Siasa za Tanzania: Je! matamshi ya waziri Simbachawene wa Tanzania ya kudhibiti matumizi ya mitandao huenda yakadumaza uhuru wa kutoa maoni?

    • Author, Markus Mpangala
    • Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
  • Iliyochapishwa

Matamshi yaliyotolewa na Waziri wa mambo ya ndani nchini Tanzania, George Simbachawene kuwa 'Tanzania yanakusudia kuweka mfumo wa kudhibiti mijadala inayoendelea kwenye mitandao ya Kijamii na kuwachukulia hatua wale wote wanaotumia vibaya hususani Facebook,Instagram na 'Space' ya Twitter.

Mitandao hiyo inadaiwa kukusanya watu wengi na wakiachwa waendelee bila utaratibu wanaweza kuleta uvunjifu wa amani kwani wanakashifu viongozi", ni dhahiri yanakiuka mtazamo na msimamo wa rais Samia Suluhu Hassan ambaye mara kadhaa amehimiza wananchi kukosoa serikali, kuheshimu uhuru wa maoni pamoja matumizi chanya ya mitandao ya kijamii.

Licha ya Simbachawene kudai majukwaa hayo 'hutumika kukashifu viongozi' akiwemo rais Samia Suluhu Hassan, kwa upande mwingine amedhihirisha namna nyota ya nchi hiyo ya kurudisha nyuma demokrasia inavyong'ara kama ambavyo ripoti mbalimbali zinaonesha na kutengeneza utawala wa hofu miongoni mwa wananchi wake.

Pia agizo la waziri huyo kwa vyombo vya ulinzi na usalama ni kinyume cha Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Tanzania inayotoa uhuru wa watu kupata habari pamoja na msimamo wa serikali ya Rais Samia.

Akizungumza katika mahojiano na Mtangazaji wa kipindi cha Dira ya Dunia cha BBC, Salim Kikeke mnamo Agosti mwaka huu Rais alisema anasikiliza ukosoaji dhidi ya yake kwenye mitandao ya kijamii na wanachama wa upinzani na wanaharakati na kuongeza kuwa amezoea, lakini "inatusaidia kujua watu wanafikiri nini, ikiwa tutaipiga marufuku hatutakuwa na jukwaa hilo,".

Hali kadhalika katika mkutano wake na vijana jijini Mwanza, Rais Samia alisistiza matumizi ya mitandao hiyo katika kukosoa serikali yake.

Kadhalika alipohutubia Bunge la Tanzania mjini Dodoma April 22, 2021, aliwataka wabunge kuikosoa vikali serikali japo kwa lugha ya kibunge - kielelezo kuwa yupo tayari na anapendelea kukosolewa ili yeye na wasaidizi wake wajisahihishe na kuenenda katika njia nyoofu zaidi.

Hata hivyo, amri ya Simbachawene inaongeza ushahidi ambapo wananchi wameshuhudia vikwazo dhidi ya uhuru wa kukusanyika,siasa na maoni vinavyozidi kudhibitiwa na kuiweka nchi hiyo kati ya zile ambazo zinatoa nafasi finyu kwa wananchi wake kuwasiliana,kutoa maoni, kukusanyika kwa shughuli mbalimbali za kisiasa, jamii, uchumi na kadhalika.

Ikumbukwe ripoti ya Freedom House ya mwaka 2021 imebainisha kuwa Tanzania imeanguka kidemokrasia kwa kupata alama 34 kutoka asilimia 60 iliyopata mwaka 2016.

Nayo ripoti za World Press Freedom Index zimeonesha kuwa Tanzania inaporomoka katika uhuru wa habari kutoka nafasi ya 93 mwaka 2018 hadi nafasi ya 124 kwa mwaka 2021.

Kiini ni kuongezeka kwa masuala haramu

Inavyoonekana kwa sasa masuala haramu nchini Tanzania yanaongezeka. Masuala kadhaa yameharamishwa na kuifanya jamii nzima iwe inahangaika kutafuta namna ya kushiriki masuala muhimu yanayolindwa na Katiba.

Je ni masuala yapi yaliyoharamishwa nchini humo?

Kwamba kukosekana masuala yafuatayo ndiyo kiini cha kile ambacho serikali inahangaika leo kudai ni haramu na hivyo kutafuta mwanya wa kutengeneza utaratibu wa kudhibiti.

