Mashambulizi ya genge la waendesha pikipiki Nigeria: Vifo vyaongezeka hadi 200

Chanzo cha picha, Getty Images
Takriban watu 200 katika jimbo la Zamfara kaskazini-magharibi mwa Nigeria wamezikwa baada ya wimbi la mashambulizi makali ya magenge ya watu wenye silaha kwa siku kadhaa.
Manusura waliiambia BBC kwamba majambazi waliokuwa wakiendesha pikipiki walishambulia kijiji baada ya kijiji, wakifyatua risasi kiholela.
Mashambulizi hayo yanaaminika kujibu mashambulizi ya anga ya kijeshi siku ya Jumatatu yaliyowalazimu baadhi ya magenge ya wahalifu kutoka misituni ambako walikuwa wamejificha.
Makundi hayo yameisumbua Zamfara na majimbo jirani kwa miaka kadhaa.
Magenge haya yanayojulikana kama makundi ya majambazi ni mitandao ya kisasa ya wahalifu ambao huendesha shughuli zao katika maeneo makubwa, mara nyingi huiba wanyama, kuteka nyara ili kupata fidia na kuua wale wanaowakabili.
Wiki hii, serikali iliwataja rasmi majambazi kuwa ni magaidi, na kuruhusu vikosi vya usalama kuweka vikwazo vikali zaidi kwa makundi na wafuasi wao.
Siku ya Ijumaa hapo iliripotiwa kuwa zaidi ya watu 100 waliuawa na watu wanaoshukiwa kuwa ni majambazi katika eneo hilo, baada ya watu 300 waliokuwa na pikipiki kufika katika jamii kama tisa kati ya Jumanne na Alhamisi usiku.

Watu wenye silaha walichoma nyumba na kukata miili ya wahanga wao katika shambulio hilo.
Mwanakijiji Idi Musa aliliambia shirika la habari la AFP kwamba washambuliaji pia waliiba karibu ng'ombe 2,000.
Vyombo vya habari vya ndani viliripoti kwamba makundi yenye silaha yalikuwa yanahusikia katika mashambulizi hayo yalionekana kusonga mbele - kuelekea upande wa magharibi wa jimbo la Zamfara baada ya kuacha maficho katika maeneo ya misitu ili kukabiliana na mashambulizi endelevu ya serikali.
Msemaji wa Waziri wa Masuala ya Kibinadamu Sadiya Umar Farouq ameliambia shirika la habari la AFP kuwa zaidi ya watu 200 wamezikwa.
Pia alithibitisha kuwa zaidi ya watu 10,000 wameachwa bila makao na wengi bado hawajulikani walipo.
Wakati huohuo, maafisa katika jimbo jirani la Kebbi walisema majambazi wamewaachilia watoto wengine 30 wa shule na mwalimu mmoja ambao walikuwa wamezuiliwa kwa miezi sita. Haijulikani ikiwa fidia ililipwa kwa ajili ya kuachiliwa kwao.
Mnamo Juni, watekaji nyara walichukua wanafunzi 102 na walimu wanane kutoka shule moja katika jiji la Birnin Kebbi. Nambari ambayo haikutajwa tayari ilikuwa imeachiliwa mwaka jana, baada ya wazazi wao kufanya mazungumzo na watekaji.
Utekaji nyara kwa ajili ya fidia ni biashara kubwa ya uhalifu nchini Nigeria.
Simulizi iliyovuma wikendi hii kuhusu baba kutoka jimbo la Katsina, linalopakana na Zamfara mashariki, ambaye amekuwa akiondoa paa la nyumba yake ili kuuza mabati hayo ili kupata fidia ya takriban $250 (£180) kwa mwanawe.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mtoto wake alipoenda kuwalipa majambazi hao, ndipo alipochukuliwa mateka.

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari ameahidi kuwa serikali haitalegea katika vita vyake na "waharamia".
"Mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya watu wasio na hatia ni kitendo cha kusikitisha sana ,, sasa chini ya shinikizo kubwa kutoka kwa vikosi vyetu vya kijeshi," alisema katika taarifa yake Jumamosi usiku.
Vikosi vya jeshi la Nigeria vilisema wiki hii kwamba vimewaua "majambazi wenye silaha na wahalifu wengine 537" katika eneo hilo na kuwakamata wengine 374 tangu Mei mwaka jana.
Maelfu ya wanajeshi wa Nigeria wametumwa kupambana nao.















