Waridi wa BBC: Nilipenda kunywa pombe kiasi cha kuuza milango ya nyumba yangu kukidhi kiu

Chanzo cha picha, Caroline Kagia
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
Caroline Kagia anakumbuka vyema alivyotumbukia kwenye uraibu wa pombe akiwa msichana mdogo.
Alikuwa ametimiza miaka 18, hivyo kisheria alikuwa mtu mzima. Lakini moyoni mwake, alikuwa hajiamini hata kidogo.
Kagia alidhani pombe ingemsaidia kumuongezea ujasiri lakini badala yake alijipata ameongezewa utumwa ambao baadaye alipambana nao kwa zaidi ya muongo mmoja.
Kabla ya kujinasua katika uraibu huo, alikuwa nusura apoteze maisha yake mara kadhaa.
Ilikuwaje mpaka akaingia kwenye uraibu huo?
Caroline alikuwa mtoto mpole na mwenye kuona haya mbele ya watu.
"Upole ulinitia hofu, nilikuwa naogopa watu mno," anasema.
Baada ya kujiunga sekondari, Caroline alipata rafiki ambaye ni mvuta sigara na pia alikuwa anakunywa pombe.
Mambo haya kwake Caroline yalikuwa ni mageni mno kwani yeye alilelewa mno katika misingi ya kidini.
Wazazi wake muda wote walisisitiza nidhamu ya hali ya juu. Naye Caroline alikuwa muigizaji mzuri akiwa karibu na wazazi wake, lakini alijivunia uhuru wake faraghani.
Rafiki yake ndiye aliyemhamasisha na mwishowe kumpa chupa ya mvinyo.
Walibadilishana mawazo na mwishowe akafuata ushauri wa rafiki yake huyo kwamba asubiri wazazi wake walale kisha anywe 'kwa raha zake' akiwa chumbani.
"Kileo changu cha kwanza kilikuwa chupa ya mvinyo (Redwine) yenye ujazo wa 250ml.
Hii ni pombe yenye nguvu ya asilimia 12 ," anakumbuka Kagia.
Kutokana na simulizi alizokuwa amezisikia kutoka kwa marafiki zake, alihisi kana kwamba kinywaji hicho hakikutimiza matarajio yake.
"Sikulewa au kuonyesha dalili zozote za ulevi " anakumbuka Caroline.
Mwili wake ulikuwa na uwezo wa kihimili makali ya pombe.
Anapoyatazama maisha yake ya wakati huo, Caroline anaamini hilo lilifaa kuwa onyo kwake.

Chanzo cha picha, Caroline Kagia
Caroline anakiri kuwa marafiki aliokuwa nao wakati huo walifanya iwe rahisi kwake kunywa pombe na kufurahia.
Ila nyumbani hawakuwa na habari kuwa binti wao alikuwa ameanza ulevi.
Baada ya muda Caroline alipata fursa ya kwenda masomo nje ya nchi, barani Asia.
Maisha hayakumwendea vizuri kama wazazi wake walivyokusudia, kwani aliendeleza ulevi wake barabarani na masomo kuwekwa kwenye kiti cha nyuma.
Matarajio ya wazazi wake yalikuwa kuwa angesoma na kupata shahada ambayo ingemuwezesha kupata kazi kwa haraka akirejea nyumbani Kenya.
Baada ya muda wa mwaka mmoja Caroline alimpigia babake simu na kumweleza kuwa mazingira ya nchi aliyokuwa ni magumu na kwamba ameshindwa kukamilishia masomo kule.
Wazazi wake walikubali arudi. Wakati huo tayari alikuwa mraibu wa pombe ila bado wazazi wake hawakufahamu hilo. Ila walichogundua ni kuwa muonekano wake ulikuwa umebadilika kinyume na alivyokuwa zamani.
Caroline anasema kuwa kama kifungua mimba katika familia yake wazazi wake walimwamini mno, na waliamini karibu kila alichowaambia.
