Matokeo ya uchaguzi Marekani 2020: Trump afungua mashtaka wakati njia ya ushindi wake ikiwa nyembamba

Chanzo cha picha, Getty Images
Donald Trump na Joe Biden wote kwa pamoja wanadai kuongoza katika uchaguzi mkuu wa Marekani wakati huu matokeo ya mwisho yakiwa mbioni kutolewa na pande zote mbili kudai kuchukua hatua za kisheria.
Kampeni ya Trump imekosoa mchakato wa kuhesabu kura katika majimbo muhimu ya Wisconsin, Georgia, Pennsylvania na Michigan.
BBC inatabiri kuwa Bwana Biden alishinda Michigan.
Vyombo vya habari vya Marekani vinatabiri kuwa amelinasa jimbo la Wisconsin.
Hakuna matokeo yaliyotolewa katika jimbo la Pennsylvania.
Kuongoza katika majimbo yote matatu muhimu kutampa ushindi Biden.
Bwana Biden hajatangaza kuwa ameshinda, lakini alisema kuwa ana uhakika alikuwa njiani kumshinda Donald Trump.
Kwa ujumla waliojitokeza kwenye uchaguzi wa siku ya Jumanne inaelezwa kuwa idadi kubwa kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 120 ambayo ni 66.9% imeelezwa na mamlaka za uchaguzi.
Bwana Biden alikuwa akiungwa mkono na wapiga kura milioni 70.5, idadi kubwa kuwahi kutokea katika historia ya uchaguzi nchini Marekani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Bwana Trump alipata kura milioni 67.2, kura milioni nne zaidi ukilinganisha na alizozipata mwaka 2016.
Mbio hizi za uchaguzi zimetawaliwa na janga la virusi vya corona, ambapo nchi hiyo imeshuhudiwa ikirekodi maambukizi ya juu kiasi cha watu 103,000 walioambukizwa nchini humo siku ya Jumatano, kwa mujibu wa mradi wa kufuatilia mwenendo wa ugonjwa Covid-19 nchini humo.
Kampeni zinasema nini?

Chanzo cha picha, Getty Images
Siku ya Jumatano mchana, Bw. Biden aliwaambia wanahabari huko Wilminton, Delaware: ''mchakato wa kuhesabu kura ukikamilika tunaamini tutakuwa washindi.''
Aliongeza: ''Nitaongoza kama rais wa Marekani. Urais si taasisi ya washirika wa chama.''
Mshindani wa Democratic amesema ''alikuwa akijisikia vizuri sana'' kuhusu Pennsylvania, ingawa kampeni ya Republican ya Bw.Trump ''imedai ushindi'' katika jimbo hilo.
Mkuu wa kampeni ya Trump Jason Miller amesema: ''Mpaka mwishoni mwa juma hilo itakuwa wazi kwa taifa zima kuwa Rais Trump au Makamu wa rais Pence watachaguliwa kwa miaka mingine minne.
Trump bado anaweza kushinda?

Chanzo cha picha, Getty Images
Biden yuko mbioni kunyakua kura 270 zinazotakiwa kunyakua kiti hicho cha urais. Democrat wanakura 243, wakati Republican ikiwa na 214.
Katika uchaguzi wa Marekani, wapiga kura huamua katika ngazi ya majimbo kuliko ngazi ya taifa. Kila jimbo la Marekani hupata namba ya kura kutokana na idadi ya watu ndani ya majimbo hayo na kuna jumla ya mpaka kura 538 za kunyakua.
Ikiwa Trump atapoteza Wisconsin, lazima ashinde Georgia kwa (kura 16), North Carolina (15), Pennsylvania (20) na moja kati ya Arizona (11) au Nevada (6) ili kulinda kiti chake.
Rais anaongoza kwa alama moja katika majimbo yote mawili ya North Carolina na Georgia na wagombea hawa wawili wamekuwa wakichuana vikali katika jimbo la Nevada.
Bado kambi ya Trump ina matumaini kuwa inaweza bado kunyakua Arizona.
Kuna changamoto gani kisheria?

Kampeni ya Trump imesema rais atapeleka ombi rasmi kutaka kurudia kuhesabu kura katika jimbo la Wisconsin , wakieleza ''dosari katika kaunti kadhaa za jimbo hilo''.
Pia wanalalamikia jimbo la Michigan wakitaka kuahirisha zoezi la kuhesabu kura kwa sababu walikataliwa ''kuingia'' kushuhudia kufunguliwa kwa kura na kuhesabu kura hizo.
Makundi ya watu yamenaswa kwenye video wakiimba ''acha kuhesabu'' nje ya jengo ambalo kura zimekuwa zikihesabuwa mjini Detroit, Michigan.
Polisi walisambazwa kulinda jengo hilo wakati waandamanaji walipokita kambi nje wakitaka kuruhusiwa kufuatilia mchakato wa kuhesabu kura.
Taarifa za vyombo vya habari vya Detroit zinasema kuwa tayari kulikuwa na watu 200 waliokuwa ndani wakifuatilia mchakato huo.

Chanzo cha picha, Reuters
Pia kampeni ya Trump imefungua mashtaka mawili katika jimbo la Pennsylvania kusitisha shughuli za kuhesabu kura ''mpaka kutakapokuwa hali ya uwazi''.
Rais anaongoza kwa alama tatu katika jimbo la Keystone, lakini bado maelfu ya kura yanaendelea kuhesabiwa.
Huko Georgia Trump ametaka kusitishwa kwa uhesabuji kura.
Kampeni ya Trump imesema kuwa waangalizi wa kura za Republian katika jimbo hilo la kusini walishuhudia kura 53 zilizochelewa kuongezwa kinyume cha utaratibu katika kura za kaunti ya Chatham.