  • Kupigwa mafuruku mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa
  • Kuzuiwa makongamano ya kisiasa,wanaharakati na wananchi
  • Kuzuiwa mikutano ya ndani vyama vya siasa
  • Kupigwa marufuku na kuhamasisha maandamano kupitia mitandaoni ya kijamii
  • Vyombo vya habari kukumbana na kibano cha sheria hivyo kufinya uhuru wa habari
  • Mitandao ya kijamii kushughulikiwa kwa kile kinachoitwa usalama wa nchi kwa nia ya kutia hofu.
  • Upendeleo wa mikutano ya kisiasa kati ya chama tawala na vyama vya upinzani na wanasiasa wa upinzani na chama tawala.

Wakati Katibu wa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu na Katibu mkuu wa chama tawala CCM, Daniel Chongolo wakitembelea mikoa mbalimbali ya Tanzania kwa nia ya kukutana na wanachama na kushiriki shughuli za kisiasa, kwa vyovyote hali hii haiwezi kupokewa vizuri na wananchi wengine kwa sababu inadhihirisha uwanja wa siasa haupo sawa.

Wananchi wanafahamu mikutano ya vyama vya NCCR -Mageuzi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ilivyoharamishwa.

Kongamano la umoja wa vijana wa Chadema, mikutano ya Umoja wa wanawake Chadema ni vitendo ambavyo vinaibua mashaka zaidi miongoni mwa wanachama na wafuasi wa vyama vya siasa vya upinzani, hali ambayo inatengeneza mitazamo hasi dhidi ya serikali iliyopo madarakani.

Akizungumza wakati wa kutimiza siku 100 madarakani Juni 26, 2021, Rais Samia alisema, "Kwa sasa mikutano iliyoruhusiwa ni ile ya ndani ikiwemo ya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu, wabunge wako huru kufanya mikutano ya hadhara kwenye maeneo yao,".

Je serikali inapaswa kufanya nini?

Je, mitandao ya kijamii ina faida gani kwa wananchi? Hilo ndilo swali la msingi ambalo linafaa kuijenga hoja hii.

Kwamba ni muhimu kutambua namna mitandao ya kijamii inavyonufaisha wananchi ili serikali isiwe inahangaika kutafuta 'vijisababu' vya kufungia (kama ilivyotokea wakati wa uchaguzi mkuu wa 2020), kudhibiti (kusababisha watu kutumia huduma ya progtramu maalum ya VPN). Zipo faida lukuki Faida za mitandao ya kijamii;

  • Kupanua wigo wa haki na uhuru wa kutoa maoni
  • Kupanua wigo wa haki na uhuru wa kuchagua
  • Kupanua wigo wa haki na uhuru wa kuabudu
  • Kupanua wigo wa haki na uhuru wa kuchangamana na wengine
  • Kupanua wigo wa haki na uhuru kwenda popote nchini bila kuvunja sheria
  • Kupanua wigo wa haki na uhuru wa kujiunga na chama chochote cha siasa
  • Kupanua wigo wa haki na uhuru wa kuanzisha chama cha siasa
  • Kupanua wigo wa haki na uhuru wa kupata elimu ya kiwango chochote kwa mujibu wa taratibu kupitia App mbalimbali
  • Kupanua wigo wa haki na uhuru wa kupata huduma za serikali kwenye tovuti kama vile afya kurasa za taasisi,wizara,wilaya,mikoa,kanda
  • Kupanua wigo wa haki na uhuru wa kumiliki ardhi bila kujali jinsia
  • Kupanua wigo wa haki na uhuru wa kulindwa na vyombo vya dola
  • Kupanua wigo wa haki na uhuru wa kufuatilia mapato na matumizi ya umma.
  • Kuwa njia ya kutoa huduma za biashara au kuuza bidhaa.

Kuzuia na kuleta vikwazo vya kukusanyika bado haviwezi kusaidia serikali kwa namna yoyote ile, badala yake watatengeneza ombwe zaidi.

Kwa sasa tarakimu za wapiga kura mtandaoni zimeongezeka zaidi walio kwenye mitandao ni kama wameteka mfumo wa habari kutokana na ombwe la habari nchini.

Ni kama watendaji wa serikali hawafahamu wafanye nini katika ulimwengu wa teknolojia, hivyo kujikuta wakijikabidhi shughuli ndogo ndogo za kudhibiti majukwaa ya mitandao ya kijamii ambako inapatikana kodi na mapato ya kutosha.

Muhimu ni kuhakisha viongozi ambao ni kwa hakika ni kioo cha jamii wafuate sheria kupongeza matumizi chanya ya mitandao ya kijami badala ya kutoa makaripio kila kukicha.