Bedworth pangekuwa mahali pazuri pa kuishi’’.

‘’Kwa hivyo tukawa Waasia wa kwanza wa Uganda huko Nuneaton,’’ Bw Bedani alisema.

‘’Tuna furaha sana sasa, tumefanya mahali hapa kuwa nyumbani kwetu’’.

Suresh Shah bado anasaidia kuendesha kampuni ya Shah huko Coventry, ambayo aliianzisha mnamo mwaka 1976.
Maelezo ya picha, Suresh Shah bado anasaidia kuendesha kampuni ya Shah huko Coventry, ambayo aliianzisha mnamo mwaka 1976.

Suresh Shah, pia kutoka mji wa Masaka, alisema familia yake ilikuwa ‘’ina huzuni sana’’ kwa kuondoka Uganda na kuacha duka lake la kuuza vyakula.

‘’Tuliacha gari letu, duka letu na nchi yetu nzuri,’’ mzee wa miaka 77 alisema.

Kama Bi Patini, Bw Shah na familia yake waliishi Coventry.

Ndani ya miaka mitano, familia hiyo ilifanikiwa kununua duka la bidhaa la India, ambalo bado anasaidia kuendesha hadi leo.

“Nilirejea Masaka takribani miaka mitatu iliyopita,” alieleza.

‘’Nina kumbukumbu nzuri, lakini ilikuwa ya kihisia.’’

Maelfu ya familia zikihamia Uingereza
Maelezo ya picha, Maelfu ya familia zikihamia Uingereza