Siku ya Wanawake Duniani: Jinsi wanawake wa vijijini wanavyoweza kubadilisha jamii kiuchumi wakiwezeshwa

    • Author, Aboubakar Famau
    • Nafasi, BBC Africa, Tanzania
  • Iliyochapishwa

"Maisha yangu yalikuwa magumu. Sikuwa na pesa ya chakula kwa ajili yangu na watoto wangu, sikuwa na pesa hata ya kununua nguo, nilikuwa natembea pekupeku bila viatu," anasema Tatu Hussein Sumbi, mkazi wa kijiji cha Mkimbii kilichopo wilayani Singada, nchini Tanzania.

Mwandishi wa BBC Aboubakar Famau pindi walipokutana kijijini humo, ni dhahiri kwamba Tatu hakuwa pekee yake katika hali hiyo.

Na mara nyingi wanawake wa vijijini wanakosa nyenzo za kuwawezesha kujikimu kimaisha.

Lakini Tatu, mwenye umri wa miaka 40 anasema hakuridhishwa na hali yake, alikaa chini akajitafakari na hatimae akaamua kuchukua hatua ambayo hivi leo haijutii.

"Miaka ya nyuma nilikuwa nakaa tu nyumbani sijishughulishi na kitu chochote. Uchumi ulikuwa mgumu, nilishindwa namna ya kusomesha watoto, nilishindwa hata kununua nguo, nikiangalia hivi, nasema uchumi nitaupataje, mbona nakaa nyumbani tu,"anasimulia Tatu.

Lakini Tatu, 2019 ulikuwa ni mwaka wa mabadiliko.

Alijiunga na vikundi vya wanawake ambavyo viliundwa kwa msaada wa Shirika la Helvetas vililenga kutoa mafunzo ya kilimo hai hasa katika zao la pamba, lakini pia kuwafundisha wanawake jinsi ya kufanya biashara, kuweka akiba na hatimae kukopeshana.

"Mwaka 2019 nikatoka kwenye vikundi. Hapo nikaona mwanga. Nikapeleka hisa zangu kwenye vikundi, najishughulisha, naweka hisa zangu, nakopa hizo hela, nanunua vidagaa vyangu, napeleka kwenye masoko, najishughulisha napata hela, nikipata hizo hela naweka akiba na matumizi ya familia yangu," amesema Tatu, ambae sasa hivi, kupitia ukulima wa viazi lishe.

Hapo ndio Tatu alipoanza kuona matunda ya jitihada zake.

Tatu, mama wa watoto 8 hivi sasa amekuwa ni wa kupigiwa mfano kijijini kwao.

Kupitia vikundi hiyo, akishirikaiana na mume wake, hivi sasa wamejenga nyumba ya tofali, lakini pia wameongeza kipato cha familia kwa kununua ng'ombe wa maziwa wa kisasa na kuku.

Ingawa vikundi hivi ni kwa ajili ya wanawake pekee, lakini wanaume nao hawajaachwa nyuma. Katika kila kundi la wanawake 40, kuna idadi ndogo ya wanaume.

Hata hivyo, ushirikishwaji huu wa wanaume unaonekana kuleta tija.

Kwanza umewafanya kina baba kujua kinachoendelea pindi wake zao wanapokuwa hawapo majumbani, aidha wanapokua katika vikundi au mashambani, lakini pia, imetoa hamasa kwa wanaume kuwaruhusu wake zao kushiriki vikundi hivyo.

"Nimeona ni muhimu mke wangu kujiunga na vikundi, kwa sababu kuna unafuu ninaoupata, hata maisha yangu yanaenda vizuri, kwa sababu akichukua hisa kuna mambo yananisaidia, tumeweza kujenga na kununua ng'ombe," anasema Issa Shabani, mume wa Tatu Hussein.

Habiba Salim Kilee ambae pia ni mwanakikundi nae alijawa na bashasha pindi aliponikaribisha katika bomba lake ambalo lilikuwa na nyumba kadhaa za tofali, zizi la ng'ombe na kuku wa kienyeji wakirandaranda katika boma.

Aliolewa katika boma la wauza pombe ya kienyeji, lakini hakukata tamaa.

Alianza kwa kujishughulisha na ukulima wa viazi lishe na hatimae kuanza kutengeza unga wa ulevi utokanao na viazi lishe.

Habiba alionekana kujawa na furaha pindi alipokuwa anazungumzia mafanikio yake ikiwa ni pamoja na kununua makochi mapya sebuleni mwake.

Kwa upande wake, Monica Ngimba ambae ni mratibu wa mradi huo kutoka Shirika la Helvetas anasema sio wote wanaoanza safari hii huikamilisha.

Anasema wengine wanaokuja na dhana ya kupata fedha za kupewa huishia njiani.

Mbali na kutoa elimu ya kuweka na kukopa, lakini pia kina mama hawa wamewezeshwa kwa kupewa masanduku ya kuhifadhi fedha ambayo ni kama benki ndogo.

"Sio kila mradi unakuja na vifaa. Tunawafahamisha kwamba chanzo cha pesa ni kutoka kwao wenyewe, aidha amelima pamba akauza, basi ile pesa itamsaidia, nyengine atatumia nyengine ataweka akiba," amefafanua Monica.

Pamba nyingi inayolimwa na kina mama hao ni kwa njia ya kilio hai na inanunuliwa na kampuni ya Bio Sustain Tanzania Ltd iliyopo mjini Singida.