Caroline alimaliza masomo yake ya uandishi wa habari katika chuo kimoja nchini Kenya na muda sio muda akapata ajira na kuanza maisha rasmi.
Bi Caroline anasema kuwa hali ilikuwa mbaya sana, kwamba siku ambazo hakunywa kilevi au kuvuta sigara, alihisi kana kwamba alikuwa anapoteza ufahamu.
Anasema kuwa wakati mwingine alishikwa na hali ya kifafa kutokana na kuwa na pombe nyingi kwenye mwili wake, na kukosa pombe siku iliyofuata.
"Kwa kuwa nilikuwa nimeanza kunywa pombe kila siku mara nyingi nilikuwa nikijifungia nyumbani kwangu. Nilichukia kushirikiana na watu kwa sababu nilihisi walikuwa wananihukumu," anasema.
Aliongeza "Siku ambazo nilikunywa pombe, nilihisi mwenye furaha sana."
Licha ya uraibu wake anakiri kuwa haya yote pia yalikuwa kama njia ya kubana maumivu na fujo ambazo zilikuwa zimezingira maisha yake.

Pombe adui wa kazi
Caroline alifanya kazi katika kampuni moja ya uuzaji. Katika fani yake alikuwa miongoni mwa wafanyakazi waliobobea.
Kwa miaka 10 kutoka 2006-2016.
Siku zote alijizatiti kufanya kazi yake na kuwa hodari kuliko wote. Lakini wakati ulevi ulipoanza kumnyemelea, alianza kuwa na matokeo mabaya kazini.
"Sikuweza kutimiza malengo yangu katika mauzo kwa sababu sikuwa nikikutana na wateja. Nilikuwa kwenye baa kila wakati kutoka saa nne asubuhi, lakini
ningewadanganya wakubwa wangu kupitia maandishi juu ya mikutano yangu ya siku hiyo na kujitokeza siku inayofuata kazini na hadithi za huku na kule," anakumbuka Caroline.
Mwanadada huyu aliishia kuacha kazi, bila kufukuzwa.
Vituko kutokana na ulevi
Katika hali ya kuwa mlevi, mwanamke huyu alifanya vitimbi na vituko vingi mno anakiri kuwa alikuwa na tabia ya kuwaacha watoto wake wakiwa wamelala usiku na kuingia kwenye vyumba vya ulevi hadi usiku wa manane.
Cha ajabu pia anadokeza kuwa wakati mwingine angeingia kwenye kilabu ambapo hakujua hata mtu mmoja, bila pesa mfukoni, akitumai mtu atalipia vinywaji vyake.
Siku kama hizo angepoteza vitu vya thamani alivyokuwa navyo.
"Viatu vyangu vilichukuliwa kwa sababu sikuweza kulipia vinywaji vyangu. Niliwahi kufungiwa kwenye baa kwa siku nne kwa sababu sikuweza kulipia vinywaji vyangu.
Siku ambayo mmiliki wa baa aliamua kunipeleka kituo cha polisi, nilipata njia ya kutoroka na sikuonekana tena katika eneo hilo," Bi Caroline anakumbuka.
Vituko vengine vya uraibu huu wa pombe ni pamoja na kumhadaa muhudumu wa baa na kumpa kifaa cha kujazia moto simu ambacho kilikuwa bandia, kujifanya kana kwamba niliingia chooni na huyo akapotea na bili ya malipo.
Wakati fulani anakumbuka kuwa aliuza vitu vyake vya nyumbani ili kuendeleza tabia yake, pamoja na milango ya nyumba.
Msimu wa mabadiliko
Kukurukakara na vitimbi za unywaji wake, vilimfanya atamani mabadiliko.
Vilevile watoto wake wawili walikuwa waamtia hofu mno kuwa wataingia kwenye ufahamu wa mambo na kumjua mama yao kama mlevi wa kipindukia.
Haya ni baadhi ya mambo yaliyomfanya mwanadada huyu atamani kuishi bila kunywa pombe.
