Ufilipino: Hasira juu ya kifo cha mtoto aliyetenganishwa na mama yake aliyefungwa jela

Chanzo cha picha, Kapatid
Kifo cha mtoto wa miezi mitatu aliyetenganishwa na mama yake licha ya wito uliotolewa wa kutowatenganisha umewashangaza wengi huko Ufilipino, mwanahabari wa BBC Preeti Jha amesema.
Reina Mae Nasino, mfanyakazi wa shirika la haki za binadamu, hakujua kwamba ni mjamzito alipokamatwa na polisi mwaka jana huko Manila.
Alidhania kwamba kukosa siku zake za hedhi kumetokana na msongo wa mawazo aliopata wakati polisi walipomvizia na kumkamata pamoja na wanaharakati wenzake wawili.
Lakini wakati anafanyiwa vipimo akiwa gerezani hapo ndio mwanahakati huyo, 23, alipobaini kwamba ni mjamzito.
Kifo cha mtoto wa Bi. Nasino wiki iliopita - chini ya miezi miwili baada ya mtoto wake kuchukuliwa na mamlaka - kumezua maswali mengi kuhusu vile wanawake wa Ufilipino waliopo gerezani wanavyochukuliwa huku wengi wakipaza sauti zao dhidi ya mfumo wa haki kwa kushindwa kumhakikishia mtoto huyo usalama.
Changamoto ya kujifungua
Bi. Nasino, ambaye anafanyakazi na kundi la Kadamay la kukabiliana na umaskini maeneo ya mjini, alikamatwa Novemba 2019 na wanaharakati wenzake wawili baada ya polisi kuvamia ofisi ambayo wakati huo walikuwa wanaishi.
Walishtakiwa kwa makosa ya umiliki wa silaha kinyume cha sheria pamoja na kupatikana na vilipuzi ingawa wote watatu wamekanusha madai hayo.
Wanasema kwamba silaha hizo ni njama ya mamlaka huku kukiwa na kamakamata dhidi ya wanaharakati wanaoegemea mrengo wa kushoto.
Licha ya yaliotokea, Bi. Nasino "alikuwa na furaha sana ya kuwa mama", wakili wake Josalee Deinla alisema. Alikuwa amejitayarisha kukabiliana na changamoto ya kujifungua akiwa kizuizini na alifahamu kwamba kuna uwezekano mkubwa michakato ya kisheria ikachukua muda mrefu.
Lakini vile janga la ugonjwa wa corona lilivyo athiri Ufilipino, wasiwasi wake uliendelea kukua tena kwa haraka. Chama cha taifa cha Mawakili, ambacho kilikuwa linamwakilisha Bi.Nasino, kiliwasilisha hoja zao mfululizo kikitaka aachiliwe huru.
Mara ya kwanza mnamo mwezi Aprili, chama hicho kilitaka kuachiliwa huru kwa muda kwa wafungwa wa kisiasa 22 walio katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya virusi vya corona ikiwemo Bi. Nasino.
Baadae, kilitaka mahakama kumruhusu mwanaharakati huyo na mtoto wake kuishi pamoja hospitali au gerezani alikozuiliwa.
"Tulishtuka kuona mahakama ikikataa ombi kama hilo. Alichohitajika kufanya hakimu ilikuwa ni kuiangalia hoja hiyo kwa mtazamo wa ubinadamu.
Lakini kwa bahati, huruma na rehema haikuzingatiwa kwa mama huyo na mtoto wake," amesema Bi. Deinla.
Maombi ya kuachiliwa huru
River Masino alizaliwa Julai mosi. Uzito wake ulikuwa wa chini lakini baada ya siku chache mtoto pamoja na mama yake walirejeshwa katika jela ya mji wa Manila walikoishi kwenye chumba cha kubadilishana zamu kwa wahudumu.
Chini ya sheria ya Ufilipino mtoto anayezaliwa kizuizini anaweza kusalia na mama yake kwa mwezi wa kwanza tu baada ya kuzaliwa, ingawa mipangilio mingine inaweza kufanyika.
Kwa ulinganisho, watoto waliozaliwa na kina mama waliofungwa gerezani nchini Malaysia wanaruhusiwa kusalia nao hadi umri wa miaka mitatu hadi minne.
Uingereza, vyumba vya mama na mtoto vinawezesha kina mama kusalia na watoto wao wachanga hadi watakapotimiza miezi 18.
Wanaharakati waliendelea kushinikiza mamlaka kumuachiliwa huru Bi. Masino na mtoto wake.
"Tungefunga utepe wa buluu kwenye milingoti ya milango ya mahakama ya juu zaidi. Walisimama na River.
Tuliweka mishumaa nje. Lakini hawakusikiliza," amesema Fides Lim, mkuu wa chama cha Kapatid, kundi la familia na marafiki wa wafungwa wa kisiasa nchini Ufilipino.

