Mzozo wa Ukraine: miji ya Severodonetsk na Lysychansk imesambaratishwa - Zelensky

Chanzo cha picha, Getty Images
Vikosi vya Ukraine vinavyoendelea kupambana katika mji wa mashariki wa Severodonetsk vimezidiwa na vikosi vya Urusi, Rais Volodymyr Zelensky amesema. Pande zote mbili zinapambana kuhodhi jiji hilo kwa mapigano ya ardhini na mtaani siku ya Jumatatu huku mizinga ya makombora ikivurumishwa kutoka juu.
Mapamano makali yanayoendelea huko na karibu na Lysychansk umefanya"miji hiyo kufa (kusambaratika)", Bw Zelensky alisema.
Ikiwa miji hiyo itashikiliwa na Urusi, malengo mawili ya kimkakati ya urusi itakuwa ni kupeleka vikosi katika eneo lote la Luhansk mashariki mwa Ukraine.Tangu iondoe vikosi vyake kutoka eneo la Kyiv mwezi Machi, Urusi imeelekeza upya juhudi zake za kijeshi katika eneo la Donbas la mashariki mwa Ukraine ikisonga polepole huko katika wiki za hivi karibuni.
Licha ya idadi kubwa ya Warusi, Bw Zelensky alisema wanajeshi wa Ukraine walikuwa wanaendelea kupambana na walikuwa na "kila nafasi" ya kujibu

Chanzo cha picha, Getty Images
Mashambulizi ya mizinga pia yameongezeka katika eneo jirani la Lysychansk, ambalo Bw Zelensky alisema alitembelea Jumapili kama sehemu ya ziara yake katika eneo la mashariki.
Mkzee mmoja mkazi katika jiji hilo, Oleksandr Lyakhovets, alisema kombora la Urusi lilipiga nyumba yake muda mfupi baadaye, na kuiteketeza kwa moto.
"Wanapiga risasi hapa bila kikomo... hali ni ya kutisha," mzee huyo mwenye umri wa miaka 67 aliliambia shirika la habari la AFP.

Vikosi vya Urusi vimepiga hatua polepole katika eneo la Donbas Mashariki mwa Ukraine katika wiki za hivi karibuni. Wanajeshi wao kwa sasa wanadhibiti karibu eneo lote la Luhansk pamoja na sehemu kubwa ya eneo jirani la Donetsk. Mikoa hiyo miwili inaunda Donbas.
Mapigano yamekuwa ya polepole na ya umwagaji damu pande zote mbili zikipata hasara kubwa ama kuathirika pakubwa.
Siku ya Jumatatu Uingereza ilithibitisha kuwa itapeleka makombora ya masafa marefu kwa mara ya kwanza Ukraine ikiwa ni sehemu ya misaada ya kijeshi ambayo inaituma Ukraine. Kuhusu hilo Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema anachukulia uwasilishaji wowote wa silaha za masafa marefu na nchi za Magharibi kuwa ni jaribio la makusudi la kurefusha mzozo huo ama vita hiyo.
Wapiganaji wa Azovstal
Huko Mariupol, ambayo ilitekwa na Urusi mnamo mwezi Mei baada ya kuzingirwa kwa muda wa miezi kadhaa, shirika la habari la Associated Press linaripoti kwamba makumi ya maiti za wanajeshi waliokuwa wakilinda kiwanda cha chuma cha Azovstal cha jiji hilo hatimaye zimerudishwa Kyiv kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya DNA.
Wanajeshi wengine walionusurika katika tukio hilo la kuzingirwa na kushambuliwa na Urusi walipelekwa katika maeneo yanayotawaliwa na Urusi. Siku ya Jumatatu, Bw Zelensky alisema kuwa zaidi ya wanajeshi 2,500 kati yao walikuwa wakishikiliwa kama wafungwa wa kivita.
Wakaazi katika mji wa bandari unaodhibitiwa na Urusi sasa wamekuwa wakikabiliwa na mzozo wa kibinadamu unaoongezeka, unaochangiwa na uhaba mkubwa wa chakula na maji.
Siku ya Jumatatu afisa wa Ukraine alisema uchafuzi kutoka kwa maiti zinazooza na takataka umesababisha mlipuko wa kipindupindu - na kusababisha kuwekwa karantini jiji zima.
"Tunaona jiji likifungwa," Petro Andryuschenko, ambaye ni mshauri wa meya wa jiji hilo, wa United News TV.
"Neno 'kipindupindu' linatajwa ndani ya jiji," aliongeza.
BBC haijaweza kuthibitisha madai haya kwa uhuru.
Urusi yaishambulia Ukraine: Mengi zaidi
- MOJA KWA MOJA:Biden amuonya Putin: ''Madikteta watagharamika
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine












