Mwanamgambo mtoro wa Uganda: IS ilinilazimisha kupigana

Chanzo cha picha, AFP
Kundi la Allied Democratic Forces (ADF) limelaumiwa kwa mashambulizi ya hivi majuzi ya kujitoa mhanga katika mji mkuu wa Uganda. Mwandishi wa BBC Patience Atuhaire amekuwa akiongea na mwajiriwa wa zamani wa kundi hilo ili kuelewa zaidi kuhusu nini na ni nani yuko nyuma ya kundi hili lenye uhusiano na Islamic State.
Katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili akiwa mwanajeshi, ambaye aliingizwa huko kwa nguvu, alishuhudia kukatwa viungo na kukatwa vichwa, wakati mwingine kukilengwa na wenzake ili kuhakikisha watu hawakiuki.
"Kundi linaendeshwa kwa Sheria, ukiiba unapoteza mkono, ukimbaka mtoto unakufa, ukisema uongo juu ya mtu ukapatikana unakufa," anasema kwa msisitizo.
Hofu hii, pamoja na itikadi ya Kiislamu na kuanzishwa kwa uhusiano na kundi la Islamic State, kumefanya ADF kuwa kundi tishio kwa Uganda kwa mara nyingine tena.
Serikali, ambayo imejijengea urithi wake juu ya usalama, kwa miaka mingi ilikuwa imesema kuwa ADF ni jeshi lililoshindwa. Lakini hiyo haionekani kuwa kweli tena.

Chanzo cha picha, AFP
Msururu wa machafuko tangu Oktoba, yakiwemo mashambulizi pacha ya watu waliojitoa mhanga katikati mwa jiji la Kampala, yamesababisha vifo vya takribani watu wanane, wakiwemo wanamgambo watatu, na kujeruhi zaidi ya 40.
Hapo awali iliundwa na Waganda waliochukizwa na serikali katika miaka ya 1990 ambao walitaka kuwepo kwa msingi wa Kiislamu wa serikali nchini humo.
Lakini lilifurushwa na kuondolewa katika kambi zake katika eneo la magharibi la Rwenzori, ambako ilikuwa ikishambulia vijiji na kuchoma shule katika muongo wa kwanza wa Karne.
Waliobaki walikimbia kuvuka mpaka, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Hapo awali, wapiganaji wa ADF walifanya kazi na Jumuiya za wenyeji kuanzisha biashara, ambayo iliwafanya kupendwa na watu wengi karibu na mji wa Beni, kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa ya 2011. Lakini hiyo ilibadilika walipoanza kushambulia jamii za wenyeji.
Kuingizwa kwenye kundi kwa ulaghai
Miaka michache iliyopita, Peter, anayeishi Uganda, alivutiwa na uwezekano wa kupata kazi nchini DR Congo. Alikuwa amekutana na mtu ambaye aliahidi kwamba wanaweza kutengeneza pesa.
Peter alikuwa amedanganywa.
Sababu hasa iliyomfanya avuke mpaka ilimjia wakati, alipokuwa akisafiri huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, watu wenye silaha walitoka vichakani na kumwamuru aandamane nao.
Aliingizwa kinguvu kwenye kundi hilo, kwa mtutu wa bunduki.
"Sikuwa na muda wa kufahamu kilichokuwa kikitokea. Tulitumia njia kadhaa za usafiri, ikiwa ni pamoja na boti, kabla ya kufika kwenye kambi ya mafunzo.
"Ukifika wanakusomea sheria: ukijaribu kutoroka utakatwa kichwa, ukikataa mafunzo utakatwa kichwa," anaambia BBC.

Chanzo cha picha, AFP
Alikuwa sehemu ya kile ambacho serikali ya Uganda inaendelea kukiita ADF, lakini kundi lenyewe linasema linaitwa Madina huko Tauheed Wau Mujahedeen (MTM), ikimaanisha Jiji la Kuamini Mungu Mmoja na Wapiganaji Watakatifu.
MTM imeahidi utii kwa IS. "Huo ndio wakati ambapo [Abu Bakr] al-Baghdadi, kiongozi wa zamani wa IS, alikuwa bado hai. Wana kiongozi mmoja tu; serikali moja. Hatungefanya chochote, kama kushambulia kambi ya jeshi, kabla ya kupokea amri kutoka kwa wakuu. ," Peter anaeleza.
"Wapiganaji wote wanajua kwamba kiongozi wao mmoja ndiye mkuu wa IS. Wao ni jeshi la Mwenyezi Mungu."
Kupanga kutoroka ilikuwa ngumu kwani haikuwezekana kufanya kazi na mtu yeyote bila kuogopa kuripotiwa.
Wapiganaji watoto wasio na woga
Baadhi ya wapiganaji waliojitolea zaidi ni watoto kati ya miaka 10 na 15, anasema.
"Wale ni wepesi wa kujitolea kwa misheni. Hawana hofu, kwa sababu wanaamini mafundisho ya kwenda Janaah [mbinguni]. Wengi ni watoto wa Kongo, waliochukuliwa na familia wakati wa mashambulizi dhidi ya vijiji," anaelezea.
Uchunguzi wa Ofisi ya Pamoja ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa unaonyesha kuwa kati ya Januari 2019 na Juni 2020, raia 1,066 waliuawa na watoto 59 walioandikishwa na ADF katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri.
ADF ilibadilika na kuwa kundi lenye mtazamo wa kimataifa zaidi baada ya Musa Baluku, raia wa Uganda mwenye umri wa kati ya miaka 40, kurithi uongozi wa ADF baada ya kukamatwa na kurejeshwa nchini mwanzilishi wake Jamil Mukulu.
"Wakati Mukulu alianzisha ADF kwa nia ya kurejea Uganda ili kuanzisha serikali ya Kiislamu ambayo ingewavutia wapiganaji wenye mawazo kama hayo duniani kote, Baluku alitaka kuliweka ADF kama sehemu ya harakati pana za kimataifa," ripoti ya hivi majuzi kutoka. Mpango wa Chuo Kikuu cha George Washington kuhusu Misimamo mikali unasema.

Chanzo cha picha, AFP
Uhusiano wa kundi hilo na jihad ya kimataifa vinaonekana katika miaka ya 2017.
Katika video iliyotolewa kupitia Mujahidina TV mwaka jana, Bw Baluku alitangaza: "Hakuna ADF tena. Mwenyezi Mungu akipenda, ADF ilikoma kuwapo muda mrefu uliopita… Kwa sasa, sisi ni jimbo, Jimbo la Afrika ya Kati, ambalo ni jimbo moja kati ya majimbo mengi yanayounda Dola ya Kiislamu."
Chini ya uongozi wake, shirika hilo linasemekana kupata ufadhili kupitia mitandao ya kifedha ya IS.
"Lengo la kikundi hiki sio Uganda peke yake," anasema Peter, mpiganaji wa zamani.
"Lengo lao ni kuwa Uislamu utawale dunia nzima. Kuna wapiganaji wa Kitanzania, Wakenya, Wanyarwanda, Warundi, Wasomali, hata Waarabu."
Kutoroka kwenye mikono ya ADF
Hatimaye Peter alitoroka na kurejea Uganda miezi michache iliyopita. Amepokea msamaha rasmi wa serikali kupitia Tume ya Msamaha, akiwa mmoja wa wapiganaji 23 wa zamani wa ADF ambao wameomba msamaha tangu 2019.
Kwa ujumla, tume hiyo imewasamehe na kuwapa makazi mapya zaidi ya waasi 2,000 wa zamani tangu mwaka 2000.
Lakini bado wakiwa nchini DR Congo, wanamgambo hao wanaonekana kudhamiria kuanzisha upya kampeni yao nchini Uganda.

Chanzo cha picha, AFP
Mamlaka nchini Uganda zinasema kuwa wamefaulu kusambaratisha kile wanachokiita seli za ugaidi nchini kote; kutoka eneo la milima la Rwenzori hadi kwenye viunga vya makazi duni ya Kampala, jambo ambalo linaonyesha tishio lililoenea.
Waziri wa Usalama Meja Jenerali Jim Muhwezi anasisitiza kuwa mashambulizi mengi yanayoweza kutokea yamezuiwa. Lakini kuna wasi wasi kwamba kwa kuungwa mkono zaidi na kundi la Islamic State ADF imekuwa ni jeshi hatari zaidi ambalo linaendelea kutoa tishio kwa Uganda.
Katika msako wake kufuatia mashambulizi ya wiki jana, serikali imewakamata zaidi ya watu 100 na kuwaua washukiwa saba. Walakini, pamoja na watu kama Peter inajaribu pia kuwashawishi watu kutoka kwa maisha ya vurugu.
Alipokea kifurushi kidogo cha makazi mapya chenye thamani ya karibu dola $100 (£75) lakini hajapata chochote katika njia ya usaidizi wa kisaikolojia au urekebishaji. Pia ameona ni vigumu kupata kazi ya kawaida.
Mambo haya yanaweza kufanya iwe vigumu kwa mamlaka kusambaratisha mtandao wa wapiganaji katika siku zijazo.