Chanzo cha picha, Kapatid
Mama yake Nasino, akisaidiwa na chama cha Kapatid, pia aliwasilisha picha na barua kwa mamlaka karibu kila wiki, akiomba mtoto wake aachiliwe huru.
"Tulijua umuhimu uliokuwepo wa mtoto River kunyonyeshwa," amesema Bi. Lim, ambaye pia amekuwa akishiriki kampeni ya kutaka kuachiliwa huru mara moja kwa mume wake mfungwa wa kisiasa, 70.
Hospitali ambayo Bi. Nasino alijifungua ilipendekeza mtoto huyo asitenganishwe na mama yake, amesema wakili Nasino, Bi. Deinla. "Lakini usimamizi wa gereza umesema ulikosa raslimali. Walitafuta visingizio vingi, na kukiuka haki ya mtoto kwa mama yake ya kunyonya maziwa ya mama," alisema.
Chini ya "Sheria za Bangkok" - Miongozo ya Umoja wa Mataifa kuhusu tiba ya wafungwa wanawake - uamuzi wa ni lini mama anatenganishwa na mtoto wake unastahili kuzingatiwa kwa maslahi ya mtoto.
BBC imewasiliana na mamlaka ya gereza ya Ufilipino ili kuzungumzia suala hili lakini bado haijapata jibu.
Utenganisho wa mama na mtoto
Agosti 13, mtoto River alitenganishwa na mama yake. "Hakutaka mtoto wake afariki, Bi. Deinla amesema. Alikuwa anaomba aruhusiwe kusalia na mtoto wake kidogo."
Kwasababu sheria za ugonjwa wa Covid-19 zilizuia wafungwa kutembelewa, Bi. Deinla na wenzake wameweza tu kuendelea kuwasiliana na Nasino kupitia simu.
Afya ya mtoto River ilianza kudorora mwezi uliofuata, kulingana na Bi. Lim.
Inasemekana kwamba mtoto huyo hatimae alikabidhiwa bibi yake baada ya kuanza kuhara.
Wito wa kumuunganisha mama na mtoto wake ulishika kasi zaidi pale mtoto River alipolazwa hospitali Septemba 24 na hali yake kuanza kuwa mbaya. Lakini bado Bi. Nasino hakuruhusiwa kumuona mtoto wake.
Wiki iliyopita, mtoto River alifariki dunia kwa homa ya mapafu na kifo chake kilishtua wengi nchini Ufilipo ambako risala za rambi rambi zimekuwa zikimiminika kwenye mitandao ya kijamii.
Aidha, wengi pia wameonesha hasira na kutoridhishwa na mfumo wa sheria, huku wengine wakilinganisha kuachiliwa huru kwa msamaha kwa baharia wa Marekani hivi majuzi aliyeshtakiwa kwa kumuua mwanamke aliyebadilisha jinsia yake nchini Ufilipino na hatua ya mahakama ya kukataa kumruhusu Bi. Nasino kumuona mtoto wake.

Chanzo cha picha, Kapatid
Wengine wamekuwa wakilinganisha vile wanaharakati vijana wanachukuliwa ikilinganishwa na watu wa ngazi ya juu na wafungwa matajiri ambao wameruhusiwa kuachiliwa huru kwa muda kuhudhuria matukio kama vile harusi za watoto wao au watoto wao wanapohitimu.
Jumanne, mahakama ya eneo ilimruhusu Bi. Nasino kuachiliwa huru kwa siku tatu kuhudhuria mazishi ya mtoto wake.
Lakini baada ya maafisa wa gerezani kuingilia kati kupunguza siku za kuachiliwa kwake, aliruhusiwa tu kuondoka gerezani kwa saa tatu Jumatano na Ijumaa siku ya mazishi ya mtoto River.