Anakiri kuwa alihisi kama mfungwa na mwanamke ambaye alikuwa hana muongozo wa kutoa kwa watoto wake .
Caroline alijua alikuwa na shida kubwa mnamo Novemba 2015 baada ya kuvunjika kwa uhusiano wa kimapenzi uliokuwa na dhuluma.
Ni uhusiano ambao ulikumbwa na ugomvi na vita vya kila mara.
"Nilipunguza uzito haraka sana na nilivaa suruali mbili ili tu kuonekana kama nilikuwa na nyama kwenye mifupa yangu. Sikuweza kufikiria au hata kuongea bila pombe katika mfumo wangu," anasema.
"Mnamo Januari 2017, mwishowe nilisema tosha, na nikachukua uamuzi kwamba ilikuwa wakati wa kubadilika na kurudisha maisha yangu kuwa yenye mwelekeo."
Caroline alieleza wazazi wake kuwa alitamani apelekwe chumba salama ambapo walevi husaidiwa kuacha uraibu huo.
Wazazi wake walimwamini na hapo hapo akapelekwa kwenye taasisi mmoja ambapo alikaa kwa miezi 6.
Alipotoka kwenye kituo hicho, alikuwa amebadilika.
Alitaka kuanza maisha upya
Kipindi alichokuwa anakunywa pombe uhusiano wake na watu wa karibu wa jamii yake ulizorota.

Chanzo cha picha, Caroline Kagia
Kwa mfano mtoto wake wa kiume alishuhudia vitimbi vingi mno kutoka kwa mamake nyakati za ulevi wake . Caroline anasema kuwa ilibidi amuite na kumuomba msamaha.
Kipindi cha msamaha na mabadiliko anasema kuwa
kilikuwa na machozi mengi mno kwa kujutiahali aliyowaweka watoto wake na watu wa familia yake.
Caroline anasema kuwa barabara ya uponaji inachukua nguvu na kujitolea kwingi.
" Ninaamini nilivutiwa na pombe kwa sababu nimekuwa nikipambana na hali ya kutojithamini tangu utotoni. Mimi ni mzaliwa wa kwanza katika familia ya ndugu watano, Pamoja na haya yote, nilikuwa na hali ya kujiona mtu wa chini.
Wenzangu wa shule wangeniita "sura mbaya " nikiwa katika shule ya msingi. Singejitolea kamwe kushiriki katika shughuli yoyote kwa sababunilihisi kukosa uwezo, na hata nyakati ambazo nilijitolea kufanya kitu, nisingechaguliwa. " Caroline anasema.
Msaada wa baba
Wazazi wake Caroline Kagia walisimama na yeye katika safari ya kubadilika kwake.
Caroline anazungumzia mchango wa baba yake katika kubadilika kwake.
"Katika safari yangu ya kupona baba yangu alikataa kabisa kuniacha. Aliendelea kuniangalia, kuniombea na kuzungumza mazuri juu ya maisha yangu.
Baba yangu alibadilisha hatima yangu kupitia upendo wake usioyumba na usiokoma.
Caroline anasema kuwa baba mzazi alizidi kumpenda na hata wakati alijichukiamwenyewe kwa kujiona kuwa mwovu sana na kutofaulu vile."
Anasema baba hakumlaani kamwe lakini kila mara alimbariki kwa maneno yake.
Na daima Caroline anasema: "Nguvu ya ulimi ni ya kweli. Bila msaada mzuri, ni rahisi kurudi tena. Uraibu ni ugonjwa kama mwingine wowote, na unapaswa kutibiwa kama hivyo. Inawezekana kwa mraibu kupona kabisa lakini tu katika mazingira sahihi na kwa Msaada sahihi."
Kwa sasa Caroline Anazungumza juu ya juhudi zake za kuwawezesha wale ambao ni mateka wa pombe na kuelimisha jamii zao jinsi ya kuwapenda na kuwakubali.












