"Kwanini hutaki kuwa mwanamke aliyefanikiwa maishani, badala tu ya kuwa aliyeolewa na fulani pekee?"

Chanzo cha picha, Getty Images
Mary Cholhok anaangazia jinsi alivyofanikiwa na kuwa mchezaji wa netiboli wa kulipwa katika klabu ya Loughborough Lightning nchini Uingereza licha ya changamoto alizopitia.
Ni nyota mchezaji wa pili wa kulipwa wa mpira wa netiboli, 23, kutoka Uganda anayetaka kuwapa moyo vijana wa kike kufuata nyayo zake.
"Kukua ukiwa msichana ni changamoto kubwa kila nchi hasa Afrika, kwa sababu kuna baadhi ya utamaduni na mila tunazofuata kama wasichana," amesema.
"Kuna baadhi ya tamaduni kama vile ndoa za mapema, na kwasababu ya hilo, hupati muda wa kutosha wa kuwekeza kwenye michezo au kile unachotaka kufikia kitaaluma.
"Kuna wasichana wengi ambao hawana ufahamu kwamba wanapitia changamoto. Ni lazima ifikie wakati waanze kufungua macho yao."

Chanzo cha picha, Mary Cholhok
Familia ya Cholhok ambayo asili yake ni Sudan Kusini ilitoroka nchi hiyo kwa sababu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na ukosefu wa uthabiti wa kisiasa ilianza kutafuta kuanza maisha mapya baada ya kifo cha baba yao.
Akiwa na urefu wa futi 6 na nchi 7, Cholhok alijipata akiwa mchezaji mzuri wa netiboli na kuchukulia mchezo huo kama njia moja ya kufikia kitu chenye tija maishani mwake.
Mama yake na mjomba wake kwa upande wao ililazimika washawishiwe.
"Hawakuwa na raha sana kuhusu hilo, walihisi kana kwamba ni kitu ambacho kitanitatiza na kuathiri masomo yangu, kwahiyo kidogo walikuwa na msimamo mkali kuhusu hilo. Wakati mwingine ningetoroka ili nikacheze na kujitahidi kuweka uwiano kwa yote mawili.
"Inafikia wakati, mtu anagundua kile anachoweza kufanya kwa weledi zaidi akiwa na umri fulani au kiwango fulani kwahiyo nikaamua kusalia kwenye mchezo huu kwasababu nilihisi nina fursa ya kupata ufadhili wa masomo kupitia michezo."
Ndoto hiyo ya Cholhok ilionekana kudidimia pale alipopata ujauzito akiwa bado shule ya upili na kuanza kumlea mtoto wake kama mzazi mmoja.
Shinikizo la kuachana na mchezo wa mpira wa netiboli kulimfanya kuwa imara zaidi na kuwa na malengo ya kutaka kufanya kitu cha kipekee kwa ajili ya maisha yake na yale ya kijana wake Yasson.

Chanzo cha picha, Mary Cholhok
"Nikipata mtoto nilikuwa na umri wa miaka, 20 nilihisi… kama maisha yamefika mwisho. Kwa hiyo nikajitahidi kutokufa moyo, nikawajibika na kuwa mama na pia kufikiria hatma ya kijana wangu.
"Wengi walikuwa wanasema, 'oh, unahitajika kuwa na kijana wako', lakini ikiwa nitafanya hivyo na kushindwa kupata shahada yangu, nikishindwa kutimiza ndoto yangu ya kuwa mchezaji wa kulipwa wa netiboli na kufikia kitu cha manufaa maishani mwangu, nitamuonesha nini?
Kwa mfano, 'Kijana wangu, niliamua kukosa moja ili nipate jingine'."
Lakini kujinyima kwake kunaonekana kulipa.
Wakati ambapo mtoto wake wa miaka mitatu anatunzwa na bibi yake katika mji wa Kampala, nchini Uganda, ameenda Uingereza na kujiunga na timu ya Loughborough Lightning mwaka 2018 wakati huohuo, akiwa anasomea shahada ya biashara.
Alimaliza msimu wake aliojiunga na timu kama mfungaji bora na kilichofuata alishiriki mchezo wa netiboli wakati wa Kombe la Dunia huko Liverpool mwaka jana.
Mwaka huu, baada ya kutokea kwa janga la virusi vya corona, ligi yake iliahirisha mchezo baada tu ya wiki nne.

Chanzo cha picha, Mary Cholok
Akiwa na hofu kwamba huenda akasambaza virusi vya corona, aliamua kutorejea Uganda ambayo baadae ilifunga mipaka yake na Uingereza.
"Ilikuwa jambo la hisia kufungiwa ndani peke yangu, anasema.
"Ilinichukua muda sana kufikiria kwamba nina virusi vya corona kumbe niko sawa. Kipindi hicho kila mmoja alikuwa amechanganyikiwa.
"Nilihisi kuishiwa na matumaini, kwasababu kila wakati alikuwa anauliza, 'Mama, unakuja lini, Tutafanya hivi na vile'.
Hilo lilinifanya kuwa na hisia sana kama mama."
Lakini wakati hayuko karibu na familia yake na pia hawezi kushiriki majukumu mingine, aliamua kuanza kuangazia mambo mengine kama kuendesha baiskeli, kufanya mazoezi ya kupiga gitaa na kutia wengine moyo kupitia Zoom.

Chanzo cha picha, Mary Cholhok
"Cholhok anakubali kwamba mara ya kwanza alikuwa na chagamoto kuzoea maisha ya Loughborough, hasa upande wa chakula na hali hewa, lakini alifurahia sana akiwa uwanjani.
"Mara nyingi, maisha yetu huusiana kwa karibu na michezo na wanapokosa kushiriki michezo yao kuna wale wanaoshindwa kabisa kujidhibiti kimaisha na hata kupata matatizo ya akili.
"Sasa hivi nahisi kana kwamba nimefanikiwa kudhibiti mengi maishani mwangu, kile ninachofanya, kile ninachofanikiwa, shahada yangu, ikiwa nitafanikiwa maishani mwangu itakuwa jambo bora sana maishani mwangu."